The House of Favourite Newspapers

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 36

0

ILIPOISHIA:

Ghafla akiwa anakuja mbio, lile gari lilitokeza tena na kuja kwa kasi pale lilipokuwa limepaki awali, nikashtuka kugundua kuwa kumbe wale watu hawakuwa wameondoka, nikajua lazima watashtukia mahali nilipo kutokana na jinsi Raya alivyokuwa anakuja kwa kasi.

SASA ENDELEA…

“Naomba unisaidie kitu, huyu dada akifika hapa kuniulizia mwambie nimeshashuka kwenye gari nimeelekea upande wa wodi za wanaume, nikishuka funga huu mlango haraka,” nilimwambia dereva teksi ambaye alibaki ameduwaa, akiwa haelewi kinachoendelea.

Harakaharaka nikafungua mlango wa upande wa pili, nikashuka kwa kasi na kubingirika mpaka chini ya ile teksi, nikatulia huku mapigo ya moyo wangu yakinienda mbio kuliko kawaida. Nilimuona Raya akikimbia mpaka pale kwenye ile teksi, nikajikausha kimya.

“Kaka samahani, nimeelekezwa kuwa mgonjwa wangu yupo ndani ya hili gari, yuko wapi?” nilimsikia Raya akimuuliza yule dereva teksi huku akihema.

“Alikuwepo lakini ameshuka ameelekea kule kwenye wodi za wanaume,” yule dereva teksi alijibu kama nilivyomuelekeza. Nikasikia Raya akiguna akiwa ni kama haamini, mara nikaliona lile gari limekuja na kupaki palepale lilipokuwa limepaki mara ya kwanza, nikaiona miguu ya watu wakishuka na kusogea pale Raya alipokuwa amesimama akizungumza na dereva teksi.

Yaani kama mtu angepata wazo la kuchungulia chini ya ile teksi, basi huenda siku hiyo ndiyo ingekuwa mwisho wangu.

“Habari yako kaka,” nilimsikia mmoja kati ya wale wanaume walioshuka kwenye lile gari, Isuzu Bighorn.

“Safi!”

>>>Usikose kutembelea Simulizi za Majonzi

“Kuna mtu tunamtafuta, tunahisi yupo ndani ya hili gari lako,” alisema mwingine kwa sauti nzito, bila kusubiri kujibiwa, nikawasikia wakifungua milango ya teksi hiyo, yule dereva na Raya wakawa wanashangaa.

“Kwani nyie ni akina nani?” nilimsikia Raya akiwauliza lakini hakuna aliyemjibu, nikasikia wakibamiza milango ya teksi hiyo kwa nguvu, nadhani ni baada ya kufungua na kunikosa.

Nikawaona wakiondoka kwenye teksi hiyo bila kusema kitu, wakaelekea kwenye gari lao, wakapanda kisha nikaona gari likirudi nyuma na kuondoka tena.

“Kwani wale ni akina nani? Mbona wamekuja kisharishari namna hiyo?” nilimsikia Raya akimuuliza yule dereva teksi lakini hakuwa na majibu. Baada ya kuhakikisha wameshaondoka na gari lao, nilibingirika na kutoka uvunguni mwa gari.

Kwa bahati nzuri, pale kwenye maegesho ya magari palikuwa na lami kwa hiyo sikuchafuka sana, Raya akapigwa na butwaa kuniona nikitoka uvunguni mwa gari.

“Jamal! Ooh maskini pole mpenzi wangu, wale ni akina nani wanaokusaka kama jambazi?” alisema Raya huku akinisogelea na kunikumbatia huku akinimwagia mvua ya mabusu.

“Na muda wote huo ulikuwa umeenda wapi? Mbona nimekuja muda mrefu tu kukuletea chakula lakini haukuwepo?” Raya alizidi kunihoji, nikamwambia atulie kwanza nitamueleza kila kitu vizuri.

Yule dereva teksi akawa ananitazama kwa macho yaliyoonesha kuwa na maswali mengi yasiyo na majibu.

“Yule daktari alikuwa anasemaje kule wodini?” nilimuuliza Raya kimitego, akanijibu kwamba alikuwa akiniulizia kwa madai kwamba kuna kipimo inatakiwa nikafanyiwe nje ya hospitali, akawa anashangaa kwa nini sikuwepo wodini.

“Kwani wewe ulikuwa wapi mpaka madaktari wanakutafuta?” Raya aliniuliza tena, nikaendelea kumjibu vilevile kwamba atulie, nitamueleza kila kitu baadaye.

“Basi twende ukale nimekuletea chakula unachokipendaga,” alisema Raya, nikamjibu kwamba hospitalini hapo hapakuwa sehemu salama tena kwangu. Sikutaka kumuudhi Raya lakini pia sikutaka afahamu kwamba nilikuwa nimetoka nyumbani kwa Shamila na tayari mimi na yeye tulishaanzisha uhusiano wa kimapenzi.

“Naomba hicho chakula kaniletee kwenye gari, nichukulie na vitu vyangu mle wodini,” nilimwambia, akaondoka harakaharaka huku akigeuka huku na kule.

“Kaka kwani nini kinaendelea? Mbona sielewielewi?” alisema yule dereva teksi, naye nikamjibu tu kwa kifupi kwamba mambo yalikuwa magumu.

“Hawa jamaa mbona wamekuja kibabe sana halafu yule mmoja anaonekana kama ana mashine kwenye koti?” alisema yule dereva, nikashtuka sana kusikia kwamba kumbe mmoja kati yao alikuwa na bunduki, nikahisi maisha yangu yako hatarini zaidi.

>>>Usikose kutembelea Simulizi za Majonzi

“Au wanakudai?” yule dereva teksi alizidi kunihoji lakini bado sikumpa ushirikiano aliokuwa anautaka.

