The House of Favourite Newspapers

Shoga: Acha Kulilia Mapenzi, Pigania Wanao!

SHOGA leo najaribu kukufungua akili wewe mwanamke mwenzangu ambaye kila siku umekuwa ukilia kwa ajili ya mapenzi, kila kukicha unaumizwa na unayempenda.

 

Nimekuwa nikipata malalamiko mengi sana kuhusu wanawake wenzangu, kutelekezwa au kukimbiwa na wachumba au waume, ni kweli inauma sana, unakuta mwanaume umezaa naye watoto wanne lakini bado hajatulia.

 

Kweli ni tatizo na wewe mwanamke mwenzangu ulivyo dhaifu unaendelea kulia tu badala ya kupambana kwa ajili yako.

Hakuna mtu ambaye anaweza kufanikiwa kwenye magumu kama ataendelea kulialia badala yake anatakiwa ajue namna ya kuweza kuuvuka ugumu huo, shoga mapenzi au ndoa si lelemama ni vita hasa, kama ulikuwa hujui, huyo mumeo uliyenaye ndani kuna wanawake wengine wanne au zaidi nje, wanamtamani, wanataka wawe naye, sasa wewe unapokazana kulia bila kutafuta njia mbadala ndiyo hapo sasa utawarahisishia manungayembe wa mjini kumchukua.

Shoga ifike sehemu uache kulialia kwa ajili ya mapenzi, jaribu kufikiria watoto wanaokutegemea, huyo bwana mwenyewe uliyekuwa unamtegemea ndiyo hivyo ameshakutelekeza.

 

Mwanamke mwenzangu amka sasa, achana na mambo ya kulia kwa sababu mumeo au mchumba wako kakutelekeza, umelia imetosha, angalia namna ya kupambana kwa ajili ya maisha yako na mwanao au watoto wako.

 

Kulia na kuendelea kumuwazia mwanaume ambaye kakuacha na kapata mwanamke mwingine ni kuendelea kujisumbua bure, wewe pambana kwa ajili ya kuwasomesha watoto wako, pambana kuhakikisha unaweza kijisimamia katika maisha yako. Hata kama siku moja akirudi ajue kabisa kuwa unaweza kusimama na kuwapigania wanao.

 

Shoga, yangu hata kama umeteseka vipi na mapenzi au mumeo au mwenza wako, kaa chini fikiria upya kuhusu maisha yako. Nani kakwambia huwezi kuishi bila mwanaume aliyekuacha yeye mwenyewe?

Nani kasema kuwa ukiachwa na mwanaume basi huwezi kuolewa tena? Hata kama una watoto watano shoga yangu kama riziki yako ya kuolewa ipo ipo tu, hata kama itakuchukua miaka mingi lakini ikifika hakuna wakuzuia.

 

Mara ngapi umeshuhudia au kuona harusi za bibi na babu wakioana na wanaenda kuishi maisha mazuri na yenye raha na furaha kuliko hata ya wale walioana wakiwa vijana.

Kikubwa shoga yangu, ukimpata bwana, mshikilie, mtunze, mueleweshe, usichoke kumshauri pale unapohisi kuwa mwenendo wake unaenda mrama.

 

Shoga, ndoa kufika uzeeni siyo jambo la mchezo mchezo, ni mapambano hasa ndani ya nyumba. Mara vile mara hiki lakini mwisho wa siku utafika ukiwa kwenye ndoa yako na mengine itakuwa ni simulizi kwa kizazi chako.

Muheshimu mumeo mwanamke mwenzangu, hata kama amekosa angalia namna ya kumueleza ili kama kweli kakosea, baadaye akiwa peke yake ajilaumu na kujirudi mwenyewe.

 

Kwa leo mwanamke mwenzangu, yangu ni hayo, bibie, nikutakie mafanikio na mapambano mema kwenye ndoa yako.

Kwa yeyote mwenye maoni na ushauri anaweza kunitumia ujumbe mfupi wa maneno (SMS), tafadhali usipige.

Comments are closed.