Serikali Yafafanua Uhusiano Watanzania Na Kenya -Video
MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas, jana alifanya mahojiano maalum na +255 Global Radio, ambapo alizungumzia mambo mbalimbali likiwemo suala la uhusiano wa kidiplomasia baina ya Tanzania na Kenya.
Akizungumza kwenye kipindi cha Front Page kinachorushwa na redio hiyo, Dk Abbas alianza kuulizwa kuhusu madai ya mabadiliko ya kanuni za sheria ya maudhui mtandaoni 2020 kwamba, hazikupitishwa na Bunge pamoja na kushirikisha wadau, Dk Abbas alisema si kweli.
Alisema kanuni mpya zinazoongoza huduma za maudhui ya mtandaoni na zile za radio na televisheni hazijaanza leo, ni kanuni zilioanza kufanyiwa mchakato zamani na zimeshirikisha wadau wote waliopo kwenye tasnia hizo.
“Kuna wanaosema kanuni mpya zinatekelezwa na TCRA lakini zimesainiwa na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, kumbuka kwamba hizi kanuni ni za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ambayo kwa mujibu wa sera ya taifa, TCRA inawajibika kwenye Wizara mbili, yaani Wizara ya Habari na ile ya Uchukuzi na Mawasiliano.
“Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 pia imefafanua hilo, sheria inatungwa lakini kanuni zinatungwa na Mamlaka inayotekeleza sheria hiyo.
Wizara ya wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, hii inasimia mambo ya habari, wasanii, na wanamichezo.
“Wizara ya Uchukuzi na Mawasiliano inasimamia teknolojia za mawasiliano, watoa huduma za mawasiliano, uchukuaji wa masafa na kuyasafirisha, mitambo, minara na vitu vingine kama hivyo, zingekuwa kanuni zinazosimamia mitambo ya mawasiliano zingesainiwa na Waziri wa Mawasiliano, lakini kwa sababu zinasimamia maudhui ya habari ndiyo maana zimesainiwa na Waziri wa Habari.
“Wanaosema hazijahusisha wadau siyo sahihi, kanuni mpya za maudhui ya mitandaoni mchakato wake umeanza zamani, wakati naingia kwenye ukatibu mkuu, zimeshirikisha wadau na wametoa maoni yao kwa mara ya kwanza, baadaye tena tukawarudishia kwa mara ya pili tena tukawaelekeza walete kwa maandishi.
“Watu wanasema kanuni hizi zimekuja wakati wa uchaguzi, tuachane na uchaguzi, nchi ipo kabla na baada ya uchaguzi, wewe ulitaka tufanye lini?
Zile kanuni zimekuja kulingana na uzoefu ambao tumeupata kwenye miaka hii minne, kila nchi sasa inaunda sheria na kanuni kudhibiti mambo holela kwenye mitandao, uhuru binafsi kuingiliwa, taarifa za uongo, chochezi na hatarishi,” alisema,” alisema na kuongeza:“Kila nchi ina utamaduni na maadili yake, kanuni hizi mpya zimekuja kuitikia movement ya Kimataifa.
Sasa hivi duniani kote zinatungwa sheria za namna hiyo.“Haiwezekani wewe ni bloga, una-promoti ushoga, sisi tukuangalie.
Tutakushughulikia tu.”Kwenye mahojiano hayo, pia Dk Abbas alipoulizwa kuhusu vijana wasio na ajira wanaoanzisha televisheni za mitandaoni kwamba haoni serikali inao wajibu wa kuwatofautishia gharama za leseni wanaoanza shughuli hiyo na wale wazoefu, Dk Abbas alisema suala hilo linawezekana endapo tu litawekwa mezani.
“Nakumbuka hilo tulilijadili, tunasema kanuni sio za Bunge, ni za waziri. Wakati wowote pakiwa na hoja yenye mashiko na ni ya watu wengi, tutabadili kanuni wakati wowote, kwani tumeshafanya hivyo pia kwenye baadhi ya mambo ikiwemo mwanafunzi wa taaluma ya habari kupata press card ambapo sasa hivi kanuni zinatoa nafasi hata kwa wanafunzi kupewa press card,” alisema.
