The House of Favourite Newspapers

Serikali Yapinga Wadhamini wa Lissu Kujiondoa

0

UPANDE wa Mashitaka umewasilisha pingamizi la awali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kupinga maombi yaliyowasilishwa na wadhamini wa aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, ya kujiondoa kuendelea kumdhamini.

Wadhamini hao ni Ibrahim Ahmed na Robart Katula, ambapo walifikia hatua hiyo, baada ya kukosa ushirikiano kutoka kwa Lissu kwa kushindwa kufika mahakamani kama mshitakiwa.

Katika maombi yao, wanaomba Mahakama itoe hati ya kumkamata Lissu kwa kuwa wameshindwa kumpata na kumfikisha mahakamani hapo.

Taarifa ya pingamizi ya awali, iliwasilishwa mahakamani na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon ambae ndiye aliyepewa mamlaka ya kuendesha kesi hiyo.

Katika taarifa hiyo, inaeleza kuwa Mahakama hiyo haiwezi kushughulikia jambo hilo na pia haina mamlaka ya kusikiliza maombi hayo na ya kutolea maamuzi, kwa hiyo walalamikiwa wanaomba maombi hayo yatupiliwe mbali.

Maombi hayo, yaliwasilishwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, wakati shauri hilo lilipopelekwa kwa ajili ya kusikilizwa ambapo Wakili Wankyo aliomba Mahakama siku 14 ili aweze kujibu maombi hayo kwa njia ya maandishi.

Wankyo aliomba siku hizo ili aweze kupitia jalada la kesi ya msingi na pia kupitia kesi mbalimbali ambazo zilishatolewa uamuzi.

Baada ya Wankyo kudai hayo, mmoja wa wadhamini hao (Robert) na wao waliomba muda wa kuweza kujibu pingamizi hilo, ambapo Hakimu Simba alisema kiutaratibu pingamizi la awali ndiyo linatakiwa kuanza kusikilizwa.

Hakimu Simba aliwauliza wadhamini hao kama wana pingamizi na suala la upande wa Jamhuri kuwasilisha majibu yao kwa njia ya maandishi, ambapo waleta maombi hao walidai kuwa hawana pingamizi.

Alisema upande wa Jamhuri wanatakiwa kuwasilisha majibu hao Julai 28, mwaka huu, waleta maombi wanatakiwa kujibu hoja hizo Agosti 11, mwaka huu na kama kuna majibu ya ziada yatawasilishwa Agosti 18, mwaka huu na kesi itatajwa Agosti 19, mwaka huu, ambapo ndiyo itapangwa tarehe ya uamuzi.

Wankyo alidai katika majibu yake hati ya kiapo kilichowasilishwa mahakamani na waleta maombi hao kuwa Lissu aliruka dhamana toka tarehe ambayo alipona na kutoka hospitali.

Alidai kuwa wadhamini hao walikuwa na taarifa za kutosha mahali alipo kwa sababu ilitangazwa na alieleza  hivyo mahakamani.  Alieleza kwamba wadhamini wa mshtakiwa namba mbili (Lissu) wana wajibu wa kuhakikisha kwamba anafika mahakamani kwa mujibu wa amri ya Mahakama iliyotolewa Januari 20, mwaka huu na Hakimu Simba.

Mbali na Lissu washitakiwa wengine ni, Wahariri Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh.

Katika kesi ya msingi kwa pamoja washtakiwa hao, wanakabiliwa na mashtaka matano ikiwamo kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Ilidaiwa kuwa kati ya Januari 12 hadi 14, 2016 jijini Dar es Salaam, washtakiwa Jabir, Mkina na Lissu, waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar.’

Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Mshitakiwa Mehboob anadaiwa kuwa Januari 13 ,2016 katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi.

Ilidaiwa kuwa mshtakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.

Leave A Reply