KAMPENI zikiwa zinaendelea kupamba moto katika jimbo la Buchosa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, mgombea ubunge kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Eric Shigongo, amewaahidi wananchi wa Kijiji cha Majengo, Kata ya Nyakasungwa, kuwaletea maendeleo makubwa zaidi jimboni humo.
Ametoa kauli hiyo jana Septemba 30, 2020, wakati akizungumza na wananchi hao akisema iwapo watampa ridhaa ya kuwaongoza atahakikisha kwa nguvu zake na za wananchi wanajiletea maendeleo hususani upande wa elimu ikiwa ni miongoni mwa vipaumbele vitakavyofanya Buchosa kupiga hatua.
“Kazi ya ubunge ni ngumu sana lakini nimeamua kuifanya kwa miaka mitano, nitawatumia, nitateseka kwa ajili yenu, tutaboresha elimu kwa hawa watoto wetu, wana uwezo mkubwa wa akili wakipata elimu bora, watalisaidia hili taifa na kuwasaidia nyie wazazi wao.
“Tuna eneo la mraba zaidi ya kilomita 6,000 na watu zaidi ya laki tatu lakini tuna High School moja tu, hatuna chuo hata cha VETA. Kila mtoto ana nafasi ya kufanikiwa katika hili taifa, chini ya uongozi wangu watapata elimu bora, ninaongea kama ninatania lakini ninajua ninachokimaanisha, tusifanye makosa tarehe 28, Oktoba, tukaichague CCM kuanzia rais, mbunge na diwani wa CCM. Hamtasikitika, nitajituma na mtaona matokeo yake,” amesema Shigongo.