The House of Favourite Newspapers

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 49

ILIPOISHIA:

Ndani ya dakika mbili tangu tukae mkao huo, kuna mambo ya ajabu yalianza kunitokea, mapigo ya moyo yakawa yanazidi kwenda mbio kuliko kawaida kutokana na kile nilichokuwa nakishuhudia.

SASA ENDELEA…

Nilianza kuona ile hali kama ambayo ilinitokea siku ile nilipovamiwa barabarani na kujeruhiwa vibaya na baadaye kuingia kwenye ulimwengu wa tofauti, nikawa najihisi kwamba japokuwa nilikuwa nimekaa pale chini na wenzangu, taswira nyingine ya mwili wangu ilikuwa ikianza kupaa juu na kuelea angani, nikawa sielewi nini kinachotaka kutokea.

Cha ajabu ni kwamba, yule aliyekuwa akianza kupaa ndiyo alikuwa mimi kwa sababu nilikuwa najitambua kabisa, nikainamisha kichwa na kutazama chini, nikajiona nikiwa nimekaa pale juu ya zulia, nikiwa nimeshikana mikono na yule mwenyeji wetu, Raya na Firyaal, jambo ambalo lilisababisha hofu kubwa ndani ya moyo wangu.

“Noo! Sitaki kufa tena, sitakiii,” nilisema kwa sauti ya juu, nikashtukia nikiporomoka kutoka pale juu nilipokuwa nikielea, nikaanguka chini kama furushi na kujibamiza sakafuni kwa kishindo.

Nilipofumbua macho, kila mtu alikuwa amepigwa na butwaa akiwa ni kama haamini kilichotokea, nikawa nahema kwa nguvu huku nikiwa nimelala sakafuni, sikukumbuka hata niliwaachia wenzangu mikono saa ngapi, wote wakabaki kunishangaa.

“Hutaki kufa tena? Unamaanisha nini?” aliniuliza yule mwenyeji wetu, nikainuka pale nilipokuwa nimeanguka na kukaa, nikawa nawatazama mmoja baada ya mwingine huku nikijihisi aibu kubwa usoni.

“Naongea na wewe kijana, vipi mbona sikuelewi?” yule mwenyeji wetu alizidi kunibana kwa maswali lakini sikuwa na cha kujibu, Raya na Firyaal wote wakawa wanaendelea kunitazama kwa macho ya mshangao, kila mmoja akionesha kuwa na shauku kubwa ya kutaka kusikia nitajibu nini.

“Hata sielewi kilichotokea,” nilisema, wote wakashusha pumzi ndefu na kutazamana.

“Hebu naombeni mtupishe mara moja mimi na Jamal, alisema yule mwanamke ambaye kiumri alikuwa mtu mzima, Raya na Firyaal wakasimama na kutoka mle chumbani, wakaenda kukaa sebuleni, nikawa nawasikia wanazungumza lakini sikuelewa walikuwa wakizungumzia nini ingawa nilijua kwamba walikuwa wakiniongelea.

“Hebu niambie ukweli, umeona nini au kipi kilichokutokea?” aliniuliza mwanamke huyo wa makamo, mweupe na mnene kiasi, niligeuka huku na kule na nilipohakikisha tupo wawili tu, nilimuuliza swali juu ya swali.

“Umesema OBE ni nini?”

“Mbona nakuuliza swali unaacha kunijibu na wewe unaniuliza? Tupo nyuma ya muda na tunatakiwa kufanya haraka kumsaidia Shamila, niambie nini kimetokea?”

“Ninachotaka kukwambia kinahusiana na hiyo OBE na nahisi hii si mara ya kwanza kutokewa na hiki kilichonitokea,” nilimwambia, kwa mara nyingine akashusha pumzi ndefu na kunitazama. Nadhani alihisi kwamba sikuwa huru kuzungumza kwa sababu mara kwa mara nilikuwa nikigeuka na kutazama mlangoni.

Ikabidi ainuke na kwenda mpaka mlangoni, akaufunga na kurudi pale nilipokuwa nimekaa, safari hii akanisogelea karibu huku akinitazama kwa macho ya udadisi.

“Shamila si ni rafiki yako?”

“Ndiyo.”

“Unamuamini?”

“Ndiyo. Vipi kwani?”

“Kama unamuamini Shamila basi nakuomba uniamini na mimi, your secrets are safe with me (siri zako zitakuwa salama ukiwa na mimi) aliongea kwa kuchanganya na Kiingereza kuonesha kwamba alikuwa ameenda shule. Kabla sijamjibu, akaendelea:

“Nikikutazama kuna kitu nakiona lakini siwezi kukielezea mpaka mwenyewe uniambie. Halafu inaonekana kuna jambo halipo sawa kwenye mwili wako, una wapenzi wangapi?” aliniuliza swali ambalo lilinishtua sana, nikashindwa kumuelewa alikuwa ameona nini kwangu na swali lile lilikuwa na uhusiano gani na nilichomuuliza.

