Shoga, kwa uweza wa Mola ni matumaini yangu kwamba hali yako ni nzuri na unaendelea kupambana na changamoto za maisha lengo likiwa ni kufikia kilele cha mafanikio.
Leo shoga yangu, nitawazungumzia wenzetu ambao hawajikubali jinsi walivyoumbwa na Mwenyezi Mungu hivyo kuamua kumkosoa jambo ambalo ni kosa na chukizo kwake.
Nasema ni chukizo kwake kwa sababu mtu anayekwenda kinyume na Mola wake lazima aadhibiwe ndiyo maana tunaona wanaoendekeza mambo ya uasherati kila kukicha wanaondoka kwa Ukimwi.
Ukiwaacha hao, wezi, majambazi na wahalifu wengine wanapoteza maisha kwa kuuawa au kutupwa lupango na kutumikia vifungo vinavyosababisha kuwaacha wazazi,watoto,wake na ndugu zao katika wakati mgumu.
Shoga, huo ni mfano tu wa madhara ya kwenda kinyume na maagizo ya Mungu lakini nikirejea kwenye mambo yetu ya chumbani zaidi, athari za wenzetu wanaomkosoa Mwenyezi Mungu aliyewapa ngozi nyeusi na wao kujikoboa kwa mkorogo zipo.
Moja ya athari hizo ni mume wa mwanamke aliyejikoboa kukosa msisimko na mkewe kwa sababu pamoja na tabia nzuri kilichomvutia mumewe hadi akamuoa ni rangi yake ya asili.
Mume anapokosa msisimko na mkewe ni wazi atatafuta mchepuko wenye rangi nyeusi kama aliyokuwanayo mke wake, huko atajiachia kwa raha zake na akinogewa atahama nyumba na kumuacha mkewe akiendelea kujikoboa mwili.
Shoga, hicho nilichokuambia kimewakuta baadhi ya wenzetu na hivi sasa wanajuta kwa nini walitumia mkorogo ulioharibu ngozi zao na kuwa kama vinyago visivyo na rangi maalum.
Athari nyingine ni kwamba wanawake wanaotumia mkorogo ni rahisi kupatwa na maradhi ya ngozi ikiwemo saratani, hivyo swali kwao ni hili; mumeo alikupendea rangi yako ya asili, sasa mkorogo wa nini?