Shikalo: Yanga nakuja baada ya Kagame

KIPA namba mbili wa Harambe Stars na Bandari ya Kenya, Farouk Shikalo ‘Wazza’ amefi chua kuwa, ilibaki kidogo tu asijiunge na Yanga, lakini sasa atatua baada ya kumalizika kwa michuano ya Kagame. Bandari hivi sasa inashiriki michuano ya Kagame ambayo inaendelea nchini Rwanda.

 

Kipa huyo ambaye tayari amekamilisha usajili wa kutua Yanga, amesema kitendo cha Yanga kusambaza picha zake akiwa anasaini kiliwakera Bandari na kutaka kukwamisha dili hilo.

 

Kipa huyo raia wa Kenya, aliingia katika msukosuko na klabu yake baada ya kuingia mkataba na Yanga akiwa katika kambi ya timu yao ya taifa nchini Misri walipokwenda kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) inayoendelea nchini humo.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, moja kwa moja kutoka Kigali nchini Rwanda, Shikalo alisema kuwa kama viongozi wa Yanga wangefuata ushauri wake basi tayari angekuwa ameshajiunga na timu hiyo.

 

“Unajua hilo Yanga wenyewe ndiyo wamechelewesha hilo jambo kumalizika baada ya mimi kusaini mkataba wa miaka miwili wakati nipo Misri na timu ya taifa, wao wakaachia picha ikawakera viongozi wangu.

 

“Tatizo kiongozi aliyekuja kule alikosea kuachia picha wakati nasaini na walikuwa wanajua bado nina mkataba wa miezi sita na Bandari, sasa mabosi zangu walipoziona zile picha ndiyo maana wakaja juu wakataka kugomea kama kusingekuwepo na busara ingekuwa shida.

 

“Nasubiri nimalize michuano ya Kagame huku Rwanda ndiyo nije huko kuungana na Yanga,” alisema Shikalo.

Loading...

Toa comment