The House of Favourite Newspapers

SHUHUDIA MTAMBO WA KISASA WA ASALI

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu  nchini (TFS) Prof. Dos Santos Silayo (kushoto) akiangalia mitambo ya kuchakata asali iliyofungwa wilayani Manyoni mkoani Singida.

UFUGAJI wa nyuki katika mkoa wa Singida unatarajiwa kuongeza tija kwa wafugaji kutokana na kuanzishwa kwa mtambo wa kisasa wa kuchakata mazao ya nyuki wilayani Manyoni.

 

Mtambo huo wenye uwezo wa kuchakata lita 500 kwa siku umefungwa na Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS) kwa lengo la kuwa kitovu cha kuzalishia mazao ya nyuki kutoka kwa wafugaji na kutoka kwenye vituo.

Mtambo huo uliogharimu Sh. milioni 80 unatarajiwa kuondoa tatizo la ubora duni wa asali na nta katika ukanda huo na maeneo ya jirani.

 

Taarifa ya  Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa TFS, Tulizo Kilaga,  aliyoitoa jana kwa vyombo vya habari  imesema mtambo huo umefungwa katika kiwanda cha TFS lakini pia wafugaji wa nje wataruhusiwa kuchakata mazao yao.

 

Alisema kiwanda hiko kwa kiasi kikubwa kitategemea malighafi toka kwenye misitu ya Aghondi uliopo eneo la Itigi.

“Mtu akiwa na asali sasa anaweza kutuuzuia au kuchujiwa kwa gharama nafuu na kisha kwenda kuuza kwa wateja wake. Uwepo wa mtambo huu pia utasaidia kutunza mazingira kwa kuwa watakuwa na uhakika wa soko la asali yao, watafuga kwa wingi kwa sababu watakuwa wanapata asali nyingi,” alisema.

 

Kwa mujibu wa wake, katika uvunaji wa awali wafugaji wamefanikiwa kuvuna mizinga 459 kati ya 729 na kupata asali kilo 6,175  sawa na tani 6.175, ambazo ni  wastani wa kilo 13.45 kwa mzinga.

Meneja wa TFS wilayani Manyoni, Juma Mambo, alisema mtambo huo unaweza kuwasaidia kupata asali bora na hivyo kuwa na uhakika wa soko la ndani na nje. Alisisitiza kwamba mtambo huo unawezesha kuchujwa kwa asali nyingi, tofauti na ilivyokuwa hapo awali  ambapo ilikuwa ikibaki kwenye masega.

Comments are closed.