SERIKALI YA JPM KIBOKO… FAMILIA HII YAULA MIL. 343

FAMILIA ya Chacha Kiguha Babere inaweza kusema mvumilivu hula mbivu baada ya Mahakama ya Rufaa Tanzania kuuamuru Mgodi wa Dhahabu wa North Mara (Acacia) uilipe familia hiyo shilingi 343, 225, 000 kama fidia baada ya kushinda rufaa yao mahakamani hapo.  Awali familia hiyo ilishinda kesi kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania lakini uongozi wa mgodi huo ukaamua kukata rufaa katika mahakama hiyo ya juu nchini.

Hata hivyo, licha ya mahakama hiyo kuuamuru mgodi huo kuwalipa wanafamilia hao mwaka jana, haukutekeleza amri hiyo ya mahakama hivyo kusababisha Kampuni ya udalali ya jijini Mwanza iitwayo S.L.Isangi Auction Mart and Court Broker chini ya Richard Ojendo hivi karibuni kuupa notisi ya siku 14 mgodi huo wa kuilipa fidia familia hiyo.

Mgodi huo wa dhahabu wa North Mara uliopo Nyamongo, Wilaya ya Tarime mkoani hapa umepewa notisi ya siku 14, tangu Desemba 12 hadi Desemba 26, 2018 kupitia kampuni hiyo ya udalali uwe umetekeleza amri hiyo ya Mahakama ya Rufaa Tanzania. Kampuni hiyo kupitia notisi hiyo imeuonya mgodi huo kwamba iwapo hawatatekeleza amri hiyo ya mahakama ya juu nchini itakamata magari zaidi ya 32 waliyoyaorodhesha katika hati ya kukamata mali za mgodi huo ili kuyapiga mnada kulipia fedha hizo kwa familia hiyo.

Kampuni hiyo ya udalali ilikabidhi hati hiyo ya kuipa muda maalum wa kulipa mgodi huo kupitia ofisi ya meneja wa uhusiano wa mgodi mbele ya mdai na familia yake ya watu watano inayoongozwa na Chacha Kiguha Babere wa Kijiji cha Komarera, Kata ya Nyamwaga, siku ya Desemba 12 mwaka huu baada ya kuandaliwa kisheria Desemba 11 mwaka huu.

DALALI ANENA

Dalali Richard alisema, ametoa siku hizo kwa mujibu wa sheria inayomtaka kufanya hivyo kabla ya kufikia kukamata mali za mgodi huo ili kutoa nafasi ya kuilipa familia ya mzee Chacha (pichani) ambayo inaishi kwa mateso.

Wanufaika wengine wa amri hiyo ya Mahakama ya Rufaa Tanzania ni mke wa Chacha, Neema Chacha na watoto wao Bhoke, Kiguha, Motongori na Surati Chacha ambao kwa ujumla wao watalipwa shilingi milioni 343, 225, 000 kama fidia ya kuathiriwa kiafya kutokana na kuishi ndani ya mgodi huo katika leseni namba SML 17/96 ya mashimo ya Nyabigena na Gokona.

Malipo hayo yanatokana na ushindi wa kesi yao ya madai namba 9/2013 walioupata Agosti 3, 2016 dhidi ya mgodi huo ambapo ulitakiwa kuilipa familia hiyo ikiwa ni pamoja na gharama za kesi, hukumu hiyo ilitolewa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, Lameck Mlacha.

MKUU WA WILAYA APIGILIA MSUMARI

Pamoja na dalali huyo kuupatia mgodi huo siku hizo uwe umeilipa familia hiyo mamilioni hayo ya fedha, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, mkoani Mara, Glorious Luoga anayemwakilisha Rais John Magufuli eneo hilo aliutaka mgodi huo utekeleze mara moja madai ya familia hiyo vinginevyo dalali huyo afanye kazi yake kwa mujibu wa sheria.

Katika barua yake ya Desemba 13, 2018 aliyomuandikia mtendaji wa Kata ya Matongo na mkuu wa Kituo cha Polisi cha Nyamongo yenye Kumbukumbu namba AB.26/87/01A/41 ambayo gazeti hili lilifanikiwa kuiona, kiongozi huyo wa serikali aliwataka wahusika kila mmoja na kazi yake kuwezesha kusimamia na kutoa ushirikiano kwa dalali huyo kuweza kufanya kazi yake baada ya muda wa siku 14 kuisha ili haki itendeke.

