The House of Favourite Newspapers

Shoga, usijiachie kivile kwa marafiki!

0

HABARINI za leo mashostito popote pale mlipo na ni tumaini langu kuwa mnaendelea vizuri na harakati wakati mwaka ukianza kukomaa. Ninafarijika sana kwa jinsi mnavyowasiliana nami kuonesha kujali na kupenda yale ninayochangia pamoja nanyi.

Kuna jambo moja la msingi sana ningependa tulijadili leo kwa sababu uchunguzi wangu umenionesha kuwa wengi wetu huwa hatutambui kama hili ni muhimu sana katika maisha yetu ya kila siku.
Ni kuhusu urafiki. Najua kila mmoja ana rafiki yake anayemuamini sana, ambaye mara nyingi huwa ndiye msiri wake kwa mambo yake, si unajua tena sisi wanawake wakati mwingine tuna vitu vya ajabu.

Mashoga wanaweza kuwa wanaishi mtaa mmoja au hata sehemu tofauti, lakini linapomfika mmoja, lazima amtafute mwenzake na kumsimulia mwanzo mwisho ilimradi apate uafadhali katika maisha yake.

Lakini kuna jambo moja ambalo hatulifahamu, kwani ni lazima tuweke akiba ya kile tunachowaambia wale ambao tunaamini ndiyo marafiki zetu na wasiri wetu.

Unamuamini shosti wako kiasi cha kumweleza kuhusu mambo ya chumbani kwako. Unazungumzia udhaifu au uhodari wa mume wako katika mambo yetu yale, kiasi kwamba unakuwa umejivua nguo kabisa.

Nikupe kionjo cha yaliyomkuta shosti wangu mmoja, alikuwa na rafiki yake akimweleza kila kitu cha nyumbani kwake, akaanza kumsifia mume wake jinsi alivyo hodari wakati wa ulaji wa chakula cha usiku, kiasi cha kumpagawisha sana.

Yule shosti licha ya kusifia uhodari, lakini pia akawa anamweleza kero anazopambana nazo kutoka kwa mumewe. Sasa hapo ndipo alipokosea, kwani yule shosti akaanza kumshawishi kuachana na mwanaume huyo kwa sababu anamharibia raha ya maisha.

Alimshawishi hadi akafikia wakati akakubaliana naye. Akamuacha mumewe. Basi maisha yakaendelea lakini baada ya miezi michache marafiki zake wengine wakamwambia kuwa mume wake anatembea na yule shosti wake!

Sikatai, tuwe na marafiki, lakini tuwe na mipaka ya nini tunawaambia na hata ikibidi kufanya hivyo tusijiachie sana, lazima tuache akiba ili kujilinda.

Leave A Reply