The House of Favourite Newspapers

Shiboub Kutimka Simba SC

0

KIUNGO mchezeshaji fundi raia wa Sudan, Sharraf Eldin Shiboub huenda akaachana na timu hiyo mwishoni mwa msimu huu wakati mkataba wake utakapomalizika.

 

Mchezaji huyo anayemudu kucheza namba 8, 10 na 11 alijiunga na Simba msimu huu akisaini mkataba wa mwaka mmoja wa kuichezea timu hiyo.

 

Shiboub amebakisha miezi mitatu katika mkataba wake na kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), hivi sasa anaruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu nyingine itakayomuhitaji kuelekea msimu ujao.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi kutoka ndani ya uongozi wa timu hiyo, kiungo huyo atatimka baada ya kupoteza namba katika kikosi cha kwanza tangu alipokabidhiwa timu hiyo Mbelgiji Sven Vandenbroeck.

Mtoa taarifa amesema kuwa, kiungo huyo kipindi cha aliyekuwa Kocha Mkuu, Mbelgiji Patrick Aussems alikuwa akipata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza lakini mambo yamebadilika kwa sasa.

 

Aliongeza kuwa tayari baadhi ya klabu kutoka Misri na Afrika Kusini zimeonyesha nia ya kuhitaji saini yake ya kwenda kukipiga kwenye moja ya klabu kubwa msimu ujao.

 

“Shiboub hivi sasa hana furaha kwenye timu tangu alipokuja kocha Sven ambaye ameonekana hampi nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza tofauti na alivyokuwepo Aussems.

 

“Hali hiyo imesababisha kusiwepo maelewano mazuri kati ya kiungo huyo na kocha wake Sven, hivyo hivi sasa yupo kwenye mipango ya kuihama timu hiyo mara baada ya mkataba wake kumalizika.

 

“Tayari baadhi za klabu zimeanza mazungumzo naye ya kumsajili huku Simba ikiwa katika mipango ya kumuongezea mkataba, licha ya yeye mwenyewe kutokuwa tayari kubaki,” alisema mtoa taarifa.

 

Kiungo huyo hivi sasa yupo nyumbani kwao Sudan akiwa kwenye mapumziko ya muda mfupi tangu serikali ilipotangaza kusimamisha ligi kutokana na Virusi vya Corona.

 

Aidha, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa hivi karibuni alisema kuwa: “Uongozi wa timu hiyo umepanga kuwabakisha wachezaji wote wanaowahitaji hasa wale ambao mikataba yao inamalizika mwishoni mwa msimu huu.”

STORI: WILBERT MOLANDI

Leave A Reply