SEVEN DAYS IN HELL (Siku Saba Kuzimu)- 56

ILIPOISHIA:

Harakaharaka nikafungua mlango nikiwa ni kama siamini nilichokisikia, nikamkuta Shenaiza akihangaika kujigeuza, jambo ambalo hakuwa amelifanya kwa kipndi kirefu tangu akiwa kule hospitalini.

“Shenaiza! Shenaiza,” nilisema huku nikipiga magoti pembeni ya kitanda chake. Bado hakuwa amefumbua macho yake.

SASA ENDELEA…

Hata hivyo, japokuwa hakuwa amefumbua macho, niliona akiyapepesa kama anayetaka kuyafumbua, nikainua mikono juu kama ishara ya kumshukuru Mungu. Kumbukumbu za yote yaliyotokea kuanzia siku ya kwanza msichana huyo aliponipigia simu mpaka muda huo zilipita kwa kasi ndani ya kichwa changu.

Kila kitu kilikuwa kikitokea kwa kasi kubwa ambayo ungeweza kudhani ni ndoto ya kusisimua na muda si mrefu nitazinduka. Kwa kuwa Junaitha aliniambia nikamsubiri chumbani kwake, sikukaa muda mrefu ndani ya chumba hicho cha Shenaiza kwa sababu nilijua hawezi kufurahi akinikuta nikifanya tofauti na maagizo aliyonipa, nikambusu Shenaiza kwenye paji la uso kisha nikatoka na kuelekea chumbani kwa Junaitha.

Maisha aliyokuwa akiishi mwanamke huyu yalikuwa na tofauti kubwa kati ya nje na ndani. Wakati kwa nje ungeweza kudhani Junaitha ni mwanamke ‘mayai’ anayependa sterehe na anasa, ndani ya nafsi yake alikuwa mtu mwingine kabisa. Nikaingia ndani ya chumba chake kilichojaa vitu vingi vya kisasa, tena vyote vya thamani kubwa na kwenda kukaa kwenye sofa dogo lililokuwa pembeni ya kitanda.

Japokuwa kimwili nilikuwa hapo lakini kiakili nilikuwa mbali sana. Nilianza kujiuliza kwamba yale yote yaliyokuwa yananitokea, yalikuwa na maana gani hasa? Nilifikia hatua hiyo baada ya kuona ni kama naishi kwenye ‘script’ fulani ambayo tayari maisha yangu yameshapangwa kwamba ni lazima nipitie hatua moja hadi nyingine kuelekea nisikokujua.

Hata mtu mwingine yeyote angeweza kufikiria hivyo kwa sababu kabla ya mfululizo wa mambo yote hayo, nilikuwa nikiishi maisha ya kawaida kabisa, nikifanya kazi kwa bidii nikiwa na ndoto nyingi maishani. Nilikuwa nikiishi kama kijana wa kisasa anavyotakiwa kuishi lakini kila kitu kilibadilika baada ya kukutana na Shenaiza.

Yaani ni kama nilikuwa nimelala na asubuhi kulipopambazuka kila kitu maishani mwangu kilikuwa kimebadilika. Nilimfikiria Raya na jinsi tulivyokuwa tukiishi naye kabla mambo hayajaanza kwenda mrama, nikamfikiria Shamila nilivyokutana naye nikiwa hospitalini na jinsi alivyotokea kunipenda na yote yaliyotokea mpaka muda huo ambao sasa nilikuwa kwenye himaya ya Junaitha, mwanamke ambaye hata sijui nimuelezee vipi.

Nilizinduka kutoka kwenye lindi la mawazo baada ya kusikia mlango ukifunguliwa, Junaitha akaingia huku akionesha kuchoka sana, nikamuona akiufunga mlango kwa funguo kisha akanisogelea pale nilipokuwa nimekaa.

“Nimechoka sana mume wangu,” alisema na kunibusu mdomoni, nikabaki nimeduwaa. Niliduwaa kwanza kwa kitendo chake cha kuniita ‘mume wangu’ kwa sababu kiumri alikuwa sawa na mama yangu mdogo au shangazi yangu lakini pia alinibusu mdomoni, miongoni mwa mambo ambayo yalikuwa yakiufanya mwili wake uwe kama umepigwa na shoti ya umeme.

“Yaani wewe pamoja na yote haya tuliyoyafanya pamoja bado tu hunizoei?” alisema baada ya kugundua kwamba nilikuwa nimepigwa na butwaa, nikajichekesha na kuvunga. Kiukweli baada ya kuuona upande wa pili wa Junaitha, nilikuwa hata sielewi mwanamke huyo ni mtu wa aina gani.

Kuna wakati hata nilikuwa nahisi kwamba hata kitendo cha mimi kujikuta nikifanya mapenzi na mwanamke huyo kilikuwa cha hatari sana kwa sababu kumbe alikuwa na uwezo mkubwa mno wa nguvu zisizoonekana kwa macho.

Kumbukumbu za tukio lililotokea muda mfupi uliopita la kumkamata yule mwanamke kichawi na kufanikiwa kumleta mle ndani, huku pia tukifanikiwa kulikimbia joka kubwa la kutisha katika ule ulimwengu wa giza, ziliufanya moyo wangu uwe na hofu kubwa mno.

“Leo umenifurahisha sana kwa sababu tumefanya kazi mbili kubwa ambazo zinatumia nguvu kubwa lakini katika zote, wewe ndiyo umekuwa kama steringi, si unaona wenzako hakuna aliyezinduka hata mmoja wakati hakuna kazi yoyote ya maana waliyoifanya?” alisema Junaitha huku akifungua vifungo vya blauzi yake na kuanza kuivua.

