The House of Favourite Newspapers

Serikali Yatoa Tamko Bifu la Kiba, Mondi

BAADA ya mwanamuziki wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ kumwambia mwenzake, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ amkome na kukoleza bifu lao la kitambo, Serikali imetoa tamko lake juu ya sakata hilo, Amani linakujuza. 

 

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) lililo chini ya Katibu Mtendaji wake, Godfrey Mngereza, nayo imetia neno kwenye mgogoro wa Kiba na Diamond au Mondi uliodumu yapata miaka sita sasa.

 

MITAZAMO TOFAUTI

Tangu Mondi alipomualika Kiba kwenye tamasha lake la Wasafi litakalofanyika Jumamosi hii kwenye Viwanja vya Posta- Kijitonyama jijini Dar, kumekuwa na mitazamo tofauti kutoka kwenye makundi ya watu mbalimbali nchini.

 

Baadhi ya viongozi wamekuwa na maoni tofauti juu ya sakata hilo ambapo Mkuu wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Julius Mtatiro aliiambia +255 Global Radio kuwa anatamani wawili hao siku moja wamalize tofauti zao na wafanye kolabo na matamasha ya pamoja.

 

“Moja kati ya ndoto zangu kabla sijafa, ningependa kuona wimbo wa pamoja kati ya Kiba na Diamond. “Sioni kama hii mipasho yao inawasaidia, badala yake wange-concentrate kwenye kazi zao zaidi,” alisema Mtatiro.

Image result for msemaji wa basata

MSEMAJI WA BASATA

Mbali na watu binafsi, Gazeti la Amani pia limezungumza na Msemaji wa Basata, Rajab Sallo ambaye anatoa tamko la Basata ambayo ipo chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo inayosimamiwa na Waziri Dk Harrison Mwakyembe.

 

“Kwa kifupi tu ni kwamba sisi kama Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) tunaona kama jambo hili linakuza sanaa ya muziki kwani hatujapata malalamiko ya upande wowote kuonesha kwamba ni jambo la hatari. Badala yake tunaona kwamba kukiwa na makundimakundi mengi ndiyo mwendelezo wa kukuza sanaa ya muziki.

LENGO LA KUJENGA

“Kwa hiyo kimsingi sakata la Ali Kiba na Diamond lina mtazamo chanya wenye lengo la kujenga zaidi kuliko kubomoa. “Kwa hiyo siwezi kusema kwamba tumechukua hatua gani kwa sababu baraza la sanaa ni mzazi, ni mlezi, ni msajili wa wasanii wakiwepo vyama, mashirikisho, vikundi na msanii mmojammoja.

 

“Ni jukumu letu kabisa, kuyatazama mambo hayo, lakini juu ya Ali Kiba na Diamond bado hatujaona ubaya zaidi ya kutazama kwa jicho la kuliona jambo hilo kama sehemu ya kukuza muziki.

 

JE, LIKILETWA BASATA LITASULUHISHWA?

“Hakuna kitu ambacho kinashindikana kwani ndilo jukumu mojawapo la Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), kutoa ushauri wa kiufundi kwa wasanii wetu na kushauriana nao, lakini wakati mwingine tuamini tu kuwa migogoro inajenga.

 

MIGOGORO INAJENGA?

“Migogoro au bifu kama hizi mara nyingine zinamjenga msanii mmojammoja au vikundi,” alisema msemaji huyo wa Basata. Kwa maelezo hayo ni kwamba Basata wanaona bifu la Kiba na Mondi ni sehemu ya kukua kwa muziki wa Bongo Fleva.

 

TUJIKUMBUSHE

Kwa muda mrefu, Kiba na Mondi wamekuwa hawapikiki chungu kimoja ambapo awali chanzo cha msingi kilitajwa kuwa ni Wimbo wa Lala Salama ambao ilielezwa kuwa Mondi alifuta mashairi ya Kiba kwenye wimbo huo, jambo ambalo lilimkasirisha mno mwenzake huyo.

Hata hivyo, baada ya jambo hilo kupita Mondi amekuwa akionesha kuwa tayari kutaka kukaa meza moja na mwenzake huyo, lakini Kiba amekuwa hataki hata kusikia.

 

Stori: Memorise Richard, Amani.

Comments are closed.