The House of Favourite Newspapers

SERIKALI YADAKA MATAIRI VIMEO

DAR: Ama kweli Serikali hii haitaki mchezo, hivyo ndivyo unavyoweza kusema kufuatia wachapakazi wake kuingia mitaani na kufanya ukaguzi wa bidhaa mbalimbali ambapo Alhamisi iliyopita wakaguzi wa Shirika wa Viwango Tanzania (TBS) kwa kushirikiana na makachero wa Jeshi la Polisi walikamata matairi vimeo (yaliyokwisha muda wake) yakiwa kwenye bohari la duka la Gupta Auto Spare lililopo Barabara ya Nyerere eneo la Kipawa jijini Dar.

Katika tukio hilo kachero wa Oparesheni Fichua Maovu (OFM) akiwa kwenye kusaka matukio alipata taarifa kuwa watumishi hao wa Serikali wamevamia na kuanza ukaguzi kwenye duka hilo kubwa ambalo huuza matairi ya aina mbalimbali yakiwemo ya magari makubwa na madogo pia ya Bajaj.

Imedaiwa na chanzo chetu kuwa ukaguzi huo wa kushtukiza umefanyika kwenye duka hilo kufuatia taarifa na madai ya muda mrefu kuwa kuna maduka yana mchezo wa kuuza matairi yaliyokwisha muda wake (expire date), lakini wanunuzi yani wenye magari au madereva huwa hawajui kwa sababu ni vigumu kutambua kasoro hizo.

Wakaguzi hao wakiwa kazini kachero wa OFM naye aliwasili kwenye duka hilo na kukuta ukaguzi huo unaendea.

Wakiwa kwenye ukaguzi huo maofisa hao walikuta matairi ya magari na Bajaj zaidi ya 60 ambayo yanaonesha kwenye maandishi kuwa yameshaisha muda wake wa kutumika.

Baada ya kubaini hilo maofisa wa TBS wakiongozwa na kiongozi wao aliyejitambulisha kwa jina moja la Hassan walimsomea tuhuma zake mfanyabiashara huyo mwenye asili ya Kiasia.

Sambamba na kumsomea tuhuma hizo maofisa hao hawakuishia hapo walichukua sampuli ya matairi hayo na kwenda nayo kwenye maabara yao kuyafanyia uchunguzi zaidi ili kubaini kwamba licha ya kuisha muda wake kama yalivyoandikwa, yalikuwa na madhara au hayana na kama yana madhara ni kwa kiwango gani.

Gazeti hili lilishuhudia baadhi ya maofisa hao wakiyapakiza matairi hayo kwenye gari la Serikali.

“Hatua atakayochukuliwa mfanyabiashara huyu itafuatia baada ya majibu ya maabara ambayo yanachukua kama wiki moja kutoka,” alisema ofisa huyo. Wakizungumza na OFM baadhi ya wananchi waliokuwa eneo hilo walisema matairi kimeo ndiyo chanzo cha ajali za mara kwa mara.

“Mimi nawapogeza sana TBS kwa huo ukaguzi wao maana ikitokea ajali huwa tunasikia wakisema chanzo cha ajali hiyo ni kupasuka kwa tairi la mbele na gari kupoteza mwelekeo, matajiri wanapaswa kufahamu jinsi ya kusoma tarehe za matairi kwisha muda wake,” alisema Saidi Nachunga, mkazi wa Morogoro aliyekuwa jijini kwa shughuli zake binafsi.

“Kila siku ndugu zetu wanakufa ajalini inawezekana sababu ni hiihii ya matairi yaliyokwisha muda wake, mimi nawaomba hao TBS wafike kila kona ili nchi yetu na matajiri waepuke kuambiwa na madereva kuwa ajali imesababishwa na kupasuka matairi,” alisema shuhuda mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la John, mkazi wa Ilala Shaurimoyo, Dar.

Stori: Richard Bukos, Amani

Comments are closed.