The House of Favourite Newspapers

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 14

0

Seven Days

ILIPOISHIA:

“Tuondoke!” nilisema huku nikiinuka pale nilipokuwa nimekaa kwani tayari kengele ya hatari ililia ndani ya kichwa changu, Raya naye akainuka, tukaanza kuelekea kwenye lango la kutokea nje ya hospitali hiyo lakini cha ajabu zaidi, tukiwa getini tunataka kutoka, nililiona lile gari nalo likija kule tulipokuwepo.

 

SASA ENDELEA…

“Bodaboda! Bodaboda!” niliita kwa sauti huku tukitembea kwa haraka kuelekea nje ya hospitali, lile gari nalo likizidi kuja kwa kasi kule tulipokuwepo. Ilibidi nimshike mkono Raya kwani kwa jinsi alivyokuwa ‘mayai’ ningeweza kumuacha pale na kumsababishia matatizo.

 

Kwa bahati nzuri, dereva mmoja wa bodaboda alituona na harakaharaka akawasha pikipiki yake na kutufuata, mwenyewe akijiona amewazidi wenzake ujanja kwa kuwahi abiria.

 

“Tupeleke Kijitonyama,” nilisema huku nikimsaidia Raya kupanda, na mimi nikapanda lakini dereva wa bodaboda hakutaka kuondoka mpaka tukubaliane kwanza.

 

“Twende bwana nitakupa kiwango chochote unachotaka.”

“Lakini siku hizi haturuhusiwi kupakiza mishikaki nitakamatwa.”

“Twendeee,” nilisema kwa sauti ya juu, yule dereva akaondoa pikipiki, kabla hajafika popote wote tulishtukia bodaboda ikikoswakoswa kugongwa kwa nyuma na lile gari lililokuwa linatufuata kwa kasi. Dereva wa bodaboda alitaka kusimama pembeni kulipisha gari hilo lakini nilimsisitiza kuongeza mwendo na kuhakikisha analipoteza kabisa lile gari.

 

*Usikose kutembelea Simulizi za Majonzi

Akiwa haelewi kinachoendelea, hofu kubwa ikiwa imemkumba moyoni, yule dereva bodaboda alikata kona ya ghafla na kuingia kwenye uchochoro mita chache mbele, hali iliyosababisha lile gari ambalo lilikuwa likijiandaa kutugonga kwa nyuma lipitilize kwa kasi, likaenda kusimama mita chache mbele.

 

Raya alikuwa akipiga kelele kwa nguvu huku akilitaja jina la Mungu wake, hakuelewa kilichotokea kiasi cha kujikuta katikati ya mtego wa kifo kama ule, nikawa nambembeleza na kumtaka atulie.

 

Lile gari lilirudi kinyumenyume na kujaribu kupita kwenye ule uchochoro kuifuata ile bodaboda lakini sehemu ilikuwa ndogo, likashindwa. Nikawa namsisitiza dereva kuzidi kuongeza kasi, tukatokeza mtaa wa pili na kuingia kwenye barabara ya lami, safari ikazidi kupamba moto.

 

“Usipite barabara kubwa, wanaweza kuwa wanatufuatilia, ingia kushoto hapo mbele,” nilimwambia, wazo ambalo dereva huyo alilifuata, tukawa tunazidi kukata mitaa tukitumia njia za uchochoroni.

 

“Nataka twende nyumbani kwetu Jamal,” alisema Raya huku akiwa bado na hofu kubwa moyoni.

 

“Ok sawa,” nilimjibu kwa kifupi kwa sababu kiukweli sikuwa nataka kupata muda wa kukaa peke yangu na Raya kama ilivyotokea usiku uliopita lakini kwa jinsi hali ilivyokuwa sikuwa na ujanja.

 

Dakika kadhaa baadaye, tayari tulikuwa tumefika Kijitonyama lakini kwa kukwepa kuonekana tumeelekea wapi, tuliamua kushuka kwenye bodaboda, tukakubaliana bei na dereva huyo ambaye licha ya kulipwa fedha zake, alionesha kuwa na shauku kubwa ya kutaka kujua kilichokuwa kinaendelea.

 

Hata hivyo, sikuwa tayari kumueleza chochote, akaondoka kwa shingo upande huku akigeukageuka nyuma, kuna wakati alihisi huenda alikuwa ametubeba majambazi lakini alikosa ushahidi wa hilo.

 

Yule dereva bodaboda alipoondoka tu, mimi na Raya tulipanda kwenye Bajaj ambayo ilitupeleka mpaka nyumbani kwa akina Raya, tukawa na uhakika mkubwa kwamba hata kama wale watu wataamua kutufuatilia, haitakuwa rahisi kutupata.

 

“Naomba ukaoge kwanza wakati mimi nafanya utaratibu wa chakula,” alisema Raya baada ya kuhakikisha milango yote ya nyumba hiyo imefungwa kwa ndani, kuanzia geti kubwa la nje mpaka milango ya ndani.

 

Kwa kuwa wazazi wa Raya hawakuwa wamerejea safarini kama mwenyewe alivyonieleza, kwa mara nyingine tulijikuta tukiwa peke yetu ndani ya nyumba.

