The House of Favourite Newspapers

Shahidi Aanika Mazito Kesi ya Kina Aveva

SHAHIDI namba saba wa kesi inayowakabili waliokuwa viongozi wa Simba, Evans Aveva na wenzake, Frank Mkilanya(45) ameieleza mahakama jinsi nyasi za Uwanja wa Bunju zilivyonunuliwa.

 

Shahidi huyo ambaye ni Mchunguzi kutoka Takukuru, aliendelea kutoa ushahidi wake jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwenye kesi ya waliokuwa viongozi wa Simba rais, Evans Aveva makamu wake Godfrey Nyange (Kaburu) na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Zachariah Hans Pope.

 

Shahidi huyo aliulizwa maswali na mawakili wa washitakiwa ambao ni Nehemiah Nkoko, Wabaye Kunge na Benedict Inshabakati. Mkilanya aliiambia mahakama kuwa licha ya kufanya uchunguzi lakini hafahamu ni nani ambaye alipeleka taarifa za Simba ila yeye alipewa kazi za kuchunguza tu.

 

“Mimi nilipewa kazi ya kuchunguza ila sifahamu nani aliyelalamika kuhusu haya madai ya Simba,”alisema Mkilanya na Kuthibitisha fedha za mauzo ya Emmanuel Okwi kutoka kwa klabu ya Etoile du Sahel dola 300,000 ziliwekwa kwenye akaunti binafsi ya Evans Aveva (rais Simba).

 

Mkilanya aliiambia mahakama kuwa Aveva alieleza kuwa alikuwa na mamlaka ndani ya Simba na alikuwa mwenyekiti wa kamati ya utendaji ambao walikubaliana kuwa fedha za Okwi zitumike kwenye masuala ya uwanja wao wa Bunju.

 

Shahidi aliiambia mahakama kuwa katika fedha ambazo zilitoka kwenye akaunti ya Aveva ilikuwa ni kiasi cha dola 50,000 ambazo alipewa mkandarasi wa Uwanja wa Bunju, Dola 17, 000 alilipwa kocha wa Simba Kerr (Dylan) na kiasi cha dola 62,000 zilinunuliwa nyasi bandia kwa awamu tatu.

 

Haikuishia hapo shahidi huyo alieleza mahakama kuwa katika uchunguzi wake inaonyesha Hans Pope alianza mchakato wa kununua nyasi bandia hata kabla ya fedha za Okwi hazijafika Simba na wala ile ‘Invoice’ ya Dola 40,000 ya nyasi bandia hakuipeleka TRA.

 

Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba aliahirisha kesi hiyo ambayo itaendelea leo katika mahakama ya Kisutu. Ikumbukwe katika mashtaka mengine inadaiwa Aveva, Nyange na Hans Poppe kati ya Machi 10 na Septemba 30, 2016 waliwasilisha nyaraka za uongo kuonyesha Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Kimarekani 40,577.

Comments are closed.