Serikali Yataka Mabenki Kutanua Wigo wa Kurahisisha Huduma za Kifedha
SERIKALI imeyataka mabenki nchini kuhakikisha yanatanua wigo wa kufungua ofisi katika kurahisisha huduma za kifedha kwa wafanyabiashara hatua hiyo inalenga kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha na kutengeneza mazingira wezeshe na rafiki kwa biashara ili kuleta tija katika ukuaji wa uchumi.
Ameyasema hayo Agosti 16, 2024 Kaimu katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Dkt. Elfas Msenya wakati wa Uzinduzi wa Ofisi mpya ya Benki ya Biashara ya Mwalimu (MCB) Mkoani Geita na kubainisha kuwa Mkoa huo ni wakimkakati kutokana na kuwepo kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi hivyo mabenki yatumie nafasi hiyo kusogeza huduma kwa jamii.
“Ni fursa kwa mabenki mengine kuungana na Benki ya Biashara ya Mwalimu kufungua ofisi zao hapa ili kutoa nafasi kwa wananchi kupata uhakika wa huduma za kibenki jambo ambalo litachangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa sekta ya fedha katika mkoa wa Geita” amesema Msenya
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa MCB Richard Louis Makungwa amesema wamefungua ofisi mkoani Geita kwa kuwa mkoa huo una fursa kubwa hususani ya biashara na uchimbaji wa madini, hivyo wameahidi kuhakikisha wanashiriki kikamilifu kwa kutoa huduma bora zaidi katika kuvutia wateja wadogo wadogo na wawekezaji mbalimbali ili kuwasaidia kukua kifedha na kuendelea kutumia benki ya biashara ya Mwalimu kwa huduma nzuri zaidi.
“Tunajua Geita ni mji wa madini na sisi tumejiandaa kikamilifu kuhudumia kwa ubora zaidi wateja wote, hususan wale wa sekta ya madini.” amesema Richard Louis Makungwa.
Naye, Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania Mwl. Joseph Misalaba amesema, Tusiishie kwenye kufungua matawi tu, bali pia elimu inapaswa kutolewa kwa walimu na wananchi mpaka kwa wachimbaji wa madini ili waweze kufahamu fursa zilizopo na umuhimu wake.
Hivyo, Afisa Elimu Mkoa wa Geita Mwl. Anton Mtweve ameshauri na kusihi Chama cha Walimu kuendelea kutafuta njia za kuleta ushindani kwa kuvutia wateja wengi zaidi na kuongeza mitaji ili matawi kama haya yaendelee kusambaa hadi kwenye halmashauri zote.