Serikali Yawatoa Hofu Watanzania Kuhusu Ubora na Usalama wa Sukari
Serikali kupitia Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), imewatoa hofu Watanzania juu ya ubora na usalama wa sukari inayoingizwa nchini kutokana na umakini wa vyombo vyake vya Ulinzi, Usalama pamoja na Mamlaka za Udhibiti kufanya ukaguzi wa sukari yote inayoingizwa nchini kupitia Bandari na mipaka yote nchini ili kuhakikisha usalama wake kwa watumiaji.
Mkurugenzi wa Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), Profesa Kenneth Bengesi, alisema leo mchana jijini Dar es Salaam kuwa sukari iliyoingia nchini ina ubora kwa sababu imehakikiwa na Shirika la Viwango nchini (TBS) na kuiruhusu isambazwe kwa walaji.
“Mtu yeyote anayetaka kujiridhisha na ubora na usalama wa sukari iliyoingizwa nchini anaweza kuona nakala za cheti cha ithibati (certificate of conformity) na vipimo vya maabara vya TBS, ukizingatia kuwa kabla ya sukari kuingizwa huwa inakaguliwa vya kutosha nje na mamlaka zinazotambuliwa na TBS,” Alisema Profesa Bengesi.
Kutoka hadharani kwa bodi ya Sukari nchini kunatoa majibu halisi na ukweli wa hoja dhaifu zinazotolewa na baadhi ya wadau wa sukari sambamba na kuelezea faida ya mabadiliko ya sheria ya sukari kama mwarobaini wa uhaba wa bidhaa hiyo nchini.