The House of Favourite Newspapers

Shule za Kiislam Kuteketea, Bakwata Yaomba Ripoti

0

MFULULIZO wa matukio ya shule za Kiislam nchini kuungua kwa moto, bado yanawatesa baadhi ya viongozi wa dini hiyo, kiasi cha kuvitaka vyombo vya dola kutoa haraka ripoti za uchunguzi.

 

Akizungumza na UWAZI kwa njia ya simu mwishoni mwa wiki iliyopita, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Shehe Hamis Mataka alisema:

 

“Yametokea matukio mengi ya ajali ya moto, lakini sisi tumekuwa tunaviachia vyombo vya usalama vifanye uchunguzi na kutupatia ripoti.

“Ingawa kwetu sisi majanga yanatokana na mapenzi ya Mungu, lakini mambo yanapozidi hasa kwa upande wa shule zetu tu, inabidi kufanyike uchunguzi.”

 

Alipoulizwa uchunguzi huo utachukua muda gani hasa baada ya matukio ya ajali za moto kuendelea kujitokeza na kugharimu roho za watu, Shehe Mataka alisema, wao kama Waislamu, wamefundishwa kuwa na subira.

 

Alisema, pamoja na uwepo wa subira, wanaviomba vyombo vya dola kukamilisha uchunguzi wake mapema ili kuweza kuchukua hatua za kuhami madhara mengine yasitokee.

 

Wakati Bakwata ikivuta subira za kupata ripoti za majanga ya moto yaliyoziandama shule za Kiislamu, wiki iliyopita wanafunzi kumi wa shule ya Kiislam ya Byamungu English Medium Primary School iliyoko wilayani Kyerwa mkoani Kagera, waliteketea kwa moto usiku baada ya bweni walilokuwa wamelala kushika moto.

 

Kufuatia tukio hilo, wito wa kufanyika uchunguzi ulitolewa na Rais Dk. John Pombe Magufuli, huku kukiwepo na taarifa kuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alishaunda timu ya kuchunguza ajali zinazoziandama taasisi za Kiislam, ambayo hadi sasa haijatoa ripoti yake.

 

Julai 18, mwaka huu, Shule ya Mivumoni Islamic Seminary iliyoko ndani ya Msikiti wa Mtambani, Kinondoni jijini Dar es Salaam, iliungua kwa moto.

Julai 17, mwaka huu Shule ya Sekondari ya Kinondoni Muslim, iliwaka moto ambapo Julai 4, moto ulizuka katika Shule ya Sekondari ya Kiislamu ya Ilala jijini Dar es Salaam na ulisababisha vifo vya wanafunzi watatu.

Mei 17, 2016, shule hiyo ya Ilala ilipata ajali ya moto, huku tukio jingine la moto likitokea katika Msikiti wa Mtambani jijini Dar, Agosti, 2014.

 

Aidha, majanga ya moto yamekuwa yakijitokeza sehemu mbalimbali nchini na kuzihusu taasisi za Kiislam, jambo ambalo Shehe Mataka anasema linazua hofu.

 

Naye Mkuu wa Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu nchini, Shehe Mussa Kundecha alipozungumza na UWAZI hivi karibuni kuhusiana na majanga ya moto kuziandama taasisi za Kiislam, alisema: “Inashtua sana.”

 

Wakati huohuo, Mufti Mkuu wa Tanzania, Shehe Aboubakar Zubeiry bin Ally, amewataka Waislam kote nchini kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho vyombo vya dola vinafanya uchunguzi kuhusiana na ajali za moto zinazotokea kwenye taasisi za Kiislamu.

 

Wanafunzi kumi waliopoteza maisha kwenye Shule ya Byamungu na ambao picha za majeneza yao zimetumika ukurasa wa nyuma wa gazeti hili ni; Alikani Ally, Samwel Mohamed, Edmundu Erickmass, Abubakari Ibrahim, Oputatus Richald, Alfa Alauni, Abubakary Yasin, Abimari Ibrahim, Adam Silaji na Shadidu Siraji.

 

Miili ya watoto hao 10 waliokufa kwa kuungua sana bwenini, vipimo vya vinasaba (DNA) vilifanywa ili kuwatambua kabla ya kuwazika.

HABARI; Na Mwandishi Wetu, Uwazi

Leave A Reply