Shinikizo la Damu (Hypertension) – 4

Causes-hypertension-info-550x455Leo nitaelezea mambo yanayosababisha shinikizo la damu ili uyafahamu na matibabu yake.

Kama shinikizo lako la damu liko juu, ni muhimu kumuona daktari ili ufanyiwe uchunguzi wa kiafya.

Kipimo kimoja cha shinikizo la damu hakimaanishi kupatikana au kuugua ugonjwa huo, inabidi upimwe zaidi ya mara mbili.

Pima kwa kifaa maalum cha kupimia shinikizo la damu kinachoitwa Sphygmomanometer angalau mara tatu tofauti kwa wiki ili kuthibitisha kama una ugonjwa huo.

Vipimo vingine ni kuchunguza damu ili kufahamu wingi wa Cholesterol mwilini, pia kupimwa BUN na Electrolytes. Pia pima kipimo cha kuchunguza mkojo, ECG, Echocardiography na Ultrasound ya mafigo.

MATIBABU YAKE

Baada ya vipimo kuonesha kuwa mgonjwa ana shinikizo la damu matibabu hufuata ili kuzuia madhara yanayoweza kusababishwa na shinikizo la damu.

Kuna dawa mbalimbali zinazotumika kutibu shinikizo la damu kama dawa jamii ya Alpha Blockers, dawa jamii ya Angiotensin Converting Enzyme Inhibitor (ACEI), dawa jamii ya Angiotensin Receptor Blocker (ARB), dawa jamii ya Beta Blocker, dawa jamii ya Calcium Channel Blocker, dawa jamii ya Diuretics zile zinazopunguza maji mwilini au kuongeza mkojo, dawa jamii ya Renin Inhibitors na Vasodilators.

Ikumbukwe kuwa shinikizo la damu lisipotibiwa na kudhibitiwa husababisha madhara mbalimbali kama kiharusi, moyo kushindwa kufanya kazi, matatizo katika mshipa mkubwa wa damu ambapo ukuta wa ndani huchanika na damu kukusanyika katika ukuta wa mshipa huo, kushindwa kuona na pia huathiri ubongo.

USHAURI

Mbali na kutumia dawa tulizozitaja, tunashauri kuwa  tunaweza kuzuia na kudhibiti shinikizo la damu kwa njia tofauti ambazo ni:

1) Kula lishe bora na chakula kusichokuwa na mafuta mengi, na pia chenye madini ya potassium kitaalamu kinaitwa DASH diet ambacho ni maalumu kwa ajili ya kuzuia shinikizo la damu.

2) Kufanya mazoezi mara kwa mara, angalau nusu saa kwa siku.

3) Kuacha kuvuta sigara na kunywa pombe kwa wale wenye tabia hizo.

4) Kupunguza utumiaji wa chumvi nyingi katika chakula hasa ya kuongezea mezani (tunapaswa kutotumia zaidi ya gramu 1.5 ya chumvi kwa siku).

5)  Kupunguza msongo wa mawazo na kuhakikisha kuwa tunakuwa na uzito unaotakiwa kiafya kulingana na kimo, na kama tuna uzito uliozidi tunapaswa kupunguza uzito huo ili uwe katika kiwango kinachotakiwa

6) Kula samaki au kutumia mafuta ya samaki ambayo husaidia kupunguza shinikizo la damu, kwa wenye shinikizo la damu.

Tukutane wiki ijayo kwenye gazeti hili hili.


Loading...

Toa comment