The House of Favourite Newspapers

SHIGONGO AMWANDIKIA BARUA YA WAZI RAIS MAGUFULI

Rais Magufuli akizungumza na Mtukufu Aga Khan.

 

MHE. RAIS, TUSAIDIE HOSPITALI YA AGA KHAN IPOKEE BIMA YA N.H.I.F

MHESHIMIWA Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli.

Nakusalimia kwa heshima zote.

Mimi ni raia wa Tanzania ambaye Mungu kwa neema yake tu nimejaliwa uwezo wa kuugua na nikatibiwa hospitali kama Aga Khan, hii kwangu ni neema na huruma za Mungu. Lakini watu wachache pekee kuwa na uwezo huo haitoshi katika nchi yenye watu milioni 55 si jambo jema sana.

 

Nafahamu tunazo hospitali nyingi hapa nchini zinazomilikiwa na Serikali, lakini kivifaa na kiteknolojia ukiondoa Muhimbili, nyingi zinaweza kuwa hazifikii au kulingana na hospitali hii, hivyo basi wapo Watanzania wengi ambao wangetamani kupata matibabu katika hospitali hii ambayo pengine ni kubwa kuliko zote Afrika Mashariki kwa sasa baada ya upanuzi na uwekezaji wa dola zaidi ya milioni 40 uliofanyika hivi karibuni.

 

Mheshimiwa Rais, najua kwa barua hii kwako nitachukiwa na baadhi ya watu na tayari huko nyuma nilishachukiwa kwa sababu ya jambo hili, lakini nionavyo mimi ni bora kusema ukweli hata kama utachukiwa, Mheshimiwa Rais hii ndiyo tabia yangu; kusema ukweli kwani msema kweli ni mpenzi wa Mungu.

 

Najua unafahamu, Mheshimiwa Rais kwamba hospitali hii imesajiliwa kama NGO, shirika lisilotengeneza faida katika shughuli zake, hivyo basi hailipi kodi yoyote serikalini, kama nchi hatuingizi chochote kutokana na mapato yake zaidi ya kutibu watu wenye uwezo na kuwaponyesha.

 

Pamoja na kusajiliwa kama NGO, Hospitali ya Aga Khan, acha nitumie Kingereza kidogo; it is probably the most expensive hospital in the country. (Ni hospitali ambayo matibabu yake ni ya gharama kubwa pengine kuliko hospitali nyingine yoyote nchini).

 

Kinachonisikitisha zaidi Mheshimiwa Rais, ambacho kwa kweli nimekipigia kelele kwa muda mrefu bila mafanikio ni kitendo cha hospitali hiyo kutopokea wagonjwa wenye Bima ya Afya ya Taifa (NHIF), kitendo ambacho mimi hukitafsiri kama kuwatenga wanyonge wa nchi hii, ambao ndiyo Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na wewe imejipambanua kwamba inawatetea.

 

Binafsi, Mheshimiwa Rais, sina chuki yoyote na hospitali hii wala Taasisi ya Aga Khan, imenisaidia sana mimi mwenyewe binafsi na familia yangu, kwa muda mrefu marehemu mama yangu alitibiwa hapo kabla hajaanza kutibiwa Muhimbili ambapo pia huduma za afya kwa hivi sasa ni bora. Tatizo langu na taasisi hii limekuwa ni kwa nini hawataki kabisa kupokea bima ya NHIF kwenye hospitali yao kuu?

 

Mheshimiwa Rais, sitanyamaza mpaka siku utengaji huu utakapoondolewa, kwa muda mrefu nimekuwa katika mapambano haya bila mafanikio lakini sitachoka. Kama Watanzania watakumbuka, mara ya mwisho kiongozi wa Madhehebu ya Shia Ismailia duniani, Mtukufu Prince Aga Khan ambaye ndiye mmiliki wa hospitali hizo alipokuja nchini, niliandaa mabango nikijaribu kufikisha ujumbe kwako ili upate kumtaka Prince Aga Khan akubali kupokea bima ya afya kwenye hospitali yake kuu iliyopo Barabara ya Barack Obama karibu na Gymkhana jijini Dar es Salaam.

