The House of Favourite Newspapers

Shoo Nyepesi Kabisa Hii! Yanga vs Wolaitta Dicha Leo

YANGA ina saa moja na dakika 30 tu za kujenga heshima Afrika leo Jumatano saa 10:00 jioni watakaporudiana na Wolaitta Dicha mjini Awassa, Ethiopia ambako nyota wa Brazil, Ronaldinho alitembelea wiki hii.

 

Lakini hali ya kujiamini kwa Yanga ambayo kwenye mchezo wa awali ilishinda mabao 2-0 jijini Dar es Salaam, imewatia hofu Wolaitta ambao wanatumia njia mbalimbali kuwahamasisha mashabiki kumiminika kwa wingi kuwapa nguvu.

Kikosi cha Yanga.

Kwa hesabu zilivyo, ili Wolaitta iwatoe Yanga, inahitaji kushinda kwa mabao 3-0 kwenye mchezo huo. Lakini Yanga wakifungwa mabao 3-1 watafuzu makundi, wakifungwa mabao 2-0 wanakwenda kwenye mikwaju ya penalti. Droo ya aina yoyote Yanga anavuka pia.

 

Kitendo cha Yanga kuingia tu kwenye hatua ya makundi leo kinamaanisha kwamba watakuwa na uhakika wa Sh 336 milioni na Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) litapewa Sh 34 milioni bila jasho.

Kila Yanga wanavyozidi kusonga mbele zawadi itaongezeka na ikicheza tu fainali itakuwa na uhakika wa Sh 970 milioni, bingwa anabeba Sh 1.5 bilioni.

Yanga kwenye mchezo wa leo itakuwa na Papy Tshishimbi, Kelvin Yondani, Said Makapu na Obrey Chirwa ambao kwenye mchezo wa Dar es Salaam, hawakucheza wakitumikia adhabu ya kadi mbili za njano.

 

Mkurugenzi wa Ufundi wa Wolaitta, Habtamu Wolde ameliambia Championi Jumatano kwamba: “Tuna saa moja na dakika 30, tutapambana kama nyuki na tutacheza mpira wetu, hatutajali chochote. Hicho ndicho ninachoweza kukwambia.”

 

Kocha wa Yanga, Noel Mwandila ambaye uongozi umempa mikoba ya George Lwandamina aliyetimka, amewaambia mashabiki kwamba watafanya kazi iliyowapeleka na hawataangalia matokeo ya Dar es Salaam.

Kocha huyo ambaye ni mahiri zaidi kwenye mazoezi ya viungo alisisitiza kwamba; “Ninachoangalia ni kushinda kwanza hii mechi ya Jumatano, tuna akiba ya mabao mawili lakini haitoshi, lazima tushinde ugenini na tufuzu makundi, ni muhimu sana kwetu.”

 

“Hakuna namna nyingine ya kufanikiwa, lazima tupambane tuonyeshe uwezo wetu,” anasisitiza kocha huyo asiyependa mbwembwe awapo kazini.

Kwa mujibu wa vyanzo vya uhakika vya Championi Jumatano, Wolaitta Dicha wameahidiwa Sh 90 milioni kama motisha wakiiondoa Yanga na kuweka historia ya kucheza makundi.

 

Kama Yanga ikifuzu leo, itasubiri ratiba ya makundi ya Shirikisho Afrika ambayo droo itachezeshwa Jumamosi saa 10: 00 jioni jijini Cairo, Misri yalipo Makao Makuu ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf).

 

Mechi ya kwanza ya hatua hiyo itapigwa Mei 4, mwaka huu ambayo ndiyo siku ambayo Yanga ilikuwa icheze na Mbao FC. Kufuzu kwa Yanga kunamaanisha kwamba itakuwa na mechi sita za hatua hiyo ambazo zitawapeleka mpaka Agosti wakati msimu mpya ujao wa Ligi ya Bara utakuwa unaanza.

Comments are closed.