SHILOLE ATAJA SIRI YA MAFANIKIO

Zuwena Mohammed ‘Shilole’

KUDORORA kwa fani za filamu na muziki nchini kumezidi kuwaongezea akili baadhi ya wasanii kwa kujiongeza na kujikita katika shughuli kadha wa kadha ili kumudu maisha yao ya kila siku, lakini pia kulinda heshima zao mbele ya jamii.  

 

Zamani ilikuwa nadra sana kumuona msanii akijishughulisha na kazi nyingine nje ya fani yake hiyo kwa kuwa ilikuwa inawatosheleza kuendesha maisha yao kama masupastaa tofauti na ilivyo sasa.

 

Miongoni mwa wasanii wa filamu ambao wamekuwa wakijishughulisha na kazi nyingine nje na fani zao ni Wema Sepetu, Esha Buheti, Irene Uwoya, Jacqueline Wolper, Aunty Ezekiel, Haji Adam ‘Baba Haji’, Vincent Kigosi ‘Ray’ na wengineo wengi. Kwa upande wa wanamuziki, yupo Naseeb Abdul ‘Diamond’, Jux, Ambwene Yessaya ‘AY’ Faustina Charles ‘Nandy’, Zuwena Mohammed ‘Shilole’ na wengineo ambao kama si kuwa na maduka ya nguo na vipodozi, utawakuta wakiendesha biashara kadha wa kadha kama za vyakula na maduka ya vipodozi.

Katika makala haya ya leo, mwandishi amezungumza na Shilole ambaye ni miongoni mwa wakali wa muziki wanaofanya vizuri kwa sasa, japo alianzia katika filamu. Kabla ya kujikita katika muziki, Shilole alitambulishwa rasmi na tasnia ya filamu ambapo alijizolea umaarufu kutokana na umahiri wake katika fani hiyo.

 

Miongoni mwa kazi za kisanii zilizomtambulisha msanii huyo ni Filamu za‘Fair Decision’, ‘Crazy Of Love’, ‘Pigo’, ‘Bed Rest’, ‘Cut Off’ na nyinginezo, alizocheza na wasanii mahiri hapa nchini kama Ray, Johari, Rose Ndauka, Cloud, Thea, Mainda na Aunty Ezekieli.

 

Lakini kutokana na kile alichodai tasnia hiyo ya filamu kuvamiwa na baadhi ya watu wasiokuwa na vipaji na hivyo kuharibu soko, Shilole aliamua kubadili upepo na kuhamia katika muziki. Katika hilo, mwanadada huyo mwenyeji wa Igunga, Tabora, anasema: “Kuibuka kwa watu kila mmoja akijifanya msanii wakati hana kipaji, kuliitia doa sanaa yetu na kutufanya tuonekane waigizaji wote ni wababaishaji.”

Japo alikuwa na ndoto ya kufika mbali katika filamu kama alivyowahi kusema; “Ninataka kuwa ‘First Lady’ wa Bongo Movie,” mwanadada huyo alijikuta akiikacha fani hiyo na kutumbukia katika muziki. Tangu ametua katika muziki, Shilole amejikuta akijipatia umaarufu wa hali ya juu kutokana na jinsi alivyoitendea haki fani hiyo.

Akiwa ametoa nyimbo lukuki kama Chuna Buzi, Nyang’anyang’a, Kigori, Hatutoi Kiki, Malele, Nakomaa na Jiji, Say My Name, Paka la Baa na nyinginezo. Nyimbo zake hizo zimefanya vizuri na hivyo kumpa ‘madili’ ya kufanya shoo katika matamasha mbalimbali kama tamasha la Fiesta na hata kusafiri nje ya nchi kwa ajili ya maonyesha.

Lakini pamoja na yote hayo, Shilole aliamua kujiongeza ili kuendesha maisha yake bila kulegalega na hivyo kujikita katika ujasiriamali. Katika hilo, msanii huyo anajishughulisha na biashara kama ya mama ntilie akiuza na kusambaza vyakula na bidhaa mbalimbali kama Shishi Chili, vyote hivyo akivifanya chini ya lebo yake inayokwenda kwa jina la Shilole Entertainment.

Katika mahojiano na mwandishi wa makala haya mwishoni mwa wiki iliyopita, Shilole anasema kuwa alianza biashara zake hizo na mtaji wa shilingi 50,000 tu. “Nilianza biashara zangu na mtaji wa shilingi 50,000 tu mpaka hapa mnaponiona nimefikia kwa sasa, japo haikuwa rahisi kama mnavyodhani kwa sababu walikuwepo walionisema vibaya kwamba sitafika popote, wakunikatisha tamaa walikuwa wengi lakini namshukuru Mungu kwa kuwa maneno yao hayakufanikiwa.

“Nilihakikisha napambana kadri niwezavyo ili nifikie malengo yangu, nashukuru leo hii wote waliokuwa wananisema vibaya wanayaona mafanikio yangu,”anasema.

 

Anaongeza: “Namshukuru Mungu ninaendelea vizuri na biashara zangu, nikiendesha maisha yangu bila kumtegemea mtu yeyote, hivyo nawashauri na wengine ambao wana ndoto yakuja kuwa wajasiriamli wakubwa, kwanza kabisa wasikate tamaa waamini katika malengo yao na pia waanze biashara na kidogo walichonacho siyo mpaka wawe na mtaji mkubwa mwisho wa siku watayaona mafanikio,” anasema Shilole

 

Pengine kile alichokisema Shilole kuhusu maisha ni kitu cha kuzingatiwa na kila mtu kwa sababu mafanikio hayaji kirahisi ni lazima mtu apambane na changamoto na kuzishinda.

Loading...

Toa comment