The House of Favourite Newspapers
gunners X

SHILOLE AWAPA SOMO WEMA SEPETU, UWOYA

Zuwena Mohamed ‘Shilole’

BAADA ya kuanika mjengo wake aliojenga maeneo ya Majohe, Dar, staa wa muziki wa Bongo Fleva, Zuwena Mohamed ‘Shilole’ ameibuka na kuwapa somo mastaa wenzake wa kike akiwemo Wema Sepetu na Irene Uwoya. Akipiga stori na Risasi Mchanganyiko, Shilole aliwataka mastaa hao wa kike kuacha maisha ya kuigiza mitandaoni ambapo wanaonekana wamependeza kwa kuvaa nywele zenye thamani ya shilingi milioni moja na zaidi huku wakiwa hawajafanya la maana litakalowasaidia maishani.

“Nawasihi wasanii wenzangu wote siyo Wema na Uwoya tu, wapambane na waithamini shilingi mia moja maana unakuta mtu ananunua nywele za shilingi milioni moja na hana hata kiwanja hebu jiulize hapo angenunua mifuko ya simenti angepata mingapi, jamani wasanii wenzangu jitahidini kufanya mambo yatakayowasaidia katika maisha ya mbeleni.

“Inashangaza sana kuona msanii anafariki msiba unaenda kufanyika kwa shangazi yake kwa sababu kuna nyumba nzuri, kwa nini tusijikwamue sasa hivi angali tuna nguvu ili baadaye tuwe na cha kujivunia jamani, inabidi tubadilike zama za kujianika mitandaoni na nywele za mamilioni zimepitwa na wakati,” alisema Shilole.

Mwanamama huyo aliendelea kueleza kuwa siri ya yeye kuweza kujenga mjengo huo ni kutokana na kuthamini kila shilingi anayoipata na aliamua kuachana na anasa za kijinga na maisha ya kuigiza mitandaoni.

“Hii nyumba nimejenga kwa fedha nyingi ambazo mpaka sasa sijui jumla ni gharama kiasi gani maana sijajumlisha na fedha hizo nilikuwa kila nikipata hela kidogo nanunua simenti au mchanga na vifaa vingine hivyo mpaka nikae chini niangalie risiti nianze kuzijumlisha.

“Namshukuru Mungu kwa hatua hii niliyofikia na akili aliyonipa kwani wapo watu wengi wanapata fedha lakini hawana hili wazo la kujenga na natarajia kuhamia mwishoni mwa mwezi huu, ” alisema Shilole.

STORI: Gladness Mallya, Risasi Mchanganyiko

Comments are closed.