Shoga; hata ‘singlendi’ ni nguo za ndani, usimpe hausigeli kufua!
NAAM naam! Leo ni Jumanne nyingine ambapo naamini wasomaji wangu wote mmeamka salama u-salimini. Kama ni kweli namshukuru Mungu kwa ajili yenu.
UFAFANUZI KWANZA
Jumanne ya leo nimependa kuongea na wanawake wenzangu zaidi. Hii ni baada ya kupata ukumbi huu kwa mapana. Ndiyo maana umeona safu hii ya Love and Life ‘Mapenzi na Maisha’ na ile ya ‘Chumbani Zaidi’ imekuwa kitu kimoja.
TWENDE KWENYE MADA
Leo nazungumzia tabia ya baadhi ya wanawake wenzangu kuchagua nguo za kumpa msichana wa kazi ‘hausigeli’ kufua. Utakuta mama ndani asubuhi anamwita msichana wake, anampa suruali, mashati, fulana na sing’lendi anamwambia fua hizi huku akiacha ‘kufuli’ tu kwamba, atafua yeye mwenyewe.
SINGLENDI NI NINI?
Hapa nazungumzia singlendi zile ambazo akina baba huzivaa ndani ya mashati tu na si zile wanazovaa nje kama wanamichezo. Zile ambazo kazi yake sahihi ni kuziba sehemu kubwa ya kifua toka mabegani hadi tumboni. Ina mikono ya kukatisha mabega.
Vazi hili huwasaidia akina baba au wanaume kwa ujumla kusiriti mashati kulowa jasho inapotokea kuwepo kwenye joto kali. Lakini pia huchangia uimara wa vazi la nje katika mtoko.
NAFASI YAKE KUBWA KATIKA NGUO
Katika nguo wanazovaa wanaume, singlendi imewekwa kwenye kundi la ‘nguo za ndani’ au kwa lugha ya kigeni ‘under wear’.
Kwa akina baba mnaonunua nguo hizo madukani au kwa machinga, ukiangalia maandishi ya utambulisho kwenye karatasi wanazofungia, yanasomeka; under wear’.
KAMA NI HIVYO SASA…
Sasa tukirudi kwenye maisha ya majumbani mwetu, wewe mwanamke mwenzangu ni kwa nini umpe msichana wako wa kazi, nguo ya ndani ya mumeo ili akufulie? Maana hapa tumeona under wear si ‘kufuli’ tu, hata singlendi. Inamhusu vipi dada wa kazi kwa mfano?!
Tambua kwamba, kama una mazoea ya kumpa dada wa kazi singlendi za mumeo afue, basi mpe na ‘kufuli’ nazo afue kwani zote ni kufuli ambazo hatakiwi kuona na mahali pake sahihi ni chumbani tu.
Vinginevyo, anzeni mazoea ya kufua singlendi wenyewe ili kuwatunzia heshima waume zenu kwani wasichana wa kazi wanapofua nguo hizo na kuziona zimefumuka au kuchanika ni sawa na kuona kufuli ikiwa hivyo.
Mimi hata nguo nyingine za mume wangu nafua mwenyewe, msichana wa kazi hazimhusu kwani tabia ya kumwachiamwachia yeye iko siku mtajikuta mmekuwa wake wenza! Ohoo!
NA NYIE AKINA BABA ACHENI TABIA HII
Lakini nikija kwenu akina baba na nyie acheni tabia ya kuvaa singlendi mbele za watu. Utamkuta baba ameamka chumbani, anavaa bukta na juu singlendi halafu anatoka mpaka nje, wengine mpaka dukani kwa Mangi. Hapo mjue ni sawa na mtu aliyetoka nje akiwa amevaa kufuli tu bila bukta na kuanza kuzurura, aibu gani hiyo!
KWA NINI NIMESEMA?
Nimeona niliseme hili kwani mimi najifunza mambo mengi kila kukicha ndiyo maana kwenye kazi zangu za u-MC, hata wa Kitchen Party huwa najua namna ya kuwafunda warembo wanaokwenda kuanza maisha ya ndoa ili kuepukana na tabia kama hizi!
Kwa leo niishie hapa, asanteni wote kwa kunisoma.