Kuhusu kulegalega kwa uhusiano wa kidiplosia wa Kimataifa, Dk Abbas alisema nchi ina uhusiano mzuri wa kidiplomasia.“Unapozungumzia uhusiano wetu, tuko vizuri. Tunapozungumza hapa, Rais wetu ni mwenyekiti wa SADC.
Tunaenda kukabidhi, hatuna ushirikiano, wangetuchaguaje? Kwenye miaka miwili iliyopita, alikuwa mwenyekiti wa jumuiya ya Afrika Mashariki, hatuna ushirikiano, wangetuchaguaje?
“Ukiangalia pale ikulu kila siku mheshimiwa Rais anapokea mabalozi, inakupa jibu. Sisi pia mheshimiwa Rais anaapisha mabalozi wanakwenda nchi nyingine. Hivyo kwa kweli diplomasia yetu ipo vizuri kabisa,” alisema.
Alipoulizwa kwa upande wa Kenya kufungulia baadhi ya nchi mipaka yake na Tanzania kutokuwa moja wapo, Dk Abbas alisisitiza kwamba, jambo hilo halina ubaya, bali ni utashi wa kila nchi katika kushughulikia ugonjwa wa Corona.
“Watu wasichanganye hili la Corona. Watu wasichanganye nchi moja kuchukua hatua kudhibiti Corona, wakasema hiyo nchi inazuia mipaka nchi nyingine.
Sisi na Kenya tupo vizuri. Wao walifunga mpaka wakiamini Corona itapungua, lakini bado ipo,” alisema na kuongeza:“Diplomasia inaongozwa na kanuni inayoitwa reciprocity.
Funga mpaka wako na mimi nafunga. Ukisema ndege zako hazitakuja kwangu, mimi nakuja kwako kufanya nini? Hiyo ni kanuni ya demokrasia,” alisema.Kuhusu suala la serikali kutoshughulikia masuala mbalimbali ya uvunjaji wa sheria katika kipindi hiki cha uchaguzi, msemaji huyo wa serikali alisema sheria zipo na zinafanya kazi muda wote.“Wakati wa uchaguzi sheria hazisimami.
Sheria mbalimbali za nchi zipo na zinaendelea kutumika isipokuwa serikali inaangalia kipaumbele, haiwezekani sisi tupo kwenye kushughulikia miradi mikubwa ya maendeleo, halafu mtu sijui amevunja sheria ya kuimba wimbo wa taifa uhangaike naye, hilo tumewaachia wahusika ambao ni msajili wa vyama vya siasa,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu mradi wa bomba la mafuta la kutoka Tanzania hadi Uganda, Dk Abbas alisema upo kama kawaida na utaendelea.
“Ni mradi mkubwa sana. Uganda ndiyo wanausimamia zaidi, walitoa nafasi kwa nchi za Afrika kununua hisa na sisi ni wanahisa.
Ule mradi unatekelezwa kupitia wabia. Sasa wale wabia ambao ndiyo watekelezaji, ilifika wakati walitofautiana, lakini baadaye walikubaliana wakauziana hisa na kwa sasa kampuni ya Total ndiyo atasimamia.
“Changamoto imekwisha, kama hawajatangaza basi watatangaza tenda mwezi huu wa nane au wa tisa,” alisema.Dk Abbas pia alizungumzia suala la uchumi wa kati kwa kuwataka Watanzania kuwa watulivu.“Uchumi wa kati maana yake ni nchi imetoka kwenye kiwango cha kuwa masikini, sasa mnaingia kwenye kiwango cha kuwa matajiri, lakini mnatakiwa kuwa matajiri sana,” alisema.
Stori na Erick Evarist, Risasi