The House of Favourite Newspapers

Shoga, Ona Aibu kuwa jike shupa

0

Couple-in-BedKama kawa kama dawa, najua sasa hivi kila mtu yupo bize kwa vile kila kitu ni mwendokasi na mimi nawasalimia kwa salamu za mwendokasi, mu hali gani mabibi na mabwana. Kama ilivyo ada najua mmekaa mkao wa kula kutaka kujua Naa miye nawapakulia kitu gani. Jamani maneno yangu kama maji huwezi kuyakwepa usipoyanywa basi utayaoga, basi ndiyo mimi.

Jamani leo kuna kitu kimenikwaza kwa tabia ya wanawake kujigeuza majike shupa. Najua bado umebakia njia panda huyu jike shupa ni nani? Inawezekana kabisa mwanangu Nuh Mziwanda kafikisha ujumbe ambao leo nataka niwaweke kitako wanawake wenzangu kuwaeleza mwanamke anatakiwa kuwa vipi.

Jamani kumekuwa na tabia za baadhi ya wanawake kuwapiga waume zao hasa wakijua wamewazidi nguvu. Basi mwanamke kwenye nyumba anakuwa kama amejioa mwenyewe. Hii haipendezi hata kidogo mwanamke kugeuka jogoo ndani ya nyumba wakati jogoo halisi yupo.

Shoga nataka kuwaeleza wanawake wenzangu kuwa na nguvu kumzidi mumewe hakumbadilishi uanamke wake, utabakia yuleyule, siku zote haibadili chini kuwa juu na juu kuwa chini.

Hata ukimpiga lakini mwisho wa siku wewe ndiye unayekwenda chumba cha kujifungulia, hawaendi waume zetu pamoja na sisi kujigeuza jike dume bado tutaendelea kunyonyesha.

Basi ingekuwa kazi, kwa vile wanaume wengi wanatuzidi nguvu, ingekuwa wanatupiga na kutunyanyasa lakini wao ndiyo wamekuwa na upendo wa dhati. Sisi hata aibu zimehama kwa wanawake na kuhamia kwa wanaume.

Shoga hata uwe na mwili kama nyumba na mumeo mfupi kama Andunje, bado wewe ni mwanamke unatakiwa kumheshimu mumeo au uwe na pesa na mumeo hana kitu, bado haikubadilishi wewe kuwa juu ya mwanaume.

Hata vitabu vya dini vimetuelekeza kuwaheshimu waume zetu nao watupende. Hebu mwanamke mwenzangu kama una nguvu bado unatakiwa kumheshimu mpe haki ya kichwa cha familia ili nawe ufaidi raha ya ndoa.

Shoga kwa tabia zako angalia usije mpiga teke chura, hakuna mwanaume anayetaka kuwa chini ya mwanamke. Wapo wanaosali usiku na mchana kutafuta hata mwanaume suruali ili tu awe ndani ya ndoa na kuwa wadogo kama pilitoni. Lakini wewe unaona sifa kujisifu kwa wanawake wenzako mwenye akili hawezi kukusifia ujinga huo.

 

Yangu kwa leo yametosha nami naondoka kwa mwendokasi ni mimi Anti Nasra Shangingi Mstaafu. 

Leave A Reply