The House of Favourite Newspapers

Serikali Yaridhishwa na Maandalizi ya Kilimanjaro Marathon 2021

0
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Alhaji Rajabu Kundya (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wachezaji wa Timu ya Riadha watakaoshiriki mbio za Kilimanjaro Marathoni Februari 28 wakati alipotembelea kambi yao katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU).

SERIKALI imeridhishwa na maandalizi ya mbio za mwaka huu za kimataifa za Kilimanjaro Premium Lager Marathon zinazotarajiwa kufanyika Jumapili ya wiki ijayo Mjini Moshi.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Alhaj Mwangi Kundya wakati alipotembelea kambi ya wanariadha wa kitanzania watakaoshiriki mbio hizo iliyopo Moshi, mkoani Kilimanjaro.

“Serikali inafuatilia kwa karibu maswala yote ya kiusalama ya kiafya kwa manufaa ya wananchi wetu kila siku ikiwemo siku ya mbio hizo maarufu, inatia moyo kuona ya kuwa wandaaji wa mbio hizo wamechukua tahadhari za kutosha hii inatia moyo”, alisema.

Aliendelea kusema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wandaaji wa mbio hizo pamoja na wadhamini wake mbalimbali ili kuhakikisha usalama wa kiafya wa washiriki wote kwa njia moja au nyingine.

Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Alhaji Rajabu Kundya alipokuwa akizungumza.

Aidha aliwashukuru wale wote waliofadhili kambi hiyo ambapo alisema ni hatua moja wapo ya kuhakikisha ya kuwa wanariadha wa Tanzania wanafanya vyema kwenye mbio hizo za mwaka huu zinazotarajiwa kufanyika Februari 28, mjini Moshi katika Uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU).

“Serikali imeweka mikakati kabambe yenye lengo la kukuza michezo hapa nchini ukiwemo mchezo wa riadha ili kulilitea hesima Taifa kupitia sekta ya michezo, nachukua fursa hii kuwapongeza wandaaji wa mbio za Kilimanjaro Marathon kwa kuziendeleza kila mwaka”, alisema.

Akiongea wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa chama cha riadha mkoani Kilimanjaro (KAAA) Adrma Mikumi, alisema tahadhari za kiafya zilizochukuliwa ni pamoja na kuweka maji tiririka kwenye maeneo yote ya uwanja wa Ushirika, pamoja na watu watakaokuwa na vitakatishi (sanitizers) kwa ajili ya wale watakaofika uwanjani siku hiyo.

“Ili kuepuka misongamano ya watu kwenye maeneo ya kunawia mikono pamoja na kupulizia vitakatishi, kutakuweko na watu ambao watakuwa na jukumu la kusanitize watu ili wasisongamane eneo moja ikiwa ni sehemu ya tahadhari”, alisema na kuongeza kuwa washiriki wote na watazamaji watapewa barakoa  za kutumika kabla na baada ya kukimbia wanapokuwa katika mkusanyiko.

Aidha alisema pia kutakuweko na maji tiririka yenye dawa maalum kila kituo kinachohusika na mbio hizo ambako wakimbiaji watapitia ili    kuhakikisha usalama wa washiriki wa mbio hizo.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Chama cha Riadha nchini (RT) John Bayo, aliwatoa hofu washiriki na wananchi wengine ambapo amesema tahadhari hizo hazimaanishi ya kuwa kuna changamoto yoyote ya kiafya.

Baadhi ya wachezaji wa Timu ya Riadha watakaoshiriki mbio za Kilimanjaro Marathoni Februari 28 waliopo kwenye kambi yao katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) wakipasha.

“Barakoa zitakazotolewa haimaanishi ya kuwa kuna changamoto yoyote ya kiafya bali ni tahadhari tu maana Tanzania haiko kwenye kisiwa na pia kutakuwepo na wageni wengi hivyo tahadhari ni muhimu sana haswa ikitiliwa maanani Serikali pia imeshatoa angalizo kwa wananchi wachukue tahadhari za kiafya kama inavyoelekezwa na wataalam wa afya”, alisema Bayo, ambaye pia ndiye Mkurugenzi wa mbio za Kimataifa za Kilimanjaro Premium Lager.

Katika hatua nyingine, washiriki wa mbio hizo waioko Jijini Dar es Salaam wanatarajiwa kuanza kuchukua namba zao za ushiriki Jumamosi Februari 20 na Jumapili Februari 21 kuanzia saa sita mchana hadi saa kumi na mbili jioni ambapo washiriki hao pia watapewa barakoa za kuvaa kabla ya kuanza mbio na baada ya kumalizika kwa mbio wanapokuwa katika mkusanyiko wa watu.

“Tunawaomba wale watakaokwenda kuchukua namba kuzingatia muda kwa sababu zoezi litafanyika kwa siku mbili  kwa mkoa wa Dar es Salaam kabla ya zoezi hilo kuhamia kwa wakazi wa mkoa wa Arusha na kufanyika tarehe 23 na 24 mwezi huu katika hoteli ya Kibo Palace kuanzia saa nane mchana hadi saa moja usiku na baadae kuhamia Moshi kwa siku tatu kuanzia Februari 25 (saa sita mchana hadi saa kumi na moja ), Februari 26 (saa nne asubuhi hadi saa mbili usiku) na Februari 27 (saa tatu asubuhi hadi saa kumi na moja jioni) katika hoteli ya Keys,” walisema waandaaji wa mbio hizo.

Walisema kuwa zoezi la kujiandikisha kwa mbio za kilomita 42 na zile za kilomita 5 kwa ajili ya kujifurahisha linaendelea katika vituo vya kuchukulia namba lakini litafanyika kwa malipo ya papo kwa papo lakini zoezi hilo limefungwa kwa wale wanaotaka kukimbia mbio za kilomita 21.

Mbio za mwaka huu zimedhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager kwa upande wa mbio ndefu za kilomita 42km, Tigo wamedhamini mbio za kilomita 21km (Half Marathon) wakati Grand Malt wamedhamini mbio za kilomita 5km.

Wadhamini wa vituo vya kunywa maji (water table) ni   Unilever Tanzania, Simba Cement, TPC Sugar, Kilimanjaro International Leather Company Limited, Kibo Palace Hotel na watoa huduma maalumu ni Garda World Security, Keys Hotel na CMC Automobile.

Mbio hizi zimeandaliwa na Kilimanjaro Marathon Company Limited na kitaifa zinaratibiwa na kampuni ya Executive Solutions Limited.

Leave A Reply