SHEHE Ahmed Kandauma kutoka taasisi ya dini ya Kiislam IRSHAD ya Temeke jijini Dar amemuwakia msanii Nasibu Abdul ‘Mondi’ au Diamond kwa kile alichodai kuwa msanii huyo anakiuka misingi ya dini.
Kuwaka kwa shehe huyo kumekuja siku chache baada ya Mondi kumfanyia mwanaye Naseeb Jonior sherehe ya Arobaini iliyoambatana na Dufu lenye vionjo vya muziki wa kidunia maarufu kama ‘muziki moto’.
“Suala la uhalali wa mtoto silisemei kwa sababu linajulikana, lakini nazungumzia kufanya sherehe inayoitwa ya dini ya Kiislam halafu unachanganya na mambo ya kidunia.
“Niliona kwenye mitandao ya kijamii jinsi akina mama na akina baba walivyokuwa wanacheza, sijui ndiyo huo muziki moto au kingine.
“Sina ubaya na Diamond lakini anatakiwa kuchagua, kama anataka kuwa mtu wa kidunia awe; asichanganye mambo.
“Kibaya zaidi kwenye matukio mengi ambayo amekuwa akiyabatiza jina la kidini, kuna mashehe wenzangu huwa nawaona kwenye hizo sherehe; hata hii ya juzi (arobaini ya Naseeb Junior) walikuwepo lakini hawamkemei.
“Sijui wanakuwa wamepofushwa na nini au wanamuogopa kumuambia kwa sababu ni mtu maarufu? Kwa Mungu hakuna upendeleo,” alisema shehe Kandauma.
AZUNGUMZIA NDOA
Kuhusu Diamond kuendelea kuishi bila ndoa, shehe Kandauma alisema nalo si jambo jema.
“Suala la ndoa ni Sunna, mtu halazimishwi kuoa lakini zinaa inakatazwa sana kwenye maandiko.
“Mtu ambaye hawezi kuzuia tamaa yake ya ngono habembelezwi kuoa, ni lazima kwake kwa sababu asipooa na akaendelea kuzini atafikia motoni.
“Namwambia kijana mwenzangu Diamond aoe; aache kuzaazaa nje ya ndoa ni haramu kufanya hivyo,” alisema shehe huyo.
Hadi sasa Diamond ana watoto wanne ambao amewazaa nje ya ndoa kwa wanawake watatu tofauti.
Kwa mpenzi wake wa zamani Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’, Mondi amezaa watoto wawili ambao ni Tiffah na Nillan ambapo kwa Hamisa Mobeto msanii huyo amebahatika kupata mtoto mmoja aitwaye Daylan.
Kwa mpenzi wake wa sasa Tanasha Donna raia wa Kenya, Mondi amefanikiwa kuzaa naye mtoto mmoja kwa kiume aitwaye Junior.
SI MARA YA KWANZA MONDI KUONYWA
Kutokana na kukiuka misingi ya dini kwa baadhi ya mambo Mondi amekuwa akishukiwa mara kwa mara na viongozi wa dini ya Kiislam.
Januari mwaka huu Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa alimshukia Mondi na kulaani kitendo chake cha kujitokeza mbele ya viongozi wa dini akiwa na mpenzi wake Tanasha ambaye alikuwa amevaa nguo isiyostili vyema maungo yake.
Shehe huyo wa mkoa amekuwa akimshukia Mondi katika masuala mbalimbali kama ya kutokuoa, kuacha kujimwambafai kwa kuonesha ufahari wa fedha hadharani na kujiepusha na masuala ya zinaa.
MUZIKI MOTO WAPIGWA MARUFUKU
Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zuberi Desemba 9, mwaka huu alipiga marufuku dufu na kaswida maarufu kama ”mziki moto” ambazo alisema zinaaibisha na kuchafua sura ya uislamu.
Hata hivyo, siku chache baadaye Mondi aliruhusu dufu la aina ya “muziki moto” kupigwa na kuchezwa kwenye sherehe ya mwanaye na kuwafanya baadhi ya watu kumuona kama mtu asiyesikia maonyo.
MONDI ASIFIWA
Mbali na kumkosoa katika baadhi ya mambo, shehe Kandauma hakusita kumsifia Mondi kwa kusema ni mtu mzuri kwenye jamii.
“Mimi kama mtu wa dini, nimesemea mambo ambayo mtoto wa Kiislam anatakiwa kuyazingatia, lakini upande mwingine Diamond ni mtu mzuri.
“Nimekuwa naona anasadia jamii, anawasaidia watoto yatima, ni mambo ya heri kabisa. Lakini akitaka yawe na nguvu kabisakabisa basi ajitahidi kumcha Mwenyezi Mungu na kufuata alichoagiza.”
Mkurugenzi, Mariam Sabaha akimkabidhi mshindi zawadi.
MWANDISHI WETU, RISASI