Akili yangu ilikuwa ikiwaza mambo tofauti kabisa, kwanza ilikuwa ni lazima nijue kuhusu biashara aliyokuwa akiifanya baba yake Shenaiza lakini pia ilitakiwa niwe makini kulinda maisha yangu kwani kwa ilivyoonesha, tayari walikuwa wameshtukia kwamba nawafuatilia.

Muda mfupi baadaye, Raya alirudi akiwa ameongozana na Shamila, wote wakaingia kwenye ile teksi, Raya akakaa pembeni yangu na Shamila akakaa siti ya pembeni ya dereva.

“Nimepata wazo, unajua hapa kuna wodi za ‘private’ ambazo zinalindwa, unaonaje tukikuhamishia huko maana hali imeshachafuka,” alisema Shamila, wazo ambalo kwa kiasi fulani niliona kama ni la msingi.

“Kwani huyu ni nani?” Raya aliuliza baada ya kumsikia Shamila.

“Huyu ndiyo nesi anayesimamia matibabu yangu lakini ameguswa na matatizo yangu na ndiyo maana ameamua kunisaidia kwa karibu. Shamila, kutana na Raya, mchumba wangu,” nilisema kwa kujiamini, nikamuona Shamila akitoa tabasamu la uongo.

Dereva teksi kwa kuwa alikuwa anajua mchezo unavyoenda, alijifanya yuko bize kurekebisharekebisha vitu pale kwenye ‘dashboard’ ya gari lake.

“Nimefurahi kukufahamu,” Raya alijibu kwa kifupi, Shamila akanyoosha mkono na kumpa, wakashikana kwa sekunde chache na kuachiana. Ilikuwa ni lazima nifanye vile na kusimama kama mwanaume kwani nilishaanza kumuona Raya akikosa raha.

“Unalionaje wazo alilolitoa nesi?” nilimuuliza Raya, naye akaliunga mkono.

“Basi tufanye hivyo haraka, wanaweza kurudi tena,” nilisema, wote tukashuka kwenye teksi harakaharaka na kuanza kumfuata Shamila ambaye ndiye aliyekuwa akituongoza.

“Usitembee haraka hivyo, utajiumiza tena kidonda,” alisema Raya huku akitaka kunipokea laptop niliyokuwa nimeing’ang’ania lakini nikamkatalia. Muda mfupi baadaye tayari tulikuwa kwenye lifti, tukapanda mpaka ghorofani kulikokuwa na wodi za private.

Mazxingira ya wodi hizo yalikuwa mazuri kwa sababu kwanza kulikuwa na walinzi wenye silaha koridoni, halafu milango ya wodi ilikuwa imara, kidogo nikawa na amani moyoni mwangu. Tulipoingia tu wodini, harakaharaka niliiwasha ile laptop na kuanza kuyaangalia yale mafaili machache niliyokopi kutoka kwenye ile ‘hard disk’.

“Hivyo ni vitu gani unavyoviangangalia kwenye hiyo laptop?” Raya aliniuliza wakati akiandaa chakula huku Shamila naye akiwa bize kuwekaweka vitu vyote vizuri ndani ya wodi hiyo, nikamdanganya Raya kwamba kuna kazi nilikuwa nimetumiwa kutoka kazini.

“Mh! Kutoka kazini? Nani anayeweza kukupa kazi wakati watu wote wanajua kwamba unaumwa? Isitoshe asubuhi nilipitia kule kazini na kila mtu akawa anakupa pole,” Raya alizidi kunibana, nikamwambia nitamfafanulia baadaye.

Niliendelea ‘kuperuzi’ yake mafaili, moja baada ya jingine. Kama nilivyokuwa nimeona awali, yalikuwa yamejaa taarifa za watu mbalimbali, wakubwa kwa wadogo, yakiwa na taarifa kuhusu hali zao za kiafya na viungo mbalimbali kwenye mwili, bado nikawa sielewi.

Niliendelea kuchimba kwa undani, taratibu nikaanza kugundua mambo ambayo ama kwa hakika yalinishangaza sana. Kwa jinsi ilivyoonesha, kulikuwa na mtandao mpana sana wa watu kutoka hapa nyumbani Tanzania, India, Marekani, Uingereza na nchi za kiarabu ambao ulikuwa ukihusisha hospitali kubwakubwa duniani.

Nilipoendelea kufuatilia kwenye mafaili yake, nikaanza kugundua kwamba kumbe kulikuwa na biashara ya viungo vya binadamu ilikuwa ikifanyika katika nchi mbalimbali, kwamba baba yake Shenaiza alikuwa akiwakusanya watu kutoka maeneo mbalimbali ya nchi na kuwasafirisha kwenda kwenye hospitali kubwakubwa duniani kwa ajili ya kuchangia viungo mbalimbali vya miili yao.

Kilichonishangaza sana ni kugundua kuwa wengi walikuwa wakisafirishwa kutoka Tanzania, wakiwa hawajui chochote kinachoenda kuwatokea. Mbaya zaidi, kulikuwa na watu ambao wameandikwa kwamba wanaenda kuchangia moyo, ninavyofahamu mimi binadamu anakuwa na moyo mmoja tu, kwa hiyo akichangia inakuwaje?

Nikajiuliza pia kwamba kuna baadhi ya watu ilionesha kwamba wanaenda kuchangia ubongo, sasa ukichangia ubongo na wewe nini kinakutokea? Unawezaje kubaki ukiwa hai? Kengele ya hatari ikalia ndani ya kichwa changu, nikawa nahisi pengine nipo ndotoni.

Je, nini kitafuatia? Usikose next issue au bofya Simulizi za Majonzi.

Leave A Reply