 

Wakati nikiendelea kujiuliza kuhusu mfululizo wa matukio yaliyokuwa yakiendelea kuniandama kiasi cha kunifanya nikose uhakika juu ya maisha yangu, Raya alikuwa akifikiria jambo jingine tofauti kabisa.

 

Niliingia kwenye chumba cha wageni ambacho ndicho nilicholala usiku uliopita na kubadilisha nguo, nikajifunga taulo na kuelekea bafuni, mawazo mengi yakiendelea kukisumbua kichwa changu.

 

*Usikose kutembelea Simulizi za Majonzi

 

Bado nilishindwa kupata majibu kuhusu Shenaiza, sikuwa nikielewa kama Shenaiza alikuwa ni mtu wa namna gani, akina nani walikuwa wakiyawinda maisha yake na alikuwa na uhusiano gani nao. Kila swali nililojiuliza halikuwa na majibu.

 

“Shenaiza Petras Loris,” nililikumbuka jina kamili la msichana huyo alilolitaja wakati akihojiwa na yule mpelelezi.

 

“Kabila langu ni Aethikes… mimi siyo Mtanzania, natokea Greece (Ugiriki), asili yetu ni Attica, baba yangu amezaliwa na kukulia kwenye Jiji la Athens lakini mama yangu ni mpare wa Mtae, Lushoto mkoani Tanga,” maneno ya Shenaiza wakati akijieleza yalikuwa yakijirudiarudia ndani ya kichwa change kama mkanda wa video.

 

“Lazima niujue ukweli! Lazima!” nilisema wakati nikifungulia bomba la maji ya mvua, maji ya baridi yakawa yananimwagikia na kuufanya mwili wangu uliokuwa umechoka sana upate nguvu mpya.

 

Japokuwa msichana huyo hakuwa tayari kunieleza ukweli zaidi ya kuishia kuniambia nisubiri ataniambia, niliamua kuutafuta ukweli kwa njia nyingine ingawa bado sikuwa naijua ni njia gani na nitafanyaje kumfahamu Shenaiza.

 

Nilikaa muda mrefu bafuni, nikiwa naendelea kujimwagia maji huku akili yangu ikienda mbio kuliko kawaida. Nilikuja kushtuka baada ya kusikia Raya akiniita na kuugonga mlango wa bafuni.

 

“Mbona hutoki bafuni mpenzi wangu,” alihoji Raya kwa sauti ya kubembeleza, harakaharaka nikafunga bomba na kuchukua taulo, nikajifuta na kufungua mlango, macho yangu yakagongana na Raya ambaye naye alikuwa amejifunga khanga moja tu.

 

“Na mimi nataka kuoga, nisubiri tuondoke wote,” alisema msichana huyo huku akinitazama kwa macho yaliyojaa ujumbe mzito, taratibu akanirudisha bafuni, nilishindwa kumzuia, naye akaingia na kufunga mlango kwa ndani.

 

“Nataka leo na mimi nideke, naomba uniogeshe,” alisema Raya na kunifanya nijikute kwenye wakati mgumu kwa mara nyingine, nikiwa bado sijui nijibu nini, msichana huyo alifungua khanga na kuitundika nyuma ya mlango, akabaki kama alivyoletwa duniani, vifuu viwili vikiwa vimechomoza kwenye kifua chake na kunifanya nisisimke mwili mzima.

 

Akalishika taulo nililokuwa nimejifunga na kulivuta kisha akalitundika pale alipoweka khanga yake, tukabaki saresare maua! Akanisogelea jirani kabisa kiasi cha kila mmoja kuanza kuzisikia pumzi za mwenzake, tukawa tunatazamana machoni huku ‘Jamal’ wangu naye akianza kufura kwa hasira.

 

***

Baada ya kumaliza kumhoji Shenaiza, yule askari mpelelezi, alitoka hadi nje alikowaacha wenzake, akawavuta pembeni na kuanza kuwaeleza alichoelezwa na msichana huyo, kila mmoja akawa ametulia akimsikiliza. Maelezo aliyoendelea kuyatoa, yalimshangaza kila mmoja, wakawa wanatazamana wakiwa ni kama hawaamini walichokuwa wakiendelea kukisikia kutoka kwa mwenzao.

 

“Kwani amesema asili yake ni wapi?”

“Ni Athens, Greece! Na kubwa zaidi, amesema jina lake kamili ni Shenaiza Petras Loris.”

“Unataka kusema kwamba ni mtoto wa Petras Loris huyu tunayemjua?”

“Sijamuuliza lakini kwa maelezo yake, upo uwezekano mkubwa akawa ni mwanaye au wana undugu fulani.”

“Aisee! Mbona hii inaonekana kuwa ngoma nzito?”

“Ni ngoma nzito kwelikweli, halafu kuna huyu kijana ameingizwa kwenye mtego bila mwenyewe kujua chochote, mpaka namuonea huruma.”

 

Je, nini kitafuatia? Usikose next issue au bofya Simulizi za Majonzi

Leave A Reply