Shoga; ukizembea ukewenza utaingia nyumbani kwako!
Shoga, ni siku nyingine ya Jumanne ambayo tunakutana katika eneo letu hili tunalolitumia kuelimishana pamoja na kukosoana kuhusu mambo mbalimbali hususan mapenzi lengo likiwa kuziboresha ndoa zetu.
Kwa kuwa hilo ndiyo lengo haswa la kona hii, leo nimeamua kuzungumza nawe kuhusiana na matatizo ambayo hukumbana nayo baadhi ya wenzetu ambao wapo kwenye ndoa za mitala.
Kama wewe na mke mwenzako mnaishi kwa amani mshukuru Mungu kwani kwa ninavyoelewa kati ya ndoa kumi za mitala unaweza kukuta mbili ndiyo akina mama husika huishi kwa amani.
Nawapongeza akina mama waliowaruhusu waume wao kuoa mke wa pili kwa sababu maalum lakini nawapa pole wale waliojikuta wameingia kwenye ndoa za mitala kwa sababu ya kuzembea.
Shoga, nasema hivyo kwa sababu kuna baadhi ya shoga zetu wanazichezea ndoa zao kwa kutowaheshimu waume wao, kutowajali, wafujaji wa fedha na vitu vingine kama vyakula nk.
Ukiacha tabia hiyo, wenzetu hao huwawekea ratiba waume zao ya kukutana faragha yaani mpaka watake wao, sasa kwa tabia hiyo unafikiri kuna mwanaume anayeweza kuvumilia kama siyo kuamua kuoa mke mwingine na kumleta nyumbani na kujikuta umezalisha ndoa ya mitala?
Shoga yangu, hebu kuwa makini na fuata yote uliyofunzwa na kungwi wako wakati ukiolewa kwani ndoa za mitala hazina amani na ukizembea mumeo ataoa mke mwenye maadili ubaki ukilia kila kukicha.