Serikali Yakusanya Trilioni 105.26 ndani ya Miaka 4 – Video
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa katika kipindi cha kuanzia Novemba 2020 hadi Oktoba 2024, Serikali imekusanya jumla ya shilingi trilioni 105.26 na kwamba katika kipindi hicho makusanyo ya mapato yameongezeka kutoka shilingi trilioni 24.3 mwaka 2021/22 hadi shilingi trilioni 29.8 mwaka 2023/2024.
Majaliwa ameyasema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuhusu utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020, kwa kipindi cha miaka minne (2020 – 2024).
Majaliwa amebainisha pia kuwa mwaka 2024/2025 mwezi Julai hadi Novemba, 2024 makusanyo ya mapato ya kodi yalikuwa shilingii trilioni 13.54 ikilinganishwa na shilingi trilioni 8.1 katika kipindi kama hicho cha mwaka 2021/2022.
Tangu kuzindulia kwa huduma ya usafiri kwa kutumia reli ya kisasa (SGR) mwezi Agosti 2024 hadi Desemba 11, 2024 abiria zaidi ya 1,200,000 wamesafiri kwa kutumia treni hiyo.
Akizungumza jijini Dodoma katika Mkutano Mkuu wa CCM wakati akiwasilisha Taarifa ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuhusu Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, kwa kipindi cha miaka minne (2020 – 2024), Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema huduma hiyo ya usafiri imepunguza muda wa kusafiri, kuongeza tija katika biashara na uchumi kwa jumla.
Majaliwa amesema kuwa mradi huo umeiingizia Serikali jumla ya shilingi bilioni 30 na kwamba katika juhudi za Serikali za kuimarisha huduma za treni hiyo, vichwa 17 vya treni ya umeme vimenunuliwa sambamba na mabehewa 65 ya abiria.