The House of Favourite Newspapers

SHOGA JEMBE LAKO, AKULIMIE NANI?

HE he he heeeeiya, acha nicheke miye Anti Naa mwana wa mashabiki, mjukuu wa maiki! Shoga hivi unajua kuna vitu vinachekesha kama siyo kusikitisha ati? Mwanamke mwenzangu mzima unalalamika kuzidiwa kete na hausigeli inahu? 

 

Loo! Ona sasa nimesahau hata kukusalimu shoga yangu wa ukwee hawa watu ujue wanakera? U mzima wewe siyo unanitumbulia macho kana kwamba hunijui, unataka kunisoma bila kujua maandishi nayo yanamuandikaji wake, upo?

 

Lakini twende mbele turudi nyuma, shoga yangu hali ya hewa hii kwa tunaoishi kwenye hili jiji la Dar hata haitabiliki mwenzangu! Unataka kufua unashindwa, unataka basi kwenda gengeni napo ni tope na maji, unataka basi kutoka out ndiyo kabisaa!

 

Hebu tuachane na hayo kwanza kwa muda tuingie katika mada ya leo maana inaniudhi kweli! Mwenzenu sijui nipoje, nikisikia jitu zima linalalamika kuzidiwa kete na hausigeli naliona kama limewasha moto ndani ya nyumba halafu linakimbilia kwa majirani walisaidie kuuzima, halooo ehhh!

 

Halafu sasa ukute jitu hilo ndilo limemuajiri lenyewe hausigeli mwenye umbo kuzidi yeye, jicho kungu kama siyo kokwa la embe, guu ndo kabisa kama siyo wa Iringa basi Mbeya maana supu si supu hata lile wanalosema la bia hili litakuwa la shampeni kabisa halafu analalamika; ‘ohh nisaidie Anti Naa’ kajisaidie mwenyewe na usafishe hicho choo kabisa! Shuuuuutuuuuu!

Hivi nawe tangu lini fisi akaachiwa bucha, wewe na mfanyakazi wako wa ndani mnazidiana nini kwa mfano? Kimaumbile, guu au nyonga?

 

Au pengine mfanyakazi wako Mungu kampendelea kuliko wewe. Unamwacha mfanyakazi wa ndani afanye kazi zote, kumsubiri mumeo wewe umelala akirudi amtengee maji ya kuoga wewe umelala, amtengee chakula huna habari unajigeuza kitandani, miguu unairushia dirishani kabisa, mbooona!

 

Anaondoa vyombo pengine amevaa upande wa kanga bila kitu ndani na kama anajua yupo katika mkao wa kula naye hufanya vibweka vya kuchezesha makalio, kuacha nido zake nje.

 

Sehemu hizo ndizo huwatoa imani wazee wetu na kujikuta wakijaribu kwa vile naye ana hamu zake ati ukichanganyia na kamvua haka ndiyo kabisssaaaaa! Basi shoga wee unalala watu wanajilia vyao. Ulikuwa wa kuamshwa usiku. “Honey leo nimeshikwa mwenzio.”

 

Unajikuta unalala kila siku bila kuguswa kutokana na uchovu wa kazi unaona sawa, kumbe nyani kaingia shambani wee wapiga usingizi mali zako zinaliwa. Leo na kesho mfanyakazi wako wa ndani anageuka mke mwenzio tena mapenzi yote mumeo anayahamishia kwake kwa vile ndiye anayemfanyia zaidi ya mke.

 

Shoga, jembe lako akulimie nani kwa mfano? Nataka nikueleze sheria za ndoa, kila siku naongea hapa hadi mwishoni nitakauka mate! Hata kama unafanya kazi gani hakikisha baadhi ya vitu hasa vimuhusuvyo mumeo, mfanyakazi wa ndani havigusi. Kufuliwa nguo, kutengewa maji ya kuoga, kula lazima ale mumeo ukiwa pembeni hata kama umeshiba basi mlishane hata tonge mbili siyo unamuacha hadi anahemewa, hilo nalo neno ati!

Mumeo ni lulu isiyotaka kuguswa na mtu, itunze kwa nguvu zako zote, hakikisha hakuna mtu atakayeigusa hata shoga yako ila wewe mwenyewe. Mfanyakazi ana mipaka yake wala asiwe na mazoea ya kuvuka mipaka na mumeo.

 

Narudia, wewe na mfanyakazi hampishani kitu, kila ulichonacho anacho, naye ana matamanio vilevile, anataka vitu vizuri. Kufanya kazi usijisahau na kuona kazi ni bora kuliko mumeo, kazi ina umuhimu kwa sehemu zake na ukifi ka nyumbani mwenye nafasi ya pekee ni mumeo kuhakikisha anapata huduma zote muhimu.

 

Kwa leo niishie hapa mwenzangu! Tukutane tena wiki ijayo! Kwa maoni na ushauri namba yangu hiyo hapo juu, tuma SMS tu!

Ni mimi Anti Naa Shangingi Mstaafu!

Comments are closed.