The House of Favourite Newspapers

Shoga: Maji ya Mchele Hayaonjwi!

0

 

KAMA nakuona vile jicho kodo kisa kuangalia eti leo MC Sophy atamchamba nani? Unikome, sipo hapa kumchamba mtu miye! Hapa unapata elimi bibi wewe kama ulikuwa hujui, upo?

 

Kwanza nikusalimu mwenzangu maana nikiaanza kutiririka utafikiri maji ya mtoni yameachiwa njia na kuingia kwenye makazi ya watu, shoga yangu u salama! Mwenzako kama ulivyoniacha nimejaa tele MC mimi, kama mgojwa basi ni jambo la kuombeana tu!

 

Tuingie kwenye mada yetu, jamani hivi muoaji wa kweli humuonja mwanamke ndipo amuoe kweli? Mmh! Simpendi jamani mwanamke mwenzangu kugeuzwa chungu cha mboga kuingizwa mkono na kuonja. Utaonjwa na wangapi mwisho wa siku unabaki kituko cha mtaa!

 

Juzi shoga nilipata malalamiko, msichana mmoja aliyefuatwa na mwanaume mtu mzima ambaye ni mume wa mtu na kumuomba awe mkewe kutokana na mkewe kuwa na matatizo ambayo siwezi kuyaanika hapa.

 

Kwa kweli mwari huyu alitatizika kuolewa ukewenza kuhofia kujiingiza katika vita ya ndani, lakini yule mwanaume alimuhakikishia kuwa kuoa mke mwingine alipata ruksa kutoka kwa mkewe. Mtoto wa kike kiguu na njia mpaka kwangu na kuniuliza akubali au akatae, loo! Kwa vile najua ukewenza si dhambi nilimweleza akubali.

 

Baada ya hapo tulipotezana na kuonana juzi akiwa anatokwa na michozi tikwatikwa kama majeruhi wa mafuriko. He! Mwari kulikoni? Nilimuuliza, jibu eti tangu wakati ule ndoa imekuwa kitendawili, kauli ile ilinishtua na kuuliza bado anaye? Jibu, ndiyo. Nilishangaa kasi ya awali na kuamini ndoa ingekuwa ndani ya wiki, lakini umevuka mwaka upo tu!

 

 

Mtoto wa kike niliinama chini kuwaza na kuwazua ili kutaka kujua sababu ya mwari wangu kuiona ndoa kama daladala inayopita mbele yake kwenda na kurudi. Kwa vile mimi ni ng’ombe mzee niliyepita mazizi mengi nilipata jibu na kumuuliza.

 

Tangu wakati ule umeshamuonjesha mwili wako? Jibu lilikuwa lilelile nililowaza kuwa alimpa baada ya msimamo wa muda mrefu na kuamini kumvulia nguo ingeharakisha ndoa kumbe siyo. Siku zote huwa sipendi kumlaumu mtu kwa kosa alilolifanya kwa bahati mbaya, lakini huwa simpendi mtu anayerudia kosa moja mara mbili kama mnyama na mwisho wa siku aombe ushauri, haipendezi.

 

Jamani wari wangu, mimi MC wenu nimeamua kutoa elimu ya bure kupitia gazeti hili kwa nini msiichukue. Usiniangalie mimi, angalia ninachokueleza ambacho huwa ni faida kwenu. Jamani hebu basi tuwe na msimamo kujitoa kimwili si njia ya kuharakisha ndoa bali kujidhalilisha.

 

 

 

 

Mwanaume kama kweli anakupenda na kutaka uwe mwenza wake, kwa nini awe na haraka ya kutaka kukuonja kwanza? Sasa umeonjwa na kuonekana si mtamu ndiyo uachwe? Kwa mtindo huo utaonjwa na wanaume wangapi shoga wewe! Kama ulikuwa hujui mwenzangu, maji ya mchele hayaonjwi na ukilazimisha hutaiona ladha, upo?

 

Mila na desturi yetu Waafrika ni kuchunguza tabia ya mtu si kuujua utamu wake, jamani haya yametoka wapi kuonjwa ndipo uolewe? Umekuwa pombe ya kienyeji? Ehee heee heeeiyaaa! Hilo nalo neeno!

 

Nawaasa wanawake wanaojiandaa kuolewa au kuwa na wachumba wasitoe miili yao ovyo, kama wanataka kuitumia wataipata baada ya ndoa, lakini wakijiroga kuitoa basi wajue itakula kwao, watatumiwa na mwisho wa siku kutupwa kama makaratasi ya kufungia maandazi au vitumbua.

Naombeni niishie hapa, tukutane tena Jumanne ijayo.

 MC Sophi:  Uwazi |Mapenzi & Maisha (Chumbani Zaidi)

Maoni na ushauri: (0713 761 135).

Leave A Reply