
MKURUGENZI Mtendaji wa Global Group na Mwalimu wa Ujasiriamali, Eric Shigongo, leo amezungumza na wanafunzi wa kidato cha sita wa Sekondari ya Saint Joseph iliyopo eneo la Posta jijini Dar es Salaam na kuwapa mbinu za kufanya vizuri na kupata daraja la kwanza (division one) kwenye mtihani wao wa kuhitimu unaotarajiwa kuanza Mei 6 mwaka huu.

Shigongo alikuwa katika shule hiyo kwa ajili ya kuzungumza nao na kuwapa hamasa kabla ya mitihani hiyo ambapo aliwataka kujiandaa vyema katika mitihani hiyo ikiwa ni pamoja na kuondoa hofu na kujiamini kuwa wanaweza kukabiliana nayo.

Shigongo akiwapa wanafunzi hao kitabu chake kinachohusu siri ya mafanikio maishani.
Mambo mengine aliyowafundisha pamoja na kujituma ni kuwa tayari kuumia kwa ajili ya maandalizi ya mitihani hiyo.
“Mnatakiwa kujituma sana hasa hiki kipindi kifupi kilichobaki, najua kwenye kujituma kuna changamoto nyingi. Wakati mwingine unataka kujisomea na usingizi nao unajitokeza, au uvivu unajitokeza, hivyo mnatakiwa kuishinda hali hiyo,” alisema.

Jambo jingine muhimu alilowakumbusha katika kusaka ushindi wowote ni nidhamu.
Aliwataka pia kuweka nia ya kubadili historia za familia zao kwa kufanya mambo makubwa zaidi ya waliyofanya wazazi wao na kuwapa mfano kuwa iwapo baba aliishia digrii moja wao wapiganie kupata kuanzia digrii mbili.

HABARI/PICHA: RICHARD BUKOS / GPL


Comments are closed.