The House of Favourite Newspapers

Serikali Ya DRC Yatangaza Zawadi Ya Shilingi Bilioni 13 Kwa Kukamatwa Kwa Viongozi Wa M23

Hali ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) inaendelea kuwa mbaya, huku serikali ikitangaza zawadi ya dola milioni 5 (Shilingi Bilioni 13) kwa yeyote atakayesaidia kuwakamata viongozi watatu wa kundi la waasi la M23. Corneille Nangaa, kiongozi wa Muungano wa Mto Kongo (Congo River Alliance), pamoja na viongozi wa M23, Sultani Makenga na Bertrand Bisimwa, wanatafutwa kwa uasi.

Serikali ya DRC inazidi kuishinikiza jumuiya ya kimataifa kuiwekea Rwanda vikwazo kwa madai ya kuunga mkono waasi hao. Ripoti ya Umoja wa Mataifa mwaka jana ilidai kuwa wanajeshi wa Rwanda wapatao 4,000 wanashirikiana na M23 ndani ya DRC. Rwanda, kwa upande wake, inakiri kusaidia M23 lakini inasema inafanya hivyo ili kuzuia mgogoro huo kusambaa hadi katika mipaka yake.

Katika juhudi za kupata msaada wa kijeshi, serikali ya DRC inadai kuwa imewaalika Wamarekani kununua madini moja kwa moja kutoka kwao badala ya Rwanda, ambayo inashutumiwa kwa kunyakua rasilimali hizo kwa njia haramu. Hata hivyo, nafasi ya kuwakamata viongozi hao wa M23 inaonekana kuwa ndogo, kwani waasi hao wameiteka miji mikubwa ya Goma na Bukavu huku jeshi la DRC likionekana kushindwa kuwazuia.

Mzozo huu unaendelea kusababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwafanya mamia ya maelfu kuyakimbia makazi yao.