Wala hakuwa na wasiwasi wowote au hakuhisi aibu yoyote licha ya mimi kuwepo pale, akaivua na kuitupia kwenye kapu la nguo chafu, akabaki kifua wazi.

“Mbona unaniangalia hivyo wakati mimi nakusemesha mambo ya maana,” alisema huku akiachia tabasamu baada ya kugundua kuwa akili na mwili wangu havikuwa kwenye ushirikiano mzuri.

“Unajua mimi nina dharau sana kwa wanaume lakini sijui kwa sababu gani wewe nimetokea kukuamini na kukupenda ndani ya muda mfupi namna hii,” alisema huku akianza kuvua za chini, akatoa zote akiwa hana hata chembe ya wasiwasi, eti mimi ndiyo nikawa na kazi ya kukwepesha macho yangu kwa aibu mpaka alipochukua upande wa khanga na kujifunga.

“Hizi nguo ukishaenda nazo kule kwenye ulimwengu mwingine hutakiwi kuzivaa tena mpaka zifuliwe kwa maji yenye udi, mdalasini na karafuu, hebu acha ushamba wako,” alisema huku akinipiga kimasihara begani, akanishika mkono na kunisimamisha, akaanza kufungua vifungo vya shati langu.

“Si unaona unaelekea kupona, hebu sogea hapa ujiangalie,” alisema huku akilitazama vizuri jeraha langu la kifuani, nikasogea kwenye kioo na kujitazama. Ni kweli nilikuwa nimeanza kupona haraka kuliko hata nilivyotegemea.

Jeraha ambalo nilikaa kwa muda mrefu hospitalini lakini likawa bado hata haliponi, leo ndani ya saa chache tu lilikuwa likielekea kupona! Ilikuwa ni zaidi ya maajabu kwangu.

“Na pale mguuni alipokujeruhi yule mshenzi panaendeleaje?” alisema, nikataka nipandishe suruali juu ili nimuoneshe lakini badala yake, alinipa taulo na kuniambia nivue tu suruali kwa sababu kuna dawa nyingine alikuwa anataka tuitumie ili kutoa nuksi zote tulizotoka nazo kule kwenye ulimwengu wa giza.

Kwa jinsi Junaitha alivyokuwa anajua kunibembeleza kama mtoto mdogo, nilijikuta nikiishiwa na ile hofu iliyokuwa ndani ya moyo wangu, nikawa nafanya kila kitu alichonigiza. Muda mfupi baadaye, nilibaki na taulo tu, na yeye alibaki na upande wa khanga.

Akatembea kimikogo huku mwili wake uliojengeka vizuri kikekike ukitingishika kwa namna ya kuvutia sana, akaenda kufungua droo iliyokuwa pembeni ya kitanda, akatoa vichupa viwili vilivyokuwa na vitu kama mafuta, akanisogelea.

“Hii dawa inabidi ukaogee na hii ntakupaka tena kwenye kidonda chako, sawa baba’angu,” alisema huku akiwa amenisogelea sana, tukajikuta tumekumbatiana tena, tukagusanisha ndimi zetu.

“Nataka suala la yote tunayofanya mimi na wewe liwe siri yetu, umenielewa mume wangu,” alirudia tena kutamka neno lile, safari hii kwa sauti iliyokuwa inasikika kwa mbali kama mtu anayejilazimisha kuzungumza, nikaitikia kwa kutingisha kichwa, akanishika mkono na kunipeleka kwenye bafu la ndani ambapo alinielekeza namna ya kuogea ile dawa.

Cha ajabu, japokuwa yale mafuta hayakuwa na rangi, nilipoyajaribu kunawia mikono tu kama alivyonielekeza mwenyewe, nilishangaa mwili wangu ukitoa uchafu mwingi mweusi kama maji yaliyochanganywa na mkaa, nikawa nashangaa kwa hofu.

“Ule ulimwengu mwingine una mambo mengi machafu sana, usipojisafisha kwa hii dawa vizuri mwili mzima, unaweza kujikuta unabadilika na kuwa kiumbe wa ajabu sana,” alisema na kunifanya nishtuke sana.

“Oga fastafasta nakusubiri,” alisema huku akitoka na kuniacha bafuni, nikafanya kama alivyoniambia ambapo nilijipaka ile dawa mwili mzima na kusogea kwenye bomba la mvua, nikafungulia maji ambayo uchafu mwingi ulikuwa ukitiririka kutoka mwilini mwangu. Nilikaa kwenye maji kwa zaidi ya dakika tatu ndiyo uchafu wote ukaisha, nikashangaa ule uchovu wote niliokuwa nao umeyeyuka kama barafu juani.

Nikajifuta kwa taulo na kutoka mpaka chumbani ambako nilimkuta Junaitha naye ameshaenda kuoga, nadhani alitumia bafu la chumba kingine maana vyumba vingi ndani ya nyumba hiyo vilikuwa ‘self contained’, akanipokea kwa mabusu motomoto na kunitaka nijilaze kidogo pale kitandani kwake ‘tupunguze uchovu’.

Hata sijui nini kilitokea lakini muda mfupi baadaye, wote tulikuwa kama tulivyoletwa duniani, tukaianza safari tamu kwenye ulimwengu wa huba, ambayo lazima niwe mkweli, iliukonga mno moyo wangu, nikajikuta nimepitiliza na kuuchapa usingizi mzito.

“Jamal! Jamal! Amka, kuna tatizo,” sauti ya Junaitha ndiyo iliyonizindua kutoka kwenye usingizi fofofo, nikakurupuka nikiwana shauku kubwa ta kutaka kujua kumetokea nini tena.

Je, nini kitafuatia? Usikose next issue au bofya>>>Simulizi za Majonzi kusoma mwendelezo.


Loading...

Toa comment