Nikashindwa cha kumjibu zaidi ya kubaki nikimkodolea macho usoni, akanishika mkono na kunifanya nizinduke. Sijui kwa nini hali ya mawazo kutengana na mwili wangu ilikuwa ikinitokeatokea sana safari hii. Yaani ilikuwa unaweza kuniona nakutazama ukahisi akili zangu zipo pale lakini kumbe nikawa nawaza kitu kingine tofauti kabisa.

“Shamila ni mwanangu, mimi ni mama yake mdogo kwa hiyo nakuomba tena usiwe na wasiwasi unapokuwa na mimi, hebu nijibu maswali yote niliyokuuliza, sawa baba,” aliongea kwa lugha ya upole na kubembeleza, nikashusha pumzi ndefu na kidogo nikaanza kuhisi amani ndani ya moyo wangu.

“Nina mpenzi mmoja tu, kwa nini umeniuliza?”

“Unajua kwa mtu mwenye utaalamu wa elimu ya nguvu zisizoonekana kama mimi, nikikutazama tu naweza nikajua wewe ni mtu wa namna gani. Nikikuangalia naona kama kwa siku za hivi karibuni umekutana kimwili na zaidi ya mwanamke mmoja na inaonesha pia upo kwenye mipango ya kufanya hivyo kwa wanawake wengine zaidi, kama nimekosea naomba unisamehe,” alisema yule mwanamke, kauli iliyozidi kunishangaza mno.

Alichokisema kilikuwa kweli, nilikuwa nimekutana kimwili na Raya na Shamila kwa kuwachanganya ingawa wenyewe hawakuwa wakijua chochote na kama hiyo haitoshi, nilikuwa kwenye mipango ya kufanya hivyo kwa Firyaal pia ambaye yeye ndiye aliyeonesha kunipenda mimi zaidi na kujikuta nikishindwa kuendelea kuvunga.

“Anyway, najua hayo ni mambo ya ujana tuachane nayo lakini kubwa nahisi kama umewahi kutokewa na jambo kubwa sana linalokufanya uwe tofauti na binadamu wengine na ndiyo maana hapa umekwamisha tulichokuwa tunataka kukifanya. Inaonesha una nguvu kubwa sana ambazo pengine hata wewe mwenyewe hujui na ndizo zinazokutesa,” alisema na kuzidi kunichanganya kichwa.

“Unamaanisha nini unaposema nguvu zisizoonekana?”

“Kwani wewe uliposema hutaki kufa tena na ukavuruga kazi tuliyokuwa tunaifanya ulimaanisha nini?” mfumo wa swali juu ya swali uliendelea kutawala katika mazungmzo yetu.

“Umewahi kufika kuzimu?” aliniuliza swali lingine, nikatingisha kichwa harakaharaka kukataa lakini alinigundua kwamba kuna jambo namficha.

“Hapo kifuani umefanya nini?” aliniuliza, eti na mimi nikawa najitazama kama najishangaa, akajua kwamba nilikuwa na mambo mengi ninayoyaficha, akazungumza kwa sauti yenye mamlaka sasa”

“Sikia, kama bado huniamini huwezi kuwa na msaada wowote katika hili tunalotaka kulifanya, itabidi wewe ukakae sebuleni utusubiri mimi na hao wenzako tufanye kinachowezekana kumuokoa Shamila, haupo tayari kushirikiana na sisi, yaani ni kama nakulazimisha hivi.”

“Hapana, siyo hivyo.”

“Siyo hivyo nini? Muda unazidi kuyoyoma, Shamila yupo kwenye matatizo, kila nachokuuliza unanichenga sasa unataka nifikirie nini?” alisema huku akisimama, akionesha kuchukia.

Siyo kwamba sikuwa tayari kumjibu maswali yake lakini alichonichanganya alikuwa akitaka kujua vitu vingi kwa wakati mmoja, wakati mambo yenyewe hayakuwa mepesi kuyafafanua mpaka mtu akaelewa.

“Nataka kumsaidia Shamila,” nilisema.

“Nijibu maswali yote niliyokuuliza.”

“Nitakujibu lakini itakuwa ni baada ya kumaliza kazi ya kumsaidia Shamila.”

“Hapana, wewe una nguvu kubwa sana ambazo mwenyewe hujui namna ya kuzitumia, unaweza kufanya tena kama hiki ulichokifanya hapa ukasababisha tudhalilike huko nje tunakokwenda.”

“Hapana, nitajitahidi naomba uniamini.”

“Unaniahidi?”

“Ndiyo,” nilisema kwa kujiamini, akanitazama usoni kisha akaenda mlangoni na kufungua, akawaita Raya na Firyaal, wakaingia ndani na tukakaa tena kama tulivyokuwa tumekaa mwanzo, kazi ikaanza upya huku akinisisitiza kuwa makini na kuishinda hofu ndani ya moyo wangu, nikatingisha kichwa kama ishara ya kukubaliana naye.

Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

Comments are closed.