The House of Favourite Newspapers

SH ELFU 14 TU KWENYE AKAUNTI YAKE, DINHO ANAENDELEA KUSOTA

HALI ni mbaya. Vyuma vimekaza. Unaweza kuchagua moja ya sentensi hizo mbili, ukiambiwa kuelezea hali ya kiuchumi ya bilionea wa zamani, gwiji wa soka, Ronaldinho Gaucho. Inafahamika kwamba fowadi huyu wa zamani wa Brazil aliyewahi kutamba na kuingiza fedha nyingi akiwa na klabu kadhaa ikiwemo Barcelona, amefilisika.

 

Lakini ‘mfilisiko’ huu kumbe ni babkubwa kwani asipokuwa makini anaweza kukosa hata hela ya kula. Tayari mamlaka za kodi nchini Brazil zinashikilia magari yake ya kifahari na bidhaa zake nyingine kutokana na muendelezo wa kushindwa kulipa faini wanayodaiwa.

 

Ronaldinho na kaka yake wanadaiwa faini ya shilingi milioni 1.75, na kwa mwanasoka huyo kushindwa kulipa kiasi hicho ambacho ni sawa na Sh bilioni 3 za Kitanzania, kinaonyesha kwamba hana kitu kabisa kwa sasa.

 

Paspoti ya nyota huyo, 38, mapema mwezi huu ilizuiwa kuto- kana na waendesha mashtaka kutaka kujiridhisha kuhusu kiasi cha pauni tano tu ambazo ni sawa na Sh 14,731 kukutwa kwenye akaunti yake. Hicho ni kiasi kidogo mno kwa mwanasoka ambaye aliingiza mabilioni ya fedha enzi zake akicheza.

 

Kutokana na kuwa na kiasi kidogo kwenye akaunti yake, polisi nchini Brazil wameenda mbali zaidi kwa kushikilia kila mali ya familia yake ili kuhakikisha kwamba supastaa huyo analipa faini yote anayodaiwa. Maofisa wamezishikilia gari zake za kifahari za BMW na Mercedes Benz katika jitihada za kufanikisha upatikanaji wa kiasi hicho anachodaiwa kutokana na taasisi yake ya kijamii kutibua mambo yahusuyo mazingira.

 

Jumla ya magari yake yaliyoshikiliwa ni matatu pamoja na kazi yake ya sanaa kutoka kwa mchoraji Andre Berardo, vitu vyote hivyo vilikutwa kwenye nyumba inayomilikiwa na familia ya Ronaldinho jijini Porto Alegre.

 

Hayo yote yametokana na taasisi yake iitwayo Ronaldinho Gaucho iliyo katika jiji hilo kushindwa kulipa faini kutokana na mamlaka kuikuta na hatia ya uharibifu wa mazingira katika ujenzi wa taasisi hiyo.

 

Imeelezwa kuwa kaka wa mchezaji huyo, Assis Moreira pamoja na Taaisisi ya Ronaldinho Gaucho Institute, ambayo imejikita kusaidia watoto na vijana wenye umri chini ya miaka 20, walipatikana na hatia ya uharibifu wa mazingira katika mahakama ya Rio Grande do Sul mwaka 2013. Walipatikana na hatia ya kukata misitu na kusababisha ukame na mmomonyoko wa ardhi bila kuwa na leseni.

Inaelezwa taasisi hiyo baada ya kushindwa mahakamani mwaka huo, ilisaini hati ya kulipa kwa ajili ya marekebisho ya uharibifu huo, lakini haikufanya hivyo hadi leo. Mwanasheria wa familia ya Ronaldinho, Sergio Queiroz, alithibitisha kwamba magari na baadhi ya vitu vimeshikiliwa na akasisitiza kuwa watakuwa na mkutano na mamlaka husika ili kujaribu kulitatua suala hilo.

 

Kiasi hicho wanachodaiwa kinatajwa kuwa ni pauni milioni 1.75 ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni tatu. Hata hivyo, suala ambalo limebaki gumzo kubwa kwa wengi ni kitendo cha akaunti ya Ronaldinho kukutwa na pauni tano tu, ambazo ni Sh elfu 14. Suala hilo limeonekana kuwashangaza wengi, hasa kwa mchezaji aliyekusanya mabilioni ya fedha kutoka kwa timu kubwa kama Paris SaintGermain, Barcelona na AC Milan.

 

Ronaldinho aliyewahi kuwa Mchezaji Bora wa Dunia wa Fifa mwaka 2004 na 2005, amekuwa na maisha mengi ya starehe na kujirusha mfululizo tangu alipostaafu soka mwaka 2015. Pia amekuwa akiripotiwa mara kwa mara kupenda vimwana, kuwahonga fedha nyingi, lakini hata wakati akicheza, maisha yake ya nje ya uwanja yalijaa anasa nyingi.

 

Akimtaja Ronaldinho kama “Mtoto jinias wa Kibrazili ambaye hakui”, mwandishi Tim Vickery aliwahi kueleza kuwa kifo cha baba yake wakati mwanasoka huyo akiwa mdogo sana, kimeathiri saikolojia yake na kumfanya asijitoe kikamilifu kufikia levo za juu zaidi.

 

Ronaldinho, mwenye mtoto mmoja anayejulikana, alipata madili mengi yaliyomuingizia fedha kibao, ndiyo maana habari za kufilisika kwake zimewashtua wengi. Alipata madili ya matangazo na kampuni kubwa kama Nike, Pepsi, Coca-Cola, EA Sports, Gatorade na Danone.

 

Na akiwa mmoja wa wachezaji waliolipwa fedha nyingi zaidi duniani mwaka 2006, alipata zaidi ya dola milioni 19 (zaidi ya Sh bilioni 43.6) kutokana na matangazo tu. Leo hii inakuwaje pauni milioni 1.75 inamdhalilisha? Kuna cha kujifunza hapo.

KOCHA ZAHERA ” Wachezaji Wanalia /Sitaki Kombe la Ubingwa”

Comments are closed.