The House of Favourite Newspapers

Serikali ya Japan Kuwalipa Waliohasiwa

MAELFU ya raia ambao walihasiwa bila ridhaa nchini Japan wameombwa radhi na serikali na wanatarajiwa kulipwa fidia.

 

Chini ya Sheria ya Kulinda Vizazi ambayo ilitekelezwa na mamlaka nchini humo kwa takribani miongo mitano, maelfu ya watu walihasiwa ili kuzuia kuzaa watoto ambao ‘wangelikuwa dhaifu’.

 

Sheria hiyo ilitumika kwa miaka 48, kuanzia 1948 mpaka 1996, na iliwalenga watu ambao walikuwa na ulemavu wa viungo, akili, na matatizo ya kitabia.

 

Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe,  ameomba radhi kwa “maumivu makali” ambayo wameyapitia.

 

Chini ya sheri mpya ambayo imesainiwa leo Jumatano, Aprili 24 wahanga wote ambao wapo hai watalipwa yen milioni 3.2 sawa na dola 22,000.

 

Wengi wa wahanga walio hai kwa sasa walikuwa watoto wakati walipofanyiwa upasuaji wa kuhasiwa. Mtu aliyehasiwa anakosa uwezo wa kupata watoto.

 

Wahanga hao sasa wanatakiwa kuomba malipo ya fidia ndani ya kipindi cha miaka mitano. Maombi yao yatapitiwa na bodi ya wataalam kabla ya kulipwa.

 

“Katika kipindi ambacho sheria ile ilikuwa ikitumika, watu wengi walilazimishwa kufanyiwa upasuaji ambao umewafanya wawe wagumba kwa sasabu tu ya hali zao za ulemavu, ama maradhi sugu. Hali hiyo imewasababishia maumivu makali,” Abe amesema kwenye taarifa yake ya kuomba radhi.

 

“Kama serikali, ambayo tulitekeleza sheria hii, na baada ya kujitathmini kwa muda, napenda kuomba radhi kutoka moyoni,” alisema.

 

Takribani wahanga 20 wa sheria hiyo hivi sasa wanaishtaki serikali mahakamani na hukumu inatarajiwa kutoka mwishoni mwa Mwezi Mei.

 

Mwanamke mmoja ambaye ameshtaki serikali akitaka kulipwa fidia ya yen milioni 11 ($98,300), alihasiwa mwaka 1972 akiwa na miaka 15 baada ya kugundulika kuwa na matatizo ya kurithi ya akili ambayo hayaonekani kwa macho ya kawaida.

 

“Tulikumbwa na siku za masikitiko,” dada wa mawanamke huyo aliwaambia wanahabari mwezi Januari. “Tumenyanyuka ili kuifanya jamii hii kuwa bora.”

 

Sheria hiyo ilipitishwa mwaka 1948 wakati  Japan ilikuwa katika harakati za kujijenga baada ya Vita ya Pili ya Dunia.

 

Inaaminika kuwa watu 25,000 walihasiwa kwenye kipindi cha miaka 48 ya utekelezaji wake. Japo kuna kumbukumbu chache kuhusiana na utekelezaji wake, inakadiriwa watu 16,500 hawakuridhia kuhasiwa.

 

Operesheni hizo zilichupa miaka ya 1960 mpaka 1970, na kuendelea mpaka operesheni ya mwisho ilipofanyika 1993. Sheria hiyo ilifutwa mwaka 1996.

Comments are closed.