The House of Favourite Newspapers

Shigongo Amrejesha CCM Mwenyekiti wa Chadema – Video

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendelea kupata pigo baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Jimbo la Buchosa, Jaji Tasinga kutangaza kurejea Chama Cha Mapinduzi (CCM).

 

Tasinga ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa muda wa wilaya wa Sengerema kupitia Chadema, alimshukuru kada wa CCM mkoani Mwanza, Eric Shigongo, kwa kumtia moyo na kuona umuhimu wa kurejea ndani ya chama hicho.

 

Tasinga ambaye kabla ya kuhamia Chadema mwaka 2015, aliwahi kuwa Mwenyekiti wa CCM wilaya hiyo ya Sengerema, alipokelewa jana na wajumbe wa Mkutano wa Jimbo ambaopo Mgeni Rasmi alikuwa Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Herry James.

 

Akizungumza na mwandishi wetu baada ya kumalizika kwa mkutano huo, Tasinga alisema sababu mojawapo iliyomsukuma kuondoka Chadema na kurejea CCM ni mazingira ya kisiasa.

 

Alisema awali akiwa ndani ya CCM mwaka 2015 alikumbana na zahama kwa familia yake kupewa misukosuko kutokana na sababu za kisiasa zilizosababishwa na baadhi ya watu wilayani humo.

 

“Nilikuwa najaribu kuomba msaada wa viongozi wa CCM lakini hawakunisikiliza licha ya kwamba alikuwa mtu mmoja tu alikuwa akiitikisa sana familia yangu hadi mke wangu kuachishwa kazi, ndiyo maana nikaamua kuhamia Chadema.

 

“Ila namshukuru sana Shigongo, amenitia moyo na kunieleza ukweli kuwa kutokana na uchapakazi wangu bado nahitaji sana CCM. Pia nawashukuru Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Sengerema Augustino Makoye, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) wilayani humo, Constancia Faida na Mzee John Maduka, wameniunga mkono pakubwa kurejea kwangu CCM,” alisema.

 

Aidha, akizungumzia kurejea kwa Tasinga, Shigongo ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Global Publishers alisema ni dhahiri kiongozi huyo wa zamani wa CCM alikuwa ni mtu muhimu kwenye chama na ilikuwa inamuuma kuhamia Chadema.

 

“Ilibidi kutumia kadiri ya uwezo wangu wote kumrejesha CCM ili akitumikie chama na kumsaidia rais kuleta maendeleo kwa wananchi.  Tasinga ni mtu mzuri, mchapakazi, ila kuna mambo yalimkera akaamua kuhama CCM kwa hasira, ndiyo maana nikaamua kuzungumza naye ili kumrejesha CCM,” alisema Shigongo.

 

Naye Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Salum Kalili,  alishukuru kurejea kwa Tasinga na kubainisha kuwa baada mkutano kumalizika atazungumza kwa kina kuhusu mapokeo ya kiongozi huyo.

 

Tasinga alikuwa Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Sengerema kwa muda wa miaka 10 kuanzia 1998 hadi 2008, na alikuwa Mwenyekiti wa CCM wilaya hiyo kuanzia mwaka 2007 hadi 2012 kabla ya kuhamia Chadema mwaka 2015.

 

NA MWANDISHI WETU

Comments are closed.