Shoga; umeolewa zilipendwa wako wa nini?
Mambo vipi shoga yangu. Na kwa wewe Muislam umejiandaaje na mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani?
Baada ya salamu napenda niende moja kwa moja kwenye jambo ambalo nimeamua kuzungumza nawe leo kufuatia juzikati kushuhudia mwenzetu akifungashiwa firago kwa uzembe wake.
Niliumia sana nilipoelezwa kwamba shoga yetu huyo kaachwa na mumewe kisa kikiwa ni kuendelea kuchati na mpenzi wake wa zamani huku akiwa kwenye ndoa.
Kwa kuwa napenda kudadisi, nilimfuata na kumwuliza kiini cha kuamua kupigiana simu na kuchati na zilipendwa wake huyo akaniambia alikuwa na vitu vingi alivyompita mumewe.
Miongoni mwa vitu hivyo alinieleza kwamba alikuwa anayajua mapenzi, mcheshi na mara kwa mara alikuwa akimtoa’out’ na vizawadi vilikuwa havikatiki.
Kufuatia utetezi huo nilimwambia alikosea sana kwani alipaswa kujua kwamba alikuwa mke wa mtu na hakulazimishwa kuolewa naye isipokuwa kwa hiari yake.
Shoga yangu, ukishaolewa inabidi uachane na zilipendwa wako wa zamani hata kama alikuwa akikujali au kujiweza kimapenzi, yote hayo yabaki kuwa historia.
Hata kama mumeo hamfikii kwa baadhi ya mambo zilipendwa wako, huyo ndiye mumeo uliyeamua kuolewa naye mheshimu kwani kuendelea kuchati na zilipendwa wako ni kujitafutia balaa kama lililomkuta shoga yetu aliyefungashiwa virago. Bye!