Shigongo Awapa ‘Madini’ TCRA-SACCOS – Video

MHAMASISHAJI namba moja Afrika Mashariki na Kati, Eric James Shigongo, amewapa ‘madini’ wana-Ushirika wa Chama cha Kuweka na Kukopa cha Wafanyakazi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA – SACCOS) ili wajiandae kufurahia maisha yao mara baada ya kustaafu.

Shigongo alitoa somo hilo jana katika ukumbi mikutano uliopo ghorofa ya tatu katika ofisi za mamlaka hiyo zilizopo Mawasiliano Tower jijini Dar es Salaam jana Ijumaa, Septemba 13, 2019.

Akiwapa hamasa wafanyakazi hao, Shigongo aliwaeleza kuwa kustaafu siyo ajali, hivyo wanapaswa kujiandaa kwa kuweka mikakati, kubuni biashara ndogondogo na kuziendelea ili wakistaafu waishi kwa furaha maisha yao yanayokuwa yamesalia kwani wengi wao wamekuwa wakichelewa kujiandaa mapema na mwisho wa siku wakistaafu maisha yanakuwa magumu kwao, tofauti na ilivyokuwa wakati wakiwa kazini.

“Tunayo mifano mifano ya wastaafu wengi ambao hawakufanya maandalizi mapema, walipostaafu wakapokea pesa zao na walishindwa wafanye biashara ipi, na wengine hukurupuka kufanya biashara ambazo hawazijui vizuri na mwisho wa siku wakaishia kufilisika, kupata presha na kufa mapema,” alisema.

Aidha, aliwaasa wana-ushirika hao kuanzisha vyanzo vingi vya mapato badala ya kutegemea mshahara peke yake.

“Jiulize hapo ulipo leo, itakuwaje siku ukiamka huwezi tena kufanya kazi kama unavyofanya sasa hivi, maisha yako yatakuwa yaleyale? Utaendesha gari lilelile? Watoto wako utawapeleka shule ileile? Ili tufanikiwe, tusiamini katika chanzo kimoja cha mapato.

“Unaweza kuwa unafanya kazi hapa TCRA na ukaanzisha biashara yako nyingine ndogo huko mtaani ukaweka mtu makini na ukaingiza pesa. Biashara hiyo ikisimama unaanzisha nyingine tena. Lazima baada ya miaka minne hadi kumi utayapata mafanikio,” alisisitiza.

Mbali na hivyo, pia aliwaasa kuwekeza katika afya zao kwa kula vizuri lishe bora, kufanya mazoezi na kufanya vipimo na uchunguzi wa afya zao ili wahakikishe zipo imara.

“Lazima afya zetu tuzijali, afya ndiyo inakupa nguvu ya kufanya kazi, uzeeni kuna magonjwa mengi, kisukari, tezi dume, shinikizo la damu na magonjwa mengine, lazima tuwe na utamaduni wa kuwekeza katika afya ili tuendelee kuwa na nguvu ya mwili na akili wakati tukitekeleza majukumu yetu,” aliongeza Shigongo.

Pia aliwaasa TCRA-SACCOS kuwekeza katika watoto wao kwa kuwapa elimu iliyo bora kwani watakapozeeka, watoto wao ndiyo watakuwa na jukumu la kuwalea, hivyo wakiwaandalia maisha hata wazazi watalelewa kwa furaha katika uzee wao kwani watoto watakuwa na uwezo.

“Mpe elimu bora mwanao, wakati mwingine mpitishe katika shida ili ajifunze kuishi na watu, ajifunze changamoto na jinsi ya kuzitatua. Ukiwa na maisha mazuri halafu mwanao ukamwacha akavuta unga utakuwa na furaha?” alihoji na kuwataka wawalee watoto wao wawe raia wema watakaoitetea nchi yao na kupigania mafanikio yao na ya taifa.

“Ili ufanikiwe unapaswa pia kuwekeza katika watu, wainue vijana wadogo kwenye idara yako, mtaani mwako, waweze kufikia malengo yao. Siku ukichoka hawa ndiyo watakaokusaidia na wewe.

“Pia jifunzeni kuanzisha biashara zisizo na purukushani, nunua kiwanja eneo la karibu na barabara, jenga fremu za maduka na uzipangishe, utakuwa unaingiza pesa ukiwa umelala. Lakini pia usijifanye unaiweza kila biashara utapotea,” alitahadharisha na kuongeza:

“Kuwa makini na mambo ya mtaani, kuna matapeli na wauza dili za uongo, watakuingiza mkenge ‘utapigwa’ na kufilisika.

“Tumieni mabenki na taasisi za fedha kukopa na kuanzisha biashara, hizi zipo kwa ajili yenu, hakuna tajiri hata mmoja asiyekopa. Tumieni chama chenu cha TCRA-SACCOS kwa ajili ya maendeleo.”

Mhamasishaji na mjasiriamali huyo ambaye pia ni mmoja wa waandishi maarufu wa vitabu ndani na nje ya Tanzania, alimalizia kwa kuwataka watumishi hao kumrudishia Mungu kidogo kutokana na kikubwa wanachofanya na kukipata na pia kurudisha kwa jamii na wasiojiweza kama msaada ili wapate thawabu zaidi.

“Ninatoa somo hapa leo mnanilipa, hii pesa ninayoipata hapa leo siitumii hata senti moja, pesa hii inakwenda kujenga mochwari ya Hospitali ya Mwananyamala. Tunapaswa kurudisha sehemu ya mali zetu kwa jamii, kuwasaidia wenye uhitaji na wenye matatizo ili na wao wawe na furaha kama sisi tunavyofurahi,” alisema Shigongo na kuwashukuru wote walioandaa semina hiyo.

PICHA NA DENIS MTIMA | STORY NA EDWIN LINDEGE


Loading...

Toa comment