The House of Favourite Newspapers

Shilole Humwambii Kitu Kwa Mapishi!

MAMBO vipi mpenzi msomaji wangu wa kolamu hii nzuri ya My Style? Hapa kazi ni moja tu; kuzungumza na mastaa mbalimbali kuhusiana na aina ya maisha yao wanayoishi kila siku ambayo naamini mpenzi msomaji wangu utapenda kuyafahamu.

 

Nyota wetu wa leo ni mwanamama mjasiriamali anayejua kuisaka pesa vilivyo, si mwingine bali ni Zuwena MohammedShilole’ au waweza kumwita Shishi Baby. Shishi amefunguka, hajaacha kitu kuhusu mlolongo mzima wa maisha yake ya kila siku kama ifuatavyo:

 

My Style: Kwa nini ulichagua kazi ya kupika na wakati kuna kazi nyingi sana za kufanya?

Shilole: Unajua kazi ya jiko ni kazi ambayo naipenda kabisa kutoka moyoni na siyo kwamba nimeijulia ukubwani.

 

My Style: Mastaa wengi wanapenda kujiremba kila wakati, je kwako sio shida maana wakati wote uko jikoni?

Shilole: Tokea niko mdogo nilikuwa napenda sana kupika mno na sijali niko vilevile, tokea asubuhi napiga kazi. Mambo ya kujiremba mpaka nitoke niende kwenye sherehe yoyote.

 

My Style: Ni kitu gani sasa unachopendelea hata kwa mitoko yako ya hapa na pale au harusi?

Shilole: Nafikiri unanionaga kwenye mitoko yangu, napigilia kwelikweli hata milioni siku hiyo naweza kuivunja. Lakini ukinikuta jikoni utadhani kama sio mimi.

My Style: Kwa upande wa manukato unapenda kutumia manukato gani?

 

Shilole: Kunukia ni kitu muhimu kwa kila mwanamke, hata kama ninashinda jikoni na moshi, lakini lazima ninukie vizuri kwa ajili ya mume wangu. Kuhusu gharama; mimi nikiwa na hela yangu nzuri nanunua pafyumu za bei tu, ila siwezi kusema ni za shilingi ngapi.

My Style: Unapendelea chakula cha aina gani?

 

Shilole: Napenda sana vyakula vya kiasili kabisa zaidi kama mlenda na ugali au wali maharage. Siku nikila hivyo roho yangu inatulia kabisa.

My Style: Nani alikufundisha kupika?

Shilole: Nyumbani kwetu ilikuwa ni lazima ujifunze kupika tena chakula cha watu wengi, ndio maana nimeweza hata sasa kusimama.

 

My Style: Muda mwingi upo kazini mpaka usiku, unapata muda kweli wa kukaa na watoto wako kuzungumza nao?

Shilole: Kwanza kabisa sina mtoto mmoja, nina watoto wawili ambao tayari wanajitambua hata wanapokuwa nyumbani wanajituma sana, na kingine kuna wakati napata muda wa kuzungumza nao mambo muhimu.

 

My Style: Unawezaje kulea watoto pekee yako bila baba zao? Na vipi mumeo wa sasa anazungumziaje kuhusu watoto wako aliowakuta?

Shilole: Naweza na nimeshaweza kabisa wala sikumbuki ya nyuma na mume wangu anawapenda sana watoto wangu, anawaona ni wanae tu.

 

My Style: Siku za hivi karibuni unaonekana kuongezeka unene kwa kasi, nini siri ya mafanikio?

Shilole: Ni kuridhika na maisha tu na si vinginevyo.

My Style: Na kuhusu kuongeza watoto wengine una mpango wowote?

Shilole : Ndio, mimi napenda sana ila bado tu sijabahatika, ila nikimpata nitafurahi.

My Style: Vipi mafanikio kwenye biashara yako?

 

Shilole: Mafanikio ni makubwa sana kwa sababu nimeweza kufanya vitu vingi sana kupitia biashara yangu tena vingi vya mafanikio makubwa.

My Style: Haya nakushukuru sana Shilole.

Shilole: Karibu tena wakati mwingine.

MAKALA: IMELDA MTEMA

Comments are closed.