Shoga, Usipojitambua Utasema Umerogwa!

Haya jamani nimekuja miye mwenye maneno ya shombo, eti sina tofauti na harufu ya nguru, sina siri kama kitanda cha chuma kilichochoka ambacho wakati wa mambo yetu hasa mwanamke anapokukuruka kisawasawa, lazima majirani wapekepeke salamu watazipata na kesho kuwa gumzo la siku.

Leo tena nashuka kama kipanga, sisi wanawake wavivu ambao tukilala hatuamki mpaka waume zetu wamekwenda kazini. Si wa kumtengea maji si wa kumpigia pasi wala kuchagulia nguo ya kuvaa. Mpaka mumeo anaondoka hujui amevaa nguo gani amependeza au haikumpendeza, wewe unaupiga usingizi na kuamka saa nne, chumba kichafu vyombo vinang’ongwa na nzi halafu unasimama mbele ya watu unajiita mke wa mtu kweliiii?

Chukiaaa, hunitishi lazima nikwambie, mnatia aibu hakuna mwanamke aliyepitia mafunzo ya kike akafanya ujinga huu. Kweli kabisa kabla ya kuolewa ulifanyiwa kicheni pati na kupewa nasaha kuwa mwanaume anatakiwa kufanyiwa nini na nyumba inatakiwa iwe katika hali gani?

Mnaweza kusema nabwabwaja kwa vile mdomo nyumba ya maneno, lakini watu wengi wana siri nzito ndani ya nyumba za mashoga zao, kuna mwanamke kabisa kaolewa na ana watoto kibaya amepanga chumba kimoja, ukiingia ndani mwake kitanda hakijatandikwa, vyombo vichafu, chumba hakijafagiliwa na huyo ndiye yupo mstari wa mbele kuwasema wenzake vibalazani.

Ndiyo haohao wanaoshinda mpaka jioni bila kuoga, wananuka kikwapa kama mpiga debe anayeshinda juani bila kuoga.Najua nimewagusa baadhi ya watu na hata kujisemea moyoni, wao kuwa vile mimi inanihusu nini. Lakini ni haohao mambo yakienda kombo wanatafuta ushauri au kwenda kwa waganga kumtafuta mchawi kumbe mchawi ni yeye mwenyewe.

Leo nataka nitoe twisheni japo kwa wengine itakuwa ngumu, lakini naamini kabisa ukiifanya kwa makini utaona mabadiliko ndani ya nyumba yako.Wahi kuamka kabla mumeo hajaamka muandalie maji ya kuoga kama anapenda ya moto mchemshie, wakati anaoga muandalie kifungua kinywa chepesi hata chai tupu kama ni mapema sana.

Muandalie nguo za kuvaa za kwenda kazini ambazo tayari umezinyoosha ambazo wewe utaona kabisa zitampendezesha mumeo.Akiishavaa simama mbele yake muangalie kapendeza? Mtengeneze msifie ili ajisikie fahari kuwa nawe. Ngoja nikuibie siri hii ambayo wanawake wengi walioolewa hawajui sababu ya nyumba zao kuyumba na nyumba ndogo kuchukua nafasi.

Basi shoga nyumba ndogo zina heshima, zinajua kumjali mwanaume kama mtoto hata kama alikuwa na mawazo yote humtoka, kila sifa unazozijua na usizozijua husifiwa mwanaume.

Siku zote heshima ya mtu huanzia kwake kama hujiheshimu nani atakuheshimu? Kuwa mke wa mtu ni heshima ambayo leo wanawake wengi wanaitafuta kwa udi na uvumba lakini hawaipati. Lakini wewe umeipata unaichezea na kutojitambua. Namalizia kwa kusema mwanamke anayejitambua hujiheshimu, hujipenda na kukilinda alichokuwa nacho (ndoa).

Ni mimi Anti Nasra Shangingi Mstaafu.

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!


Loading...

Toa comment