The House of Favourite Newspapers

SHOGA: FENI HAIWASHWI UFUKWENI!

HALOOO eeeehhh tena ya kisoda! Ukinuna nuna mimi napeta, kula nala, kunywa nanywa na siku zinakwenda, upo? Shoga mwezi dume ndiyo huooooo unakatika! Kama nakuona vile unavyofurahia mwezi wa pili kuanza.

Shoga kuna mtu ananishika sikio eti mbona sisemi kina mama watu wazima wanaong’ang’ania kuzaa wakati watoto wao nao wameshaanza kuzaa. Tena ukikuta ndiyo msimu wa mavuno mama kachoka mtoto kachoka wanaombana udongo kama wavuta sigara, heeee heeeeiyaaaaa!

 

Kwa hili kwangu walaa la kawaida mwanamke kuzaa uwezo wako mpaka mayai yaishe tumboni, lakini nawe uwe na uwezo wa kuwatunza siyo uzae uwaachie walimwengu. Labda umegeuza methali asiyelelewa na mama hulelewa na dunia, jamani iweje raha zako ziwe karaha kwa wenzako. Tuachane na haya kwa vile yalikuwa kama matangazo ya biashara picha sasa inaanza.

 

Nazungumza na wewe mwanamke usiye na haya usiyejua wakati gani kwa kumkomoa mumeo, jamani wanawake wengine sijui tumerogwa na mchawi aliyeturoga kaugua wendawazimu sijui nani wa kutuponya.

Kuna kitu kimoja jana kilinikera na kunifanya niwarudishe kwenye unyago, nikiwa nakwenda zangu mjini nilipanda kwenye daladala na kukaa siti ya nyuma, mbele yangu kulikuwa na wanawake wawili ambao walikuwa wakiongea mambo ya ndani bila aibu, ndiyo maana nikajiuliza kama waliochezwa miaka mingi wamesahau mafunzo ya unyagoni itakuwa wewe unayewekwa masaa mawili mbele ya watu eti Kitchen Party.

 

Hivi kwanza wewe mwanamke, eeh jamani aibu umeiweka wapi kufikia hatua ya kuyasema maneno ya ndani mwako ndani ya daladala bila hata kugongwa na mshipa wa aibu.

Nilimsikia akisema eti alikorofishana na mumewe na kumsubiri kitandani ndipo alipomkomoa kwa kumkaripia alipomgusa na kumwambia eti. “Nikome”

 

Wewe mwanamke ndivyo mlivyofundishwa unyagoni kumfanyia mumeo kitandani pale mnapokosana. Unajua madhara ya kumnyima mumeo kata ya maji ukweni akiwa na kiu kikali.

Kibaya zaidi upumbavu ulioufanya unamweleza rafiki yako, pengine hata hajui ndoa ni nini, majibu yake mepesi. “Shoga tena mkomeshe wanaume wamezidi.”

 

Hizi ndizo moja ya sababu za kumfanya mumeo atembee na mfanyakazi wa ndani, pengine kafikisha umri wa kutumwa sokoni akarudi.

Wewe umekataa pengine wiki akijua unamkomoa, mwanaume hakomolewi shoga, tupo deiwaka kibao tunatafuta kazi hata ya masaa, telekeza gari deiwaka alikamate kama tajiri atakukumbuka.

 

Shoga labda nikung’ate tu sikio, ni kosa kufungua mahakama kitandani ni sawa na kuweka feni ufukweni kisha ukaiwasha, mwenzio anataka wewe ndiyo unaanza “unajua,” ajue nini mpe haki yake mashtaka baadaye. Niliwaeleza, mtu hawezi kuongea huku anapiga chafya.

 

Kuna siku nitawapa kisa cha mchota maji kisimani huku akilamba asali, unajua nini alichofanya, asali yote iliishia jichoni badala ya mdomoni. Ndiyo maana nikasema kuchota maji kuna raha kwa nini ukatishe raha za mwenzako.

Unamnyima mumeo haja zake akamalize wapi, akipata nyumba ndogo inayomjali uanze kupiga kelele. Hebu wanawake tuache akili za kubebewa. Nakwambia hivi siku mumeo kakuudhi na bado kaja na kata yake kuchota maji kisimani, jua huyo hana ujanja kwako. Utamkomoa kivipi?

 

Siku hiyo shosti jitume ujuavyo mfanyie manjonjo ya kila aina, wakati akitoa sifa kwa uendeshaji wako mzuri wa mashua baada ya safari ndefu, hapo ndipo mpe kilicho moyoni mwako.

Lazima atajua kweli unamthamini pamoja na maudhi yote bado umempa penzi shatashata, lazima atajirudi, mwanaume kwa mwanamke sawa na mbuzi na kamba. Hawezi kwenda mbali ukimfunga mnyororo unamuonea, yangu yameisha tukutane wiki ijayo.

Ni mimi Anti Nasra Shangingi Mstaafu.

Comments are closed.