The House of Favourite Newspapers

Shoga; mume wako mgonjwa, kwa nini umsaliti?

0

Shoga yangu, kwa mapenzi ya Mola ni matumaini yangu kwamba upo mzima na mapambano ya maisha yanazidi kusonga mbele.

Kama utakuwa unaumwa au mambo yako kukuendea vibaya nakupa pole lakini usihuzunike sana kwa sababu yote hayo ni sehemu ya maisha.

Leo shoga yangu nitazungumzia tabia ya usaliti inayofanywa na baadhi ya wenzetu dhidi ya waume zao ambao ni wagonjwa.

Nimeamua kutiririka na mada hii baada ya kuwashuhudia akina mama kadhaa ambao waume zao wamelala vitandani wakiteseka kwa maradhi wakiwasaliti bila aibu wala  huruma.

Kwa kuwa mmoja wa wenzetu hao ni mtu wangu wa karibu nilipomuuliza kisa cha kufanya hivyo wakati mumewe yupo kitandani, akaniambia kwa sababu ya kusumbuliwa na hisia za yale mambo yetu hivyo ameshindwa kuvumilia.

Shoga yangu, kauli hiyo ilinishangaza nikamwuliza angejisikiaje kama yeye ndiyo angefanyiwa hivyo, akasema asingejisikia vizuri lakini sasa afanyeje!

Huyo ni mmoja wa shoga yetu ambaye ameolewa na kuapa kuwa na mumewe kwa shida na raha lakini mumewe alipopatwa na maradhi ameamua kumsaliti tena na kijana mdogo kisa kuwakwa tamaa ya mwili.

Shoga yangu unayemsaliti mumeo, hivi ni kweli unainjoi kufanya kitendo hicho wakati umemuacha mwenzako kitandani akiwa taabani kwa maradhi?

Kufanya hivyo ni dhambi na usipoacha lazima Mwenyezi Mungu atakuadhibu kwa sababu hakuna wakati ambao ni muhimu kwa wanandoa kuwa pamoja kama wa matatizo hususan maradhi.

Kama mumeo amepatwa na maradhi yanayomfanya ashindwe kushirikiana nawe kwa mambo ya chumbani zaidi, shirikianeni katika tiba ili apone muendelee kufurahia mapenzi yenu kama zamani na siyo kumsaliti. Bye!

Leave A Reply