 

Nakumbuka katika maongezi yako na Prince Aga Khan Ikulu, ulisisitiza aziangalie upya gharama zake za matibabu, siamini kama jambo hilo limekwishafanyika, ila ninachofahamu ni kwamba bado hospitali hiyo haipokei bima ya afya ya taifa, jambo ambalo linalalamikiwa na Watanzania wengi, si mimi peke yangu.

 

Naomba niseme wazi kabisa na Watanzania wanielewe, siidharau taasisi hii hata kidogo, mchango wake kwa Watanzania ni wa miaka mingi na unapaswa kuheshimiwa, pamoja na yote niliyoyafanya katika taifa hili, sijafikia hata 0.0001 ya kile ambacho Aga Khan amefanya katika nchi yetu.

 

Alikuwa rafiki mkubwa wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, lakini pia ni mwekezaji mkubwa wa nchi hii katika nyanja za elimu, utafiti, benki, mawasiliano, utalii, kama nikitaja vichache tu. Jambo moja tu linalonishangaza na ambalo linaweza kuonekana kama linanichonganisha na taasisi hiyo ni kutokubali bima ya afya ya taifa kwenye hospitali yao kuu. Tatizo liko wapi?

 

Ninachoomba mimi raia wa nchi yako, Mheshimiwa Rais, ni kwamba utumie ushawishi na uwezo wako ili Hospitali ya Aga Khan iliyopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam ipokee kadi za NHIF, hakika utakuwa umeokoa maisha ya Watanzania wanyonge kwani ni hospitali kubwa yenye kila aina za vifaa, ukizingatia hivi sasa imepanuliwa zaidi kiasi cha kuwa pengine hospitali kubwa kuliko zote Afrika Mashariki, sasa ni kwa nini Mtanzania wa kawaida asifaidi huduma hizi? Ana makosa gani?

 

Mheshimiwa Rais, nakuomba sana usaidie katika jambo hili. Najua unao uwezo wa kufanya litokee, umeweza kujenga ‘standard gauge’ jambo ambalo katika macho ya wengi lilikuwa haliwezekani, kweli ushindwe kuishawishi Hospitali ya Aga Khan ipokee wagonjwa wa bima ya afya ya Taifa?

 

Mheshimwa Rais, tusiseme tu kuwa; “Anayetaka kwenda Aga Khan amependa mwenyewe, mbona Muhimbili na hospitali nyingine za Serikali zipo?” Ni kweli, lakini ni vyema kukumbuka kwamba Hospitali ya Aga Khan ina vifaa vingi na ni kubwa kwa sasa kuliko hospitali zetu nyingi, sasa ni kwa nini Watanzania wanyonge wasifaidi huduma za hospitali hii iliyomo katika nchi yao na inafanya biashara kubwa ikiwa imesamehewa kodi zote, sababu tu ni shirika la dini?

 

Mheshimiwa Rais, nisikuchoshe, una majukumu mengi, naomba leo niishie hapa, nitaendelea kukukumbusha tena siku za usoni juu ya jambo hili, nitanyamaza tu siku nitakapopumzika au litakaporekebishwa. Naamini ujumbe wangu utakufikia, naomba utusaidie.

 

Sitaki Taasisi ya Aga Khan watozwe kodi kwa sababu ni shirika la dini, ninachoomba mimi na pengine Watanzania wengi ni taasisi hii kukubali kupokea wagonjwa wenye kadi ya Bima ya Afya ya Taifa ambayo ina wanachama wengi wa kipato cha chini kuliko hizo nyingine za Jubilee, Strategies, AAR na kadhalika.

Asante Mheshimiwa Rais kuisoma barua yangu,

Mungu akubariki,

Mungu aibariki Tanzania na Watanzania wote.

Comments are closed.