The House of Favourite Newspapers

SHETTA KUTOKA KUTENGWA NA BABA HADI KUMILIKI TAASISI

YAWEZE-KANA ulikuwa hujui! 2007 katika mitaa ya Mchiki-chini Boma pande za Ilala jijini Dar kulikuwa na dansa mmoja hatari ambaye alikuwa ndani ya kundi la Misifa Camp lililokuwa likiongozwa na mkongwe wa Bongo Fleva, Prince Dully Sykes.

Baada ya mwaka mmoja kupita yaani 2008, dansa huyo alipanda cheo na kuwa muitikiaji ‘backup singer’ wa Dully Sykes ambapo alidumu kwa mwaka mmoja na kuamua kuingia rasmi kwenye muziki.

Huyo si mwingine bali ni Nurdin Bilal wengi wanamfahamu kwa jina la Shetta baada ya kuachia ngoma yake ya kwanza ya Mi Naplay akimshirikisha MwanaFA.

Licha ya kutamba na ngoma hiyo, Shetta aliachia ngoma mfululizo kila mwaka ambazo ni Nimechokwa akiwa na Belle9, Mdananda akiwa na bosi wake wa zamani, Dully Sykes, Nidanganye akiwa na Diamond Platnumz, Bonge la Bwana akiwa Linah, Sina Imani akimshirikisha Rich Mavoko, Kerewa akiwa na Diamond, Shikorobo akivuka boda na kumshirikisha KCEE wa Nigeria na nyingine kibao.

Shetta kwa sasa anabamba na Ngoma ya Hatufanani akiwashirikisha Jux pamoja na Mr Blue ‘Byser’. Mbali na kufanya poa katika ngoma hiyo, Shetta ameamua kugeukia pia kusaidia jamii kupitia taasisi yake ya Shetta Foundation.

Mikito Nusunusu limefanya naye exclusive interview juu ya kuanzisha taasisi hiyo ambayo inamfanya kuwa miongoni mwa mastaa wakubwa nchini wenye taasisi.

MIKITO: Hongera kwa kufungua taasisi yako, unaweza kutuambia inadili na vitu gani?

SHETTA: Ni taasisi ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake, watoto na wazee ikiwa ni sehemu ambayo nimeamua kufanya hivyo kutokana na maisha ambayo nimepitia katika makuzi yangu.

MIKITO: Makuzi gani ambayo umepitia hayo?

SHETTA: Ni kwamba mimi ni mmoja wa watu ambao nimepitia malezi magumu kutoka upande wa mama, baba hakuwa na mimi kipindi chote lakini mama alijitahidi kadiri ya uwezo wake kunilea.

Kutokana na maisha yalivyokuwa duni ikabidi wajomba zangu waingilie kati na kunisaidia mpaka nikafanikiwa kusoma ila mama naye alikuwa akinipigania kuona mimi nafanikiwa.

MIKITO: Lakini kwenye taasisi hii mama amekusapoti kwa kiasi kikubwa?

SHETTA: (anainama kwa muda na kufikiria kitu) Kitu ambacho kiliniumiza ni pale ambapo alipofariki dunia 2006, hicho kitu kimechangia pia niamue kuanzisha hii kampeni ya kupinga ukatili maana mama yangu alifariki kutokana na msongo wa mawazo.

Kwa hiyo mimi natoa ushirikiano kwa serikali ili kutokomeza ikiwezekana kupunguza au kuondoa ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

MIKITO: Kuna watu unashirikiana nao katika hiyo taasisi?

SHETTA: Nashirikiana na serikali pamoja na jamii.

MIKITO: Nini malengo yako ya baadaye?

SHETTA: Kujaribu kuangalia uwezekano wa kupunguza na kutokomeza tatizo hili kwenye jamii kwa kushirikiana na serikali kwa sababu ina mkono mrefu kwa pamoja tunaweza kuwafikia watu wengi.

MIKITO: Vipi kuhusu changamoto unazozipata ikiwa wewe ni msanii wa muziki?

SHETTA: Ni kwamba utakuta kuna baadhi ya watu wanabadilisha maneno na kusingiziwa vitu vingi. Utakuta mengi ni maneno yasiyokuwa na ukweli huwa inaumiza lakini kwa kuwa nimeshakuwa msanii mkubwa changamoto hii siwezi kuiepuka.

MIKITO: Umelenga kuwasaidia wanawake wa aina gani?

SHETTA: Nimelenga kuwasaidia wanawake wote wenye changamoto za kimaisha ndiyo maana nasema taasisi hii itasaidia wale wote wahanga ikiwemo wanawake, watoto na wazee.

Comments are closed.