visa

Sholo Aingia ‘Chimbo’ Kisa Shoo Pasaka Dar Live

Sholo Mwamba

PRESHA inazidi kupanda na kushuka kuelekea Aprili Mosi (Sikukuu ya Pasaka) ambapo mkali wa Singeli, Sholo Mwamba yupo ‘chimbo’ akijifua kukabili shoo bab’kubwa ya Usiku wa Mwisho wa Ubishi itakayofanyika siku hiyo, ndani ya Uwanja wa Taifa wa Burudani, Dar Live uliopo Mbagala-Zakhem jijini Dar.

 

Showbiz, limemtimbia Sholo Mwamba maskani aliyoweka chimbo maeneo ya Legho jijini Dar na kuzungumza naye mengi juu ya usiku wa shoo hiyo ambapo alisema, ameshamaliza kuweka suala la pumzi sawa na kilichobaki na kukinukisha ndani ya Dar Live.

 

“Nimeimis sana Dar Live, lengo hasa la kuingia chimbo ni kujiweka sawa, wenyewe mashabiki mmeona listi ya wakali watakaokuwepo kwa hiyo hii si shoo ya mchezo, mashabiki lazima uwaridhishe hata wakitoa kiingilio waseme kweli hii ilikuwa shoo,” alisema Sholo Mwamba.

 

Showbiz pia ilifanikiwa kumzungukia Man Fongo ambaye naye amejipanga vya kutosha kulikabili jukwaa la Dar Live na ameshasema kwa mara ya kwanza atazindua ngoma yake mpya ambayo hajaitaja jina kwa sasa.

 

“Najua wajanja wote lazima waje Dar Live na pia lazima wamkute Man Fongo wa kitofauti, njoo washtue na wengine kwani siku hiyo nitawaonesha Singeli inaimbwaje na inachezwaje huku nikizindua ngoma mpya ambayo nikiitaja sasa nitakuwa naharibu njoo ushuhudie,” alisema Man Fongo anayebamba pia na ngoma kibao ikiwemo Nani Asiyependa na Safi Tu.

 

Mratibu na Meneja wa Dar Live, Rajab Mteta ‘KP Mjomba’ aliongelea usiku huo kuwa, mbali na uwepo wa Sholo Mwamba na Man Fongo, jukwaa pia litawaka kwa burudani kutoka kwa mkali mwingine asiyeshikika kwenye Muziki wa Singeli, Dulla Makabila ambapo atatoa sapraiz ya aina yake kwa kupanda na mwandani wake, Tiko Hassan na kuimba pamoja Singeli.

 

“Singeli itakuwa imeteka ukumbi mzima, Dar yote itahamia Dar Live kwa saa kadhaa. Dulla Makabila atahakikisha kila shabiki anacheza na kuimba naye pamoja nyimbo zake zote kuanzia Haujaulamba ‘Utatoa Hutoi’, Demu Wako Namba Ngapi pamoja na Makabila,” alisema KP.

 

KP aliongeza mbali na uwepo wa wakali wa Singeli, kuonesha kuwa utakuwa Usiku wa Mwisho wa Ubishi, katika Muziki wa Taarab napo kutakuwa na makundi yanayotikisa kama vile Yah TMK pamoja na Jahazi Modern.

 

“Wale wapenda Muziki wa Pwani nayo hii si ya kukosa, Yah TMK jukwaani kuoneshana umwamba na Jahazi Modern na niwaambie tu, burudani hii ya mwambao itaanza saa mbili za usiku kisha itafuatiwa na burudani ya Singeli.”

 

Kiingilio katika shoo hiyo ya aina yake kitakuwa ni buku s aba yaani shilingi 7,000 huku michezo mbalimbali ya watoto ikiwemo kuogelea itafanyika kuanzia saa nne asubuhi hadi 12 jioni kwa mtonyo wa buku tatu yaani shilingi 3,000.

SHOWBIZ
Toa comment