The House of Favourite Newspapers

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 47

ILIPOISHIA:

“Nataka nikalale na dada Shenaiza,” alisema kwa sauti ya kudeka huku akinisogelea na kujilaza kifuani kwangu, nikapitisha mkono wangu na kumshika kiunoni, nikamuona akiruka kama aliyepigwa na shoti ya umeme.

SASA ENDELEA…

“No! Usifanye hivyo,” alisema Firyaal huku akinitoa mkono kwa staili ya ‘sitaki nataka’, nikamvutia kwangu na kusababisha tuwe tunatazamana katika umbali usiozidi nchi tano, kiasi cha kila mmoja kuwa anazisikia pumzi za mwenzake.

“This is not the right time,” (Huu siyo muda muafaka) alisema huku akiipitisha mikono yake na kunishika shingoni, kwa mara nyingine nikamshika kiunoni, akashtuka tena, safari hii kwa nguvu zaidi na kufumba macho yake mazuri, tukagusanisha ndimi zetu na kuanza kuwaiga njiwa wanavyoyalisha makinda yao.

Jambo la ajabu lilitokea kwenye hisia zangu, nikawa nahisi kama nipo kwenye ulimwengu mwingine wa tofauti kabisa, tuliendelea kugandana kama ruba kwa sekunde chache, kelele za kitasa cha chumba alichokuwa amelala Raya ndizo zilizotushtua.

Harakaharaka nikamuachia Firyaal na kumuonesha kwa ishara kwamba aende chumbani alikokuwa amelala dada yake, kweli alifanya hivyo, akakimbia kwa kunyata wakati mimi nikienda kumfungulia Raya.

“Vipi?” nilimuuliza baada ya kumfungulia mlango ambao ni mimi ndiye niliyemfungia kwa nje ili nipate nafasi nzuri ya kuwa na Firyaal.

“Wewe ndiyo ulinifungia mlango kwa nje?”

“Mh! Saa ngapi tena mpenzi wangu? Itakuwa labda mlango ulijiloki,” nilimwambia.

“Kwani ulikuwa hujalala mpaka saa hizi?”

“Nilikuwa namsubiri Firyaal arudi ndiyo nifunge geti, amesharudi na nafikiri muda huu ameshalala na dada yake na mimi nilikuwa najiandaa kulala,” nilijenga mazingira ya kujitetea. Nikampachika swali jingine:

“Mbona umeamka wakati ndiyo kwanza ulikuwa unaanza kulala?”

“Nimeota ndoto mbaya sana mpaka nimeshtuka,” alisema Raya huku akijinyoosha.

“Ndoto gani tena?”

“Inatisha sana, please Jamal mi siwezi kulala peke yangu, nakuomba tukalale wote,” alisema Raya huku akinikumbatia, nikashusha pumzi ndefu kwani niliona ananiharibia sana ‘taiming’ zangu. Hata hivyo sikuwa na namna zaidi ya kukubaliana naye, nikamshika mkono na kuelekea naye kwenye kile chumba ambacho Shamila alinipa mimi nilale.

Hata hivyo, moyoni nilishajiapiza kwamba sitafanya chochote na Raya hasa ukizingatia kwamba tayari nilishampa udhuru mapema kwamba hali yangu haikuwa nzuri. Baada ya kuingia chumbani, kwa sababu muda ulikuwa tayari umeenda sana, hatukuwa na cha ziada zaidi ya kupanda kitandani na kulala.

Japokuwa Raya alikuwa pembeni yangu, akili zangu zote zilikuwa kwa Firyaal, ni kama nilikuwa nimepandwa na pepo ndani ya kichwa changu. Nilikumbuka kila kitu kilichofanyika muda mfupi uliopita, nikawa nazilaumu ndoto za Raya kwani kama asingeota na kushtuka kama mwenyewe alivyosema, huenda tayari ningeshakuwa naelea kwenye ulimwengu mwingine tofauti kabisa.

Wasiwasi wangu mkubwa ulikuwa ni je, Firyaal akija kunigongea usiku huo itakuwaje? Sikupata majibu. Kwa kuwa Raya alikuwa amechoka sana, nilipomkumbatia tu, hakuchukua muda, akaanza kukoroma tena, akiwa amelala fofofo. Niliendelea kutafakari mambo mengi na hatimaye usingizi ukanipitia.

Mlio wa simu ya mezani ndiyo ulionishtua kutoka kwenye usingizi mzito, nikamsogeza Raya pembeni na kuamka, nikatoka mpaka sebuleni na kwenda kuipokea simu hiyo.

>>> Usiache kutembelea Simulizi za Majonzi kwa hadithi na simulizi kali!

“Haloo!”

“Haloo Jamal, umeamkaje mpenzi wangu?”

“Ooh! Shamila, ni wewe? Nimeamka salama, vipi wewe huko?”

