The House of Favourite Newspapers

Shinikizo la damu husababisha

SHINIKIZO la juu la damu (high blood pressure) ni miongoni mwa maradhi yanayoendelea kuwapata watu wengi nchini na duniani kwa jumla. Kila siku idadi ya watu wenye maradhi haya ambayo yapo kwenye kundi la magonjwa yasiyo ya kuambukiza huongezeka. Ugonjwa huu jinsi ulivyo ni kuwa baada ya kuathiri mfumo wa damu husababisha madhara sehemu mbalimbali za mwili yakiwemo macho.

 

Kwa vile huanzia kwenye mfumo wa damu, madhara yake kwenye macho huhusisha mishipa ya damu iliyo ndani ya jicho, hususan sehemu ya ndani ya ukuta wa nyuma inayoitwa retina.

 

Kazi kubwa ya retina ni kupokea mwanga wenye taswira na kuubadilisha kwenye mfumo utakaowezesha taswira kusafirishwa hadi kwenye ubongo kwa ajili ya kutafsiriwa. Shinikizo la juu la damu husababisha kuta za mishipa ya damu kutanuka ikiwemo iliyomo kwenye retina.

 

Kadiri kuta za mishipa ya damu zinavyotanuka ili kukabiliana na ongezeko la msukumo wa damu kutoka kwenye moyo ndivyo inavyosababisha upenyo wa ndani ya mishipa hii ya damu kupungua. Kupungua kwa upenyo huu hupunguza kiwango cha damu kinachoweza kupita kwenye mishipa hii.

 

Upunguaji huu wa damu husababisha kiasi kidogo cha damu kufika kwenye retina. Kukosekana huku kwa kiwango kinachostahili cha damu ambayo hubeba virutubisho na hewa safi na kuipeleka kwenye chembe hai hufanya uchukuaji wa uchafu kwa ajili ya kuusafirisha mpaka kwenye ogani ambazo hufanya kazi ya kuuondoa ushindikane. Damu hii inavyopungua husababisha ukosefu wa virutubisho kwenye chembe hai zinazounda retina hivyo kusababisha retina kushindwa kufanya kazi yake sawasawa.

 

Matokeo yake kwa mgonjwa huwa ni kushindwa kuona
vizuri, yaani kupoteza uwezo wa mtu kuona sawasawa. Sababu kubwa ya kutokea kwa athari za shinikizo la juu la damu kwenye macho ni kupanda kwa shinikizo la damu. Madhara haya kwenye retina hutokea baada ya mgonjwa kuwa na shinikizo la juu la damu kwa muda mrefu, kwa miaka kadhaa.

 

SABABU ZA KUWA NA SHINIKIZO LA DAMU LA JUU

Mambo yasiyoweza kuepukika na mtu kupata shinikizo la damu ni pamoja na kuwa na umri mkubwa ambapo tatizo huongezeka mtu anapozidi kuzeeka, historia ya ugonjwa wa shinikizo la damu la juu katika familia na uvutaji sigara.
Mambo mengine yanayoweza kusababisha shinikizo la juu la damu ni unywaji pombe mara kwa mara na kupita kiasi, kutofanya mazoezi, mlo wenye kiwango kingi cha chumvi, mafuta mengi mwilini aina ya cholesterol, uzito mkubwa kupita kiasi, kupatwa na msongo wa mawazo, pia inasemekana Cafeini ambayo inapatika kwenye vinywaji kama kahawa na chai huchangia mtu kupata ugonjwa.

 

DALILI NA ISHARA ZA SHINIKIZO LA DAMU LA JUU Mara nyingi watu wenye shinikizo la damu la juu la damu hawana dalili na ishara ambazo ziko dhahiri tofauti na kuongezeka msukumo wa damu baada ya kufanya uchunguzi wa kawaida au wakati wa kuangaliwa afya kwa sababu nyingine za kimatibabu. Ingawa watu wengine wenye shinikizo la damu la juu huwa wanapatwa na maumivu ya kichwa hasa nyuma ya kichwa
mara nyingi nyakati za asubuhi, kizunguzungu, kelele masikioni, kutoweza kuona vizuri au matukio ya kuzirai.

 

MATIBABU YA SHINIKIZO LA DAMU LA JUU

Hatua ya kwanza kuchukuliwa endapo mtu amebainika kuwa na shinikizo la damu la juu ni kubadili mtindo wa maisha hususan katika mambo yote hatarishi na endapo tatizo hilo litaendelea bila mafanikio ndipo matumizi ya madawa ya shinikizo la damu la juu hutumika (antihypertensives).

 

Ili kujikinga inatakiwa kufanya mazoezi kwa ukawaida kama vile kutembea upesi kwa dakika hata 30 au zaidi kila siku, kutumia lishe bora ambayo inakuwa na matunda na mboga za majani kwa wingi, kupunguza kiasi cha chumvi kwenye chakula, kutumia dawa kama ulivyopewa utaratibu na mtaalam wa afya na si vinginevyo.

 

Pia acha kunywa pombe au ulevi wowote, acha kuvuta sigara na dhibiti msongo wa mawazo na mifadhaiko, lakini pia dhibiti kiwango cha kolesteroli. Kama una ugonjwa ni lazima kudhibiti ugonjwa huo kwa kufuata utaratibu sahihi wa mtindo wa maisha na matumizi ya dawa kama utakavyoshauriwa na mtaalamu wa afya.

 

TIBA YA MARADHI HAYA Hakuna dawa ya kutibu ugonjwa huu kabisa, lakini kuna dawa za kutumia kwa muda wote wa maisha yako ambazo zitakua zinapunguza presha ya macho yako. Dawa hizo ni zile za matone kama vile Timolol, lakini pia wakati mwingine kuna aina za upasuaji hufanyika kuweka matundu kwenye iris ili kuachia majimaji yanayoleta tatizo kupita na kupunguza presha ya macho. Mtu huwezi kuzuia maradhi haya, lakini unaweza kuzuia upofu kwa kuanza matibabu mapema na kuyafuatilia matibabu kwa umakini kama utakavyoelekezwa na daktari wa macho.

 

 

Comments are closed.