The House of Favourite Newspapers

Serikali Yazima Jaribio Kuipindua Serikali ya Bongo

 

WAZIRI wa mawasiliano nchini Gabon anasema wanajeshi waaminifu kwa serikali ya Rais Ali Bongo wamefanikiwa kuzima jaribio la mapinduzi ya serikali nchini humo.

 

Bw.  Guy-Bertrand Mapangou ameliambia BBC kwamba wanajeshi wanne waliohusika katika jaribio hilo wamekamatwa na mwingine wa tano anasakwa.

 

“Hali ni tulivu. Polisi ambao huwa hapo wamerejea na kuchukua udhibiti wa eneo lote la makao makuu ya mashirika ya redio na runinga, kwa hivyo kila kitu kimerejea kawaida,” amesema.

 

“Walikuwa watano. Wanne wamekamatwa na mmoja yupo mafichoni na atakamatwa saa chache zijazo.”

Kundi la wanajeshi nchini Gabon lilikuwa limetangaza kwamba limetekeleza mapinduzi ya serikali katika taifa hilo la Afrika Magharibi na kutangaza amri ya kutotoka nje.

 

Wanajeshi wenye vifaru na magari ya kivita walikuwa wakishika doria katika barabara za mji mkuu Libreville.

 

Tangazo kutoka kwa kundi la vijana wa umri wa makamo lilitangazwa na kurudiwa katika kituo cha redio cha serikali nchini humo, ambapo wanasema kumekuwepo na wasiwasi kuhusu uwezo wa Rais Ali Bongo kuongoza nchi hiyo.

 

Walichukua udhibiti wa kituo hicho cha redio mwendo wa saa kumi alfajiri (saa kumi na mbili alfajiri Afrika Mashariki).

 

Wanajeshi hao walikuwa wamesema wamechukua hatua hiyo “kurejesha demokrasia” na wametangaza kwamba wanataka kuunda ‘Baraza la Taifa la Ufufuzi/Ukombozi’.

 

Taarifa yao pia ilipeperushwa kupitia runinga ya taifa.

 

Walikosoa hotuba ya Mwaka Mpya iliyotolewa na Rais Bongo mnamo 31 Desemba, na wanasema kwenye hotuba hiyo mawazo yake yalionekana kutotiririka na sauti yake ilikuwa dhaifu.

 

Mwandishi wa BBC Firmain Eric Mbadinga anasema jaribio hilo la mapinduzi ya serikali limewashangaza wengi kwa sababu jeshi limekuwa likitazamwa na wengi kuwa lina uaminifu wa hali ya juu kwa familia ya Bw. Bongo.

 

Wengi wa wakuu wa jeshi wanatoka kikosi cha walinzi wa rais, wengi ambao wametokea jimbo anakotoka Rais Bongo.

 

Bongo amekuwa nje ya nchi hiyo kwa zaidi ya miezi miwili, akipokea matibabu nchini Morocco kutokana na maradhi ambayo hayajafichuliwa baada ya kuugua akiwa ziarani Saudi Arabia 24 Oktoba alikohudhuria mkutano wa kiuchumi nchini humo.

 

“Huwezi kumlaumu mtu kwa kuwa mgonjwa. Bado anapata nafuu. Ni lazima angalau uwe na heshima kidogo, na kumheshimu mtu mgonjwa, hasa kiongozi wa nchi,” alisema msemaji wa serikali Mapangou baada ya jaribio hilo la mapinduzi kuzimwa.

 

Familia ya Bongo imetawala taifa hilo kwa miaka 51 iliyopita, na imetuhumiwa kwa kujilimbikizia mali na utajiri mkubwa kutokana na rasilimali za taifa hilo.

 

Bongo alichukua madaraka ya kuiuongoza nchi hiyo kutoka kwa baba yake Omar Bongo mwaka 2009, ambaye aliiiongoza nchi hiyo ya Afrika magharibi kwa zaidi ya miaka 40.

 

Alishinda uchaguzi wa marudio mwaka 2016, katika zoezi lililotawaliwa na ghasia na tuhuma za udanganyifu.

 

Katika uchaguzi huo, Bw Bongo alipata ushindi kwa 49.8% ya kura naye Bw Jean Ping akapata 48.2 % ya kura, kura zilizowatenganisha zikiwa 5,594.

 

Bw Ping alisema uchaguzi huo ulijaa udanganyifu na “hakuna ajuaye” hasa nani alishinda.

 

Kabla ya kuingia katika siasa, Ping aliwahi kuhudumu kama mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika.

 

 

Comments are closed.