“Huku kuna matatizo mpenzi wangu, nimekupigia kukwambia kwamba inawezekana nikawa sipatikani hewani, ishu imeshtukiwa huku na imebainika kwamba nimehusika kuwatorosha wagonjwa wawili, wewe na Shenaiza, hIvi ninavyoongea na wewe tunaingia kwenye mkutano wa dharura na viongozi wetu pamoja na polisi.”

“Mungu wangu, kwa hiyo itakuwaje?”

“Nimekupigia simu kukutaarifu kwamba hapo nyumbani kwangu hapafai tena, kuna uwezekano mkubwa polisi wakaja kufanya upekuzi kwa hiyo nakuomba muondoke haraka iwezekanavyo. Chukua kalamu na karatasi, andika namba hii nitakayokutajia,” alisema Shamila na kunifanya mapigo ya moyo wangu yawe yananienda mbio kuliko kawaida.

Nikachukua kalamu na karatasi.

‘Tayari nimeshachukua,” nilimwambia Shamila baada ya kuuinua tena mkonga wa simu, akanitajia namba hiyo ya simu na kuniambia kwamba ni ya mama yake mdogo anayeishi Kimara Temboni.

“Nimeshampigia na kumwambia kila kitu, yupo tayari kuwasaidia, mpigie sasa hivi,” alisema Shamila kisha akakata simu. Nilipoweka mkonga wa simu chini, nilitazama saa ya ukutani iliyokuwa inaonesha kwamba ilikuwa ni tayari saa kumi na mbili asubuhi, harakaharaka nikaelekea kwenye chumba alichokuwa amelala Firyaal na Shenaiza ambaye bado hakuwa amerejewa na fahamu zake.

“Firyaal, Firyaal,” nilisema huku nikigonga mlango wa chumba hicho, nilipoona kimya nikanyonga kitasa, kumbe hata hakuwa amefunga mlango, nadhani alijua kwa vyovyote usiku ule nitamfuata tena.

Nikaingia na kutupa macho kitandani, Firyaal alikuwa amelala kihasarahasara, akiwa amejifunga khanga moja tu huku dada yake, Shenaiza akiwa amelala kwenye kitanda kingine maana ndani ya chumba hicho kulikuwa na vitanda viwili.

Nilishusha pumzi ndefu kwani nikiri kwamba Firyaal alikuwa akiyafanya mapigo ya moyo wangu yaniende mbio sana, hasa kutokana na hali niliyomkuta nayo, mwenyewe akiwa hana habari ameuchapa usingizi.

Taratibu nilimsogelea, nikainama pale kitandani na kumbusu kwenye paji la uso wake, akafumbua macho na kunitazama, akaachia tabasamu hafifu na kunishika mkono wangu, joto la kikekike likazidi kunifanya nisisimke mno.

“Mbona umechelewa kuja Jamal wangu, hata mlango sikufunga kwa ajili yako,” alisema huku akinivutia pale kitandani ili na mimi nilale.

“Kuna tatizo Firyaal,” nilimwambia, kauli yangu ikamfanya ayakodoe macho yake mazuri ambayo yalikuwa yamelegea sana kwa sababu ya usingizi.

“Tatizo gani tena mpenzi?” aliniuliza kwa sauti iliyojaa shauku.

“Shamila amepiga simu anasema huko kazini kwao kimenuka, wamemshtukia kwamba yeye ndiye aliyetutorosha na hivi tunavyoongea wameingia kwenye kikao cha dharura, anasema inabidi tuondoke hapa haraka iwezekanavyo,” nilimwambia.

“Mungu wangu,” alisema huku akikurupuka pale kitandani, akasimama huku akinitazama kwa wasiwasi, mkono mmoja akautumia kuirudisha ile khanga yake ambayo alipoinuka ilifunuka upande na kusababisha niyaone tena maungo yake ambayo ama kwa hakika yalikuwa yakimuamsha shetani wangu wa mahaba.

“Kwa hiyo itakuwaje?”

“Inabidi tujiandae tuondoke, oga fastafasta kisha muandae mgonjwa, ngoja na mimi nikamuamshe Raya,” nilisema, akatingisha kichwa huku akiendelea kunitazama kwa macho yake mazuri, nikageuka na kutaka kutoka, akanishika mkono huku akiliita jina langu.

“Nambie,” nilijibu kwa upole, akanisogelea hadi mwilini na kunikumbatia kwa nguvu.

“Nakupenda Jamal,” alisema kisha akanibusu kwenye shavu langu la upande wa kushoto, mwili wote ukasisimka tena, nikakosa hata cha kujibu zaidi ya mimi kumkumbatia pia na kumbusu, uvuguvugu wa joto la mwili wake ukanifanya nitamani niendelee kumkumbatia lakini nilipokumbuka mtihani mzito uliokuwa mbele yangu, nilimuachia, nikatoka haraka na kwenda kumuamsha Raya, harakaharaka tukaanza kujiandaa.

Je, nini kitafuatia? Usikose next issue au bofya Simulizi za Majonzi kusoma mwendelezo.

Comments are closed.