Hii ni mara ya pili kwa mgodi huo kupewa notisi kwani awali kampuni ya Udalali ya Ubapa Court Broker iliyopo Musoma, mkoani hapa ilitoa notisi ya siku 14 iliyoanzia Machi 8 hadi 22 mwaka huu uwe umewalipa wanafamilia hao. Hata hivyo, mara baada ya dalali huyo kuwapa notisi hiyo, uongozi wa mgodi uliamua kwenda Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza na kuzuia ukamataji huo wa mali ambazo ni magari yaliyotakiwa kupigwa mnada hadharani.

Hatua hiyo iliifanya Mahakama Kuu ya Tanzania isikilize pingamizi ya mgodi huo dhidi ya familia ya Chacha Kiguha Babere na familia yake hiyo ambapo Msajili wa Mahakama Kuu hiyo hivi karibuni aliamua kuwa magari yaliyopo katika hati ya ukamataji na hukumu Namba 18/2016 ya kutoka Mahakama Kuu Tanzania iliyotokana na kesi mama namba 9/2013 ni halali na mali ya mgodi.

SHAURI NDANI YA MAHAKAMA YA RUFAA

Katika kesi hiyo ndani ya Mahakama ya Rufaa ya Tanzania, familia hiyo ilipewa ushindi baada ya majaji watatu kusikiliza rufaa ya mgodi huo Desemba 4 mwaka 2017 na kutoa uamuzi wake Desemba 12 mwaka 2017. Majaji walioipa ushindi familia hiyo ni Jaji Bernard M. Luanda, Jaji Bethuel M. Mmilla na Jaji Rehema K. Mkuye na nakala ya hukumu hiyo ilisainiwa na Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Elizaberth Y. Mkwizu.

TUJIKUMBUSHE

Rufaa hiyo ilitokana na mgodi huo kupinga ushindi iliyoupata familia hiyo Agosti 3, 2016 uliotolewa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza kutokana na kesi ya madai ya kuathiriwa kiafya na familia yake. Familia hiyo ilipatwa na madhara ya kiafya na mke wa Chacha kuharibikiwa na mimba ambapo watoto walipatwa na madhara ya ngozi kutokana na kuishi muda mrefu ndani ya mgodi huo bila kuhamishwa kisheria huku mgodi ukiendesha uchimbaji wa dhahabu bila kujali usalama wa afya zao.

Kutokana na hukumu hiyo, baadhi ya wananchi wameisifu Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dk John Magufuli kwa kuwajali wanyonge kama familia hiyo ya Chacha na kuisifu Idara ya Mahakama chini ya Jaji Mkuu Profesa Ibrahimu Hamisi Juma kwa kutenda haki. “Mlalahoi kama yule (Chacha) kushinda mpaka mahakama ya rufaa ni kielelezo tosha kwamba sasa hivi mnyonge haonewi,” alisema John Twaha, mkazi wa Tarime.

Aliongeza kuwa, kutokana na mdai huyo kushinda, wale ndugu waliomuona mjinga kwa kudai haki zake sasa wameanza kujipendekeza kwa kujua kuwa neema inakaribia na ikiwa watalipwa, basi watauaga umasikini.

KIONJO CHA MWISHO

Hata kama jukumu la kugawana fedha liko mikononi mwa familia hiyo inayotarajia kulipwa mamilioni lakini si vibaya kuweka kionjo hiki cha fikra juu ya nani ataambulia ngapi endapo wakiamua kugawana fedha hizo kwa usawa.

Hesabu zinaonesha kuwa milioni 343 zikigawanywa mara sita ambayo ndiyo idadi ya wanafamilia wanaofidiwa kila mmoja atajipatia kitita cha shilingi zisizopungua milioni 57; jiulize ungekuwa wewe ukazipata hizo tena ukiwa katika mazingira wanayoishi akina Chacha ungefanyia nini?

STORI: IGENGA MTATIRO, MARA


Loading...

Toa comment