Staa wa filamu za Kibongo, Shamsa Ford.
TAMBO na majigambo yameanza kutapakaa kati ya Simba na Yanga kuelekea mchezo wa watani hao, Oktoba Mosi, mwaka huu huku staa wa filamu za Kibongo, Shamsa Ford akiibuka na kusema kuwa anawaonea huruma Simba kwani wajiandalie mateso siku hiyo kama ilivyowakuta msimu uliopita.
Ikumbukwe timu hizo zinakutana ikiwa Yanga ina kumbukumbu nzuri ya kuichapa Simba nje-ndani msimu uliopita ambako iliifunga mabao 2-0 kwenye mechi za ligi kuu walizokutana.
Hata hivyo, Simba ya safari hii imeonekana kuwa mpya kwani kwenye kikosi cha kwanza kilichofungwa wamesalia wachezaji wanne; Ibrahim Ajib, Jonas Mkude, Vincent Angban, Mohammed Hussein ‘Zimbwe Jr’ tofauti na Yanga ambayo wachezaji walioifungia ni walewale.
Pamoja na mabadiliko hayo, bado hayamtishi Shamsa ambaye anaamini ubora wa Yanga ni uleule kama msimu uliopita na kichapo kipo palepale Oktoba Mosi, akipewa kiburi na uwezo wa mchezaji mmojammoja.
“Siku zote Yanga hatukosei na (Simba) wajiandae na kichapo siku hiyo. Kama walikubali mara mbili msimu uliopita, nini kipya zaidi cha kutuzuia kuwafunga? Timu yetu ipo vizuri, kutoka mchezaji na mchezaji bado Yanga ni bora kulinganisha na Simba na ndiyo maana najiamini lazima wafe tu,” alisema staa huyo wa Filamu za Chausiku, Shikamoo Mzee na nyingine nyingi.
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza msimu uliopita, Yanga ilifunga kupitia Amissi Tambwe na Malimi Busungu kabla ya Tambwe kufunga tena kwenye mzunguko wa pili pamoja na Donald Ngoma.